Dar yatajwa kuongoza zoezi la uandikishaji, Jiji la Arusha laendelea kushika mkia
Charles James, Michuzi TV
JIJI la Dar es Salaam limetajwa kuongoza katika zoezi la uandikishaji wa orodha ya wapiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa huku Jiji la Arusha likiendelea kushika mkia.
Akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo amewapongeza wakuu wa Mikoa na viongozi wote kwa namna ambavyo wamekua wakihamasisha zoezi hilo.
Amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Arusha na Mkurugenzi wake kujitathimini kutokana na Jiji hilo kushindwa kufikisha lengo lililopangwa ambapo mpaka leo wameshindwa kufikia asilimia 50 ya uandikishaji.
" DC Arusha, Mkurugenzi, msimamizi wa uchaguzi wana jambo LA kujitathimini mpaka takwimu ya jana hawajafika asilimia 50 wako asilimia 37. Wengine ni Moshi lakini hawa wamefika angalau asilimia 51 wamefikia lengo kidogo. Wamejitahidi.
Halikadhalika Korogwe mjini wamejitahidi sana, kwahiyo Manispaa ya Moshi na Korogwe Mji wako asilimia 51 lakini Jiji LA Arusha kwa kweli viongozi wao wanapaswa kuongeza hamasa ili kufikia walau asilimia tulizojiwekea," Amesema Waziri Jafo.
Amewashukuru viongozi wa Kiserikali, Kisiasa na wadau wote kwa namna ambavyo wameshirikiana kuhamasisha zoezi hilo huku akisema uchaguzi huu unaweka historia ya kuwa uchaguzi ambao wananchi wanapata ujumbe wa kutosha na maandalizi yake yamekua makubwa zaidi.
Waziri Jafo amesema baada ya siku ya kwanza ya nyongeza baada ya zoezi hilo kuongezewa siku tatu idadi ya waliojiandikisha imeongezeka hadi kufikia Milioni 16.9 sawa na asilimia 74 ya lengo.
" Kwa mara ya kwanza tukumbuke uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014 malengo yalikua kuandikisha watu Milioni 18.7 lakini waliokua wameandikishwa ni Milioni 11.8 sawa na asilimia 63 ya lengo. Mwaka huu kufikia Oktoba 14 kabla ya ile nyongeza watu waliokua wameandikishwa ni Milioni 15.9 sawa na asilimia 68 ya lengo hivyo mtaona tulizidi hata uandikishaji wa mwaka 2014," Amesema Jafo.
Aidha Waziri Jafo amesema siyo kweli kwamba watumishi wa Serikali wamekua wakilazamishwa kujiandikisha kama ambavyo wanasiasa wamekaririwa wakisema bali kinachofanywa na Serikali ni kuhamasisha zoezi hilo na kutoa elimu juu ya faida za kujiandikisha na kwenda kupiga kura.
Ameitaja Mikoa iliyofanya vizuri kuwa ni pamoja na Dar es Salaam yenye asilimia 89, Pwani asilimia 86, Tanga wakiwa nafasi ya tatu. Kwa upande wa mikoa ambayo inashika mkia licha ya kufikia asilimia 50 ni Mkoa wa Kigoma wenye asilimia 57, Kilimanjaro asilimia 58 mikoa ya Arusha na Shinyanga ikiwa na asilimia 66.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake Dodoma wakati akitoa tathimini ya zoezi la uandikishaji wa wananchi kwenye orodha ya wapiga kura kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24 mwaka huu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...