Na Karama Kenyunko, globu ya jamii.

WATU watatu wakazi wa jijini Dar es Slaam, leo Oktoba 25, 2019 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka matano yakiwemo ya kukutwa na ndege aina ya Tausi wa Ikulu
wenye thamani ya Dola za Marekani 1,500 sawa na Sh 3,44 4,150  pamoja na kujihusisha na mtandao wa uhalifu.

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi amewataja washitakiwa hao ambao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 116/2019 kuwa ni, David Graha, Mohammed Hatibu na Mohammed Ally.

Mbele ya Hakimu Mkazi, Vick Mwaikambo imedaiwa,  Juni Mosi 2015 na Oktoba 14, mwaka huu jijini Dar es Salaam, washtakiwa walijihusisha na mtandao wa uhalifu ambapo wanadaiwa kuratibu genge la uhalifu wakijihusisha na biashara ya ndege aina ya Tausi bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Katika shitaka la pili, Nchimbi amedai katika tarehe hizo washitakiwa walikutwa na ndege watatu aina ya tausi wenye thamani ya USD 1,500 ambazo ni sawa na Sh milioni 3.4 mali ya serikali bila kuwa na kibali.

Pia Oktoba 14, mwaka huu maeneo ya Mikocheni jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Ally alikutwa na ndege watatu aina ya Tausi wanaopatikana Ikulu, ambao aliwapata kwa njia zisizo halali huku katika shtaka la tano, washtakiwa i Graha na Hatibu katika tarehe hizo hizo walijipatia Sh 300,000 huku wakijua fedha hizo ni mazalia ya kosa la wizi.

Hata hivyo, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo waliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuzingatia kwamba mashitaka hayo hayana dhamana.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 7 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa walirudishwa rumande kwa sababu mashitaka hayo hayana dhamana.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...