Na Mary Gwera, Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Naibu Wasajili na Mahakimu kutoruhusu maahirisho ya mashauri ya mara kwa mara bila ya sababu za msingi.
Akizungumza na Naibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wapya mara baada ya kuwaapisha Naibu Wasajili na kuwakabidhi nyenzo za kazi Mahakimu Wakazi Wafawidhi wapya mapema Oktoba 25, 2019 katika Ukumbi namba moja (1) wa Mahakama Kuu-Dar es Salaam, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa wana nguvu/mamlaka ya kuhakikisha kuwa mashauri yanakwisha kwa muda unaotakiwa.
“Nyie mna mamlaka ya kuwadhibiti Wapelelezi, Waendesha mashtaka kuhakikisha wanaharakisha kufanya upelelezi na kufuata sheria na taratibu zilizopo,” alisisitiza Mhe. Jaji Prof. Juma.
Aidha; Mhe. Jaji Mkuu aliongeza kwa kuwataka Maafisa hao wa Mahakama kuhakikisha suala la upelelezi unaofanywa na Polisi linafanyika kwa kutumia ‘video’ kama sheria inavyotaka.
Hali kadhalika, Mhe. Jaji Mkuu amewataka pia Maafisa hao kutumia sheria ya Makubaliano katika kesi za jinai ‘Plea-bargain’ ili kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani.
“Sheria hii ya makubaliano katika kesi za jinai kati ya upande wa mashtaka na mshtakiwa inatumika pia nchini Marekani na imeleta mafanikio katika kupunguza msongamano, hivyo sheria hii isiishie kutumika makao makuu pekee bali itumike katika Mahakama zote nchini,” alisisitiza Mhe. Jaji Mkuu.
Kwa upande mwingine, Mhe. Jaji Mkuu aliwataka Maafisa hao kutekeleza majukumu yao kwa kufuata misingi na taratibu za Kimahakama na Taifa kwa kuwa Taasisi imewaamini.
“Ninyi ni viongozi na mtambue kwamba ni injini ya Mahakama kwa aina ya kazi mnazofanya, ni muhimu kufanya kazi kwa kufuata kanuni za Maafisa Mahakama na vilevile ni wajibu wenu kuwaelimisha watumishi mnaowaongoza kujua maadili ya utumishi,” alisema Mhe. Jaji Mkuu.
Katika hafla hiyo, Mhe. Jaji Mkuu amewakabidhi nyenzo za kazi jumla ya Mahakimu Wakazi Wafawidhi wapya 10 naye Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewaapisha jumla ya Naibu Wasajili wapya 10 ambao wote wameteuliwa kwa lengo la kuongeza nguvu kazi ya utoaji haki nchini.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akizungumza na Naibu Wasajili wa Mahakama walioapishwa leo pamoja na Mahakimu Wakazi Wafawidhi waliokabidhiwa nyenzo za kazi. Aliwataka kuzingatia maadili ya kazi zao. Hafla hiyo ilifanyika kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam. (Kushoto) ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi na kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Beatrice Mutungi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akionesha kitabu cha maadili , wakati akizungumza na Naibu Wasajili wa Mahakama, walioapishwa leo na Mahakimu Wakazi Wafawidhi waliokabidhiwa Nyenzo za kazi kuhusu masuala mbalimbali ya utendaji kazi, likiwemo suala la kuzingatia maadili ya kazi zao. (Kushoto) ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi na kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Beatrice Mutungi.
Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Happyness Ndesamburo akiapishwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi kuwa Naibu Msajili.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimkabidhi Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe Silvia Lushashi nyenzo za kazi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimkabidhi Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe Daniel Malik nyenzo za kazi.
Baadhi ya Naibu Wasajili wa Mahakama waliapishwa leo na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wakifuatilia hotuba ya Jaji Mkuu (ambaye hayupo pichani).
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati (wa kwanza (kushoto) akiwa katika hafla hiyo na watumishi wengine wa Mahakama ya Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...