Wakati wa uzinduzi wa Baraza la Kumi na nne (14) la Michezo la Taifa, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe alitoa maelekezo ya kusimamia kwa karibu utendaji kazi wa Vyama na Mashirikisho ya Michezo nchini ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa vikifanya kazi bila kufuata utaratibu na hivyo kushindwa kuleta tija katika maendeleo ya michezo nchini. 

Katika kutekeleza maagizo hayo, Baraza la Michezo la Taifa lilitoa maelekezo kwa Vyama na Mashirikisho ya Michezo ya Taifa juu ya namna bora ya kutekeleza masuala ya Michezo hapa nchini katika Mkutano wake na Vyombo vya Habari, uliofanyika tarehe 25 Julai, 2018.

Lengo la Mwongozo huo lilikuwa kutoa maelekezo ya namna bora ya kusimamia uendeshaji wa masuala yote ya Michezo katika Vyama / Mashirikisho ya Michezo nchini ambapo tuliwataka viongozi hao kuzingatia vigezo vitatu (3) muhimu katika uendeshaji wa shughuli za Vyama / Mashirikisho ya Michezo nchini kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo. Mambo hayo ni pamoja na Vyama / Mashirikisho: 1) Kumiliki Ofisi na Anuani ya Makazi; 2) Kumiliki Akaunti za Benki; pamoja na 3) Kuaandaa Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Majukumu yao na Bajeti ya shughuli zao za mwaka. Mwongozo huo uliwataka Viongozi hao kutekeleza mambo hayo ndani ya kipindi cha miezi sita (6) tangu Mwongozo ulipotolewa, tarehe 25 Julai 2018.  

Baada ya kipindi kilichotangazwa cha miezi sita kupita, Baraza la Michezo la Taifa liliendesha zoezi la kukusanya taarifa katika Vyama /Mashirikisho juu ya utekelezaji wa Mwongozo huo na kubaini upungufu mkubwa katika utekelezaji wake. Taarifa iliyokusanywa katika Vyama / Mashirikisho sabini (70) vilivyosajiliwa katika ngazi ya taifa, ilibaini kuwa;  

Vyama / Mashirikisho kumi na nane (18) tu ndiyo vilivyokidhi vigezo vyote vitatu – vya kuwa na Ofisi ama za kumiliki wenyewe au za kukodisha, kuwa na Akaunti ya Benki, na kuwa na Mpango Kazi na Bajeti;  

Vyama / Mashirikisho thelathini na saba (37) vimetekeleza kigezo kimoja au viwili kati ya vigezo vitatu vilivyoainishwa na vyama / Mashirikisho kumi na tano (15) havijakidhi kigezo hata kimoja cha mwongozo uliotolewa na wala havifanyi shughuli zinazotarajiwa kwa mujibu wa Katiba zao.

Baraza linatoa pongezi kwa Vyama/Mashirikisho kumi na nane (18) kwa utii wao na kutekeleza maagizo kama yalivyotolewa kwenye Mwongozo huo. Ni matarajio ya Baraza la Michezo la Taifa kuwa vyama hivi vitatekeleza Mipango waliyojiwekea kikamilifu na kuhakikisha hesabu zao zinakaguliwa na kuwasilishwa kwa mamlaka husika.

Aidha, vyama hivyo vinatakiwa kuhakikisha vinaendelea kuboresha utawala bora ndani ya vyama, vinatekeleza matakwa ya katiba kikamilifu, kuhakikisha ushiriki wa timu zao katika mashindano ya kitaifa na kimataifa pamoja na kuwa na mipango ya kuibua na kuendeleza vipaji vya wanamichezo.
Rejea kiambatanisho (i) kwa orodha ya Vyama na Mashirikisho hayo.

BMT inatoa nyongeza ya muda wa siku tisini (90) kwa Vyama/Mashirikisho thelathini na saba (37) ambavyo vinakosa baadhi ya vigezo ambavyo vilianishwa katika Mwongozo wa Uendeshaji wa Shughuli za Michezo kama ulivyowasilishwa kwao mnamo tarehe 25 Julai, 2018.  Kutokutekeleza kwa wito huu kutavipelekea Vyama/Mashirikisho hayo kufutiwa Usajili wake kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Usimamizi wa Michezo nchini.  

Pia Baraza la Michezo la Taifa linakusudia kuvifutia usajili Vyama/Mashirikisho  kumi na tano (15) ambavyo havikidhi vigezo vyote vya mwongozo wala  kuendesha shughuli za michezo kwa kipindi kirefu. 
 Rejea kiambatanisho (iii) kwa orodha ya Vyama na Mashirikisho hayo.

Vyama na Mashirikisho ya Michezo yatafutiwa usajili wao kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa Kifungu cha 16 (1) (d) na 17 (1) na (2) ambavyo vinampa mamlaka na utaratibu Msajili wa vyama vya Michezo kuvifutia usajili Vyama/Mashirikisho ya Michezo ambavyo vimeshindwa kukubaliana na masharti ya Sheria hiyo. 

Vyama/Mashirikisho ya Michezo ambayo hayajakidhi Kigezo hata kimoja cha Mwongozo (Vyama vinavyofutiwa usajili)
Chama cha Wanawake cha Michezo Tanzania (TAWSA)
Tanzania Pool Association (TPA)
Tanzania Squash Rackets Association (TSRA)
Physical Education Association (PEA)
Tanzania Karate Do-Federation Association (TKA)
Tanzania Badminton Association (TBA)
Chama cha Walimu wa Riadha Tanzania (CHAWARITA)
Tanzania Canoe Association (TACA)
Tanzania Weightlifting Federation (TWF)
Tanzania Scrabble Players Association (TSPA)
Tanzania Shooting Association (TASA)
Tanzania Rugby Union (TRU)
Tanzania Jump Rope Association
Tanzania Amateur Boxing Coaches Association
Tanzania Basketball Coaches Association

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...