Shirika
la Reli Tanzania – TRC pamoja na ‘Clouds Media Group’ (CMG)
wameadhimisha miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage
Nyerere kwa kufanya safari ya kihistoria kutoka Dar es Salaam kuelekea
Dodoma kwa kutumia treni ya Deluxe kwa lengo la kuenzi mawazo ya Baba wa
taifa ya kuhamasisha watanzania kuhamia makao makuu ya nchi jijini
Dodoma kwa kutumia usafiri wa treni hivi karibuni, Oktoba 2019.
Katika
safari hiyo Menejimenti ya Shirika la Reli Tanzania ikiongozwa na
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu
Kadogosa iliungana na timu kutoka ‘Cloud Media Group’, timu ya Tigo
Fiesta pamoja na wasanii zaidi ya 200 kuelekea Dodoma kuadhimisha miaka
20 ya Baba wa Taifa lakini pia kutoa burudani na hamasa kwa wananchi wa
mkoa wa Dodoma.
Licha
ya kujionea Vivutio kibao vya nchi yetu ikiwemo maajabu ya mto Ruvu
kwenye Safari ya kihistoria kati ya CMG na TRC, timu ya Tigo Fiesta 2019
imefanikiwa kujionea utendaji kazi wa wakandarasi waliopewa dhamana na
Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
kujenga Reli ya Kisasa – SGR kuanzia Dar e Salaam hadi Makutupora mkoani
Singida ambapo wasanii walitembelea Kilosa katika eneo ambalo handaki
refu zaidi nchini linajengwa.
Katika
safari hii ya kuadhimisha miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwl.
Julius K. Nyerere, TRC na CMG walihakikisha uwepo wa Mwl. Nyerere ndani
ya treni ambapo vitu kadhaa ambavyo vilipendwa na Baba wa Taifa
vilienziwa ikiwemo mchezo wa Bao ambao alikuwa akiupenda, hotuba zake
pamoja na vyakula pendwa vya Mwl. Nyerere navyo vilipikwa katika safari
hiyo.
Aidha
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli alionekana akifurahia mchezo wa Bao
na baadhi ya wafanyakazi wa CMG, naye ACP S.K Kulyamo, Kamanda wa Jeshi
la Polisi Kikosi cha Reli pia ni moja kati ya watu ambao siku ya leo
alikuwa kwenye safari ya treni kutoka Dar mpaka Dodoma kuhakikisha
usalama wa wasafiri, kubwa ni kuweza kuandika historia kwa kumuenzi Baba
wa taifa na kuweza kukumbuka kifo cha Baba wa Taifa ndani ya treni
ikiwa ni miaka 20 toka atangulie mbele za haki.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira
Mhe. Anthony Mavunde amelipongeza Shirika la Reli Tanzania kwa mapinduzi
makubwa yaliyofanyika katika kipindi kifupi pia amefurahi kuona wasanii
wengi wameingia Dodoma kwa kutumia usafiri wa treni na anaamini kwamba
wasanii wamefurahi, wamejifunza mengi na watakuwa mabalozi wazuri kuhusu
usafiri wa reli pamoja na Mradi mkubwa wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa.
Mkurugenzi
Mkuu wa TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa kwa niaba ya Shirika
amemshukuru Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kudumisha mawazo ya
Mwalimu kwa kuhamisha serikali mjini Dodoma na kuboresha miundombinu ya
reli ambayo ndio msingi mkuu wa usafirishaji nchini, pia amewashukuru
Naibu Waziri Mhe. Anthony Mavunde, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe.
Patrobas Katambi, timu ya CMG na wasanii kwa ujumla katika maadhimisho
ya miaka 20 ya Baba wa Taifa na amesema kuwa ana imani kwamba safari
hiyo iimesaidia kutunza historia kuhusu maisha ya Baba wa taifa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...