RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali
Mohamed Shein amesema matumizi ya Vitambulisho vipya vya Mzanzibari
mkaazi (smart card) yataiwezesha serikali kuweka na kuhifadhi
kumbukumbu za matukio ya watu wote katika Daftari la Usajili na
Utambuzi. Dk. Shein amesema hayo leo katika uzinduzi wa Kadi mpya za Kielektronik ya
Mzanzibari mkaazi, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul
wakil Kikwajuni mjini Unguza.
Amesema matumizi ya vitambulisho hivyo yataisaida Serikali, taasisi na watu
binafsi kupanga vipaumbele vya utekelezaji wa shughuli mbali mbali zenye
mnasaba na huduma za maendeleo ya kijamii.
Aidha, alisema kuwepo kwa mfumo huo wa matumizi ya vitambulisho vipya kutaisadia serikali katika kuwatambuwa watu wanaostahiki kupata haki za
msingi , kama ilivyobainishwa katika Katiba ya Zanzibar ya 1984.
“Itawezesha kumtambua mtu anaestahiki kupata haki yake kama vile
malipo ya pensheni, haki za matibabu, kujiunga na masomo na
nyenginezo”, alisema.
Dk. Shein amesema, kutokana uwepo wa vitambulisho hivyo Serikali itapata urahisi
katika suala zima la ukusanyaji wa mapato hivyo kuimarisha huduma
muhimu za kijamii, ikiwemo afya, elimu, barabara pamoja na ulinzi na
usalama wa raia na mali zao.
Alieleza kuwa vitambulisho hivyo vimetengenezwa kwa teknolojia ambayo
sio rahisi kughushiwa, vikiwa na uwezo mkubwa wa kiusalama wa taarifa
za mtumiaji, akibainisha kutumika katika nchi kadhaa duniani.
Rais Dk. Shein alitowa wito kwa wakaazi wote wa Zanzibar waliofikia umri
wa miaka 18 kwenda kujisajili katika ofisi za Wakala wa Usajili wa matukio
ya Kijamii zilizopo katika Wilaya zote nchini, sambamba na wale ambao
bado hawajajiandikisha kufanya hivyo.
Aidha, amewataka watendaji wanaohusika na utayarishaji wa vitambulisho
hivyo, kuwa makini na waangalifu katika utoaji wake.
Vile vile aliwataka Wakuu wa Mikoa kusimamia vizuri taarifa za uhakiki wa
watu walioko katika maeneo yao, kuanzia ngazi za shehiya, wadi na Wilaya
ili kuhakikisha wanawatambua wananchi wao na taarifa zao zilizo sahihi.
“Ni muhimu mlifanyie mapitio daftari la wakaazi katika shehiya, ambalo
ndio msingi wa uthibitisho wa kujua taarifa za utambuzi na makazi ya watu
waliomo katika maeneo yenu”, alisema.
Dk. Shein amewataka wananchi kutambua jukumu la kuisadia Ofisi ya
Wakala wa Usajili wa matukio ya kijamii katika kutambuwa wakaazi wa
maeneo yao badala ya kuiachia jukumu hilo Ofisi hiyo pekee.
Aidha, aliwataka wananchi kuondokana na tabia ya kutumia njia za mkato
katika upatikanaji wa vitambulisho hivyo, akibainisha hatua hiyo imekuwa
chanzo cha kuibuwa rushwa.
“Naendelea kukunasihini watendaji wote wa Wakala wa Usajili wa matukio
ya kijamii Zanzibar, mfanye kazi zenu kwa uadilifu, uzalendo na
mfungamane na misingi ya haki na sheria pamoja na kufuata taaribu
zilizowekwa katika kuendesha Ofisi ”, alisema.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akipokea Kitambulisho kipya cha Kielektroniki (SMART CARDS) cha Mzanzibar Mkaazi kama ishara ya Uzinduzi rasmi wa Vitambulisho hivyo kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa,Serikali za Mitaa na Idara Maluum za SMZ Mhe.Haji Omar Kheir wakati wa hafla iliofanyika leo katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akimkabidhi Kitambulisho kipya cha Kielektroniki (SMART CARDS) cha Mzanzibar Mkaazi Mama Mwanamwema Shein mara baada ya Uzinduzi rasmi wa Vitambulisho hivyo uliofanyika leo katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akimkabidhi Kitambulisho kipya cha Kielektroniki (SMART CARDS) cha Mzanzibar Mkaazi Makamo wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Mohamed Gharib Bilali mara baada ya Uzinduzi rasmi wa Vitambulisho hivyo uliofanyika leo katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein akionesha kitambulisho chake kipya cha Kielektriniki (SMART CARDS) mara baada ya kukabidhiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein(hayupo pichani) wakati wa Uzinduzi rasmi wa Vitambulisho hivyo uliofanyika leo katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein alipokuwa akitoa hutuba yake Uzinduzi wa Kitambulisho kipya cha Kielektroniki (SMART CARDS) cha Mzanzibar Mkaazi katika hafla ya Uzinduzi rasmi wa Vitambulisho hivyo uliofanyika leo katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiangalia mfano wa Kitambulisho chake kipya cha Kielektroniki (SMART CARDS) cha Mzanzibar Mkaazi wakati wa Uzinduzi rasmi wa Vitambulisho hivyo uliofanyika leo katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar chini ya usimamizi wa Ofisi ya Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar.
Baadhi ya Wananchi wa waliohudhuria katika ya Uzinduzi rasmi wa Vitambulisho vipya vya Kielektroniki (SMART CARDS) vya Mzanzibar Mkaazi uliofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (hayupo pichani) katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar chini ya usimamizi wa Ofisi ya Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar.
Baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiwa katika Uzinduzi rasmi wa vitambulisho vipya wa Kieletroniki (SMART CARDS) vya Mzanzibar Mkaazi uliofanyika leo katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...