Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia imetenga jumla ya Shilingi bilioni 10.7
kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato mkoani
Geita.
Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi
wa chuo hicho, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce
Ndalichako amesema ujenzi wa chuo huo unatekelezwa kwa kutumia fedha za
ndani.
"Nawapongeza viongozi wa Halmashauri ya Chato kwa
usimamizi mzuri kwani mpaka sasa mradi huu umefikia asilimia 78 huku
mkandarasi akiwa ameshalipwa asilimia 41 ya pesa yote jambo
linaloonyesha kwamba kuna fedha itabaki ambayo itasaidia kuongeza
majengo mengine," amesema Waziri Ndalichako.
Aidha, Waziri
Ndalichako amewataka Wakandarasi na Washauri Elekezi wanaofanya kazi za
Wizara ya Elimu kuwa wazalendo na kuacha kuongeza gharama za miradi
inayotekelezwa na wizara hiyo.
"Tumegundua katika mikataba mingi
malipo ya washauri elekezi yanalipwa kulingana na kiwango anacholipwa
mkandarasi hivyo kufanya mkandarasi kuongeza gharama na kutokukagua
vizuri miradi hiyo," ameelezea Profesa Ndalichako.
Waziri huyo
amesema Wizara inafanya mapitio hata kwa miradi iliyoishakamilika ili
kujiridhisha na gharama halisi za utekelezaji na kuwezesha kutoa fedha
zinazolingana na gharama na kuhakikisha miradi inakamika kwa viwango
vinavyotakiwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi
Robert Gabriel amesema ujenzi wa chuo hicho cha kipekee mkoani humo ni
mwendelezo wa mageuzi makubwa yanayoshuhudiwa katika sekta ya elimu kwa
kipindi cha uongozi wa serikali ya Awamu ya Tano.
"Chuo cha VETA
Chato kitakuwa cha kwanza chenye ubora wa juu katika kanda ya ziwa kwa
kuwa ni kikubwa na kitakuwa na karakana zenye vifaa vya kisasa ambavyo
vitawezesha vijana wa Chato kuwa na ujuzi na maarifa," amesisitiza
Mhandisi Gabriel.
Aidha, Mbunge wa Chato ambaye pia ni Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani ameishukuru serikaki kwa kujenga chuo
hicho na kuahidi kuhakikisha anahamasisha vijana wa Chato kujiunga
katika chuo hicho ili kupata ujuzi na maarifa ya kuwawezesha kushiriki
katika kukuza uchumi wa nchi kupitia viwanda.
Kalemani amemuomba
mkandarasi wa mradi huo kuongeza vijana wa Chato katika mradi huo ili
uweze kukamilika kwa wakati kama ilivyopangwa na hatimaye mafunzo yaanze
kutolewa Januari 2020.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras
Bujulu amesema mradi wa ujenzi chuo hicho ni miongoni mwa miradi 40 ya
ujenzi wa vyuo vipya vya ufundi stadi pamoja na upanuzi wa vyuo
vilivyopo lengo likiwa ni kutimiza azma ya serikali ya kuongeza
upatikanaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi na hatimaye kuongeza
udahili wa wanafunzi kutoka wanafunzi 200,000 ya mwaka 2016/17 hadi
700,000 ifikapo mwaka 2020.
"Mradi huu na mingine kama hii
inayotekelezwa nchini inachangia utekelezaji wa azma ya serikali ya
awamu ya tano ya kuhakikisha kuwa vijana wanapata ujuzi stahiki
utakaowawezesha kuajiriwa au kujiajiri ili kushiriki kikamilifu katika
kukuza uchumi wa viwanda," amesisitiza Bujulu.
Akitoa taarifa
ya Mradi huo Kaimu Mkurugenzi wa VETA Kanda ya ziwa, Michael Ikongoli
amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa majengo 27 ambayo ni pamoja na
madarasa, karakana, nyumba 4 za walimu, bwalo la chakula, jengo la
utawala na kwamba samani zote za Chuo hicho zitatengenezwa na Chuo cha
VETA Mwanza kwa gharama ya shilingi milioni 693.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...