Wafanyabiashara wasafirishaji wa bidhaa za chakula na kilimo Kanda ya pwani wakifuatilia ufunguzi wa semina iliyoandaliwa na TBS, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwapatie elimu ya kusafirisha mazao hayo nje ya nchi bila vikwazo vya kibiashara.
Picha na Chalila Kibuda
Na Chalila Kibuda,Globu ya Jamii
WAFANYABIASHARA wanaosafarisha bidhaa za mazao ya kilimo na chakula katika Kanda ya Pwani kwenda nchi za nje wamepatiwa elimu kuhusiana na taratibu za usafirishaji wa mazao hayo pasipo kukumbana na vikwazo vya aina yoyote.
Awali wafanyabiashara hao walikuwa wanapata huduma hiyo kutoka kwa iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), lakini baada ya majukumu hayo kuhamishiwa kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), shirika hilo imebidi liwaandalie semina kwa lengo la kuwapa utaratibu ambao inabidi waufuate.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Yusuf Ngenya, Mkurugenzi upimaji ugezi wa shirika hilo, Mhandisi Johanes Maganga, alisema madhumuni ya semina hiyo ni kuwaelimisha kuhusiana na utaratibu wa usafirishaji bidhaa hizo unavyofanyika.
Alisema mzalishaji akishazalisha mazao yake anayotaka kusafirisha nje ya nchi, wao TBS wanamsaidia aweze kufanya biashara yake kwa urahisi bila vikwazo vyovyote.
"Kwa hiyo sisi kama shirika tuna kituo cha kuwahudumia hawa wafanyabiashara wanaopeleka bidhaa nje ya nchi kwa maana kwamba tuna taarifa zote za kule ambapo bidhaa zinakwenda, hivyo msafirishaji au mfanyabiashara akija pale tunaweza kumpa taarifa za kile kinachotakiwa na kila nchi, bidhaa inatakiwa iwe na kiwango gani.
Tunampimia bidhaa yake na kumpa cheti cha ubora kwa bidhaa ile ambayo anaipeleka," alisema Mhandisi Maganga na kuongeza;
"Akifika kule anakoipeleka na bidhaa ikawa na ile nyaraka ambayo inathibitisha kwamba imeishapimwa na TBS inakuwa ni rahisi bidhaa yake kuaminiwa inakokwenda."
Alisema wanafanya hivyo kwa lengo la kumrahisishia mfanyabiashara kufanya shughuli zake, aweze kufuata taratibu za usafirishaji bidhaa nje ya nchi kiurahisi.
Alifafanua kwamba kabla ya hapo wafanyabiashara walikuwa hawajui zile taratibu zinazotakiwa, kwa hiyo walikuwa wakipata shida.
"Kwa hiyo tumewaita hapa pamoja, tukae nao tuwaeleze ni jinsi gani ya kufanya biashara, watueleze matatizo na changamoto zinazowakabili na sisi tuwaambie jinsi ya kuweza kutatua hizo changamoto katika kusafirisha bidhaa kwenda nje," alisema Mhandisi Maganga.
Alipoulizwa changamoto ambazo wamekuwa wakikabiliana nazo wafanyabiashara hao, Mhandisi Maganga alijibu kuwa ni pamoja na kutokuelewa taratibu, hivyo kama mtu anataka kusafarisha bidhaa kwenda nje kama haelewi hizo taratibu anakuwa na mkwamo fulani kwenye hiyo biashara.
"Kwa hiyo baada ya hii semina itakuwa ni rahisi sana mtu kufuata utaratibu, anaweza kusafirisha biashara zake kwenda nje kwa urahisi zaidi kuliko ilivyokuwa mwanzoni," alisema.
Alisisitiza kuwa kabla ya bidhaa kusafirishwa kwenda nje, lazima ipimwe na ijulikane ubora wake na wanatumia vile viwango vya nchi ambako bidhaa husika inakwenda.
Kwa upande wa nchi za Afrika Mashariki, Mhandisi Maganga alisema wana soko la pamoja ambapo wameoanisha viwango, kwa hiyo bidhaa ikishapimwa Tanzania na ikapewa alama ya ubora na TBS, kwenye soko la Afrika Mashariki inaweza kwenda popote, hakuna anayeweza kuitilia shaka.
"Lakini ikienda nje ya Afrika Mashariki tunahitajika kuzipima hizo bidhaa kwa viwango vya nchi zinakokwenda kwa sababu taarifa zote ambako zinapelekwa tunakuwa nazo sisi," alifafanua Mhandisi Maganga na kuongeza;
"Tunaweza kumwambia mzalishaji ni kitu gani afuate ili kuondokana na vikwazo." Kuhusu upimaji wa ubora wa asali, alisema shirika hilo linafanyakazi hiyo na kwamba zipo kampuni ambazo zimepewa leseni ya ubora na zinafanyabiashara ya kupeleka asali nje, hazipati matatizo yoyote.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Udhibiti Ubora wa TBS, Gervas Kaisi, alisema lengo la kuwaita wasafirishaji wa bidhaa za kilimo na chakula ni baada ya mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2019 ambayo imeongezea TBS majukumu katika masuala ya usalama ya chakula na vipodozi kutoka iliyokuwa TFDA.
"Kwa hiyo katika miezi hii mitatu kunakuwa na hiyo sintofahamu ya wafanyabiashara wanaoshughulika na hayo mazao ya kilimo na chakula, tumeona ni vema tukaitisha semina ili tukatoa uelewa wa pamoja ili walio wengi hawa waweze kupeleka hiyo elimu namna gani iliyo rahisi kuweza kuthibitisha bidhaa zao za mazao ya chakula na kilimo na namna gani wanaweza kusafirisha mazao hayo kwenda nje ya nchi," alisema Kaisi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...