Na: Moshy Kiyungi,Tabora.
Novemba, 2019.
Baada ya kung’atuka kwa Mkurugenzi wa bendi ya African Stars ‘Twanga ya Pepeta’, Asha Baraka ‘Iron Lady’, Luiza Mbutu amekabidhiwa ‘usukani’ kuendesha bendi hiyo.
Mbutu amedumu katika bendi African Stars ‘Twanga Pepeta’ kwa miaka zaidi ya 20. Kwa mujibu wa rekodi ya wanamuziki wa bendi hiyo, yeye ndiye mkongwe zaidi ya wengine waliopo katika bendi hiyo.
Akiwa na furaha tele usoni kwake, Luiza alisema kuwa amepokea kwa mikono miwili majukumu alliyokabidhiwa, akaahidi kuongeza mikakati imara na kuhakikisah bendi hiyo inaendelea kufanya vizuri.
Akionesha kujiamini kwa ayasemyo mwanamama huyo alibainisha kuwa wakati wa uongozi wake amepanga kuifanyia bendi yake mageuzi makubwa zaidi akishirikiana na wanamuziki wenzake kuhakikisha wanaibadilisha Twanga Pepeta, kuipeleka kwenye kiwango kingine cha maendeleo.
Mbutu amesema mipango ipo mingi lakini akawaasa wanamuziki wa bendi hiyo kuwa na mshikamano wa pamoja.
Historia inaonesha kuwa bendi ya African Stars ilianzishwa July 01, 1994 katika Hoteli ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam. Baadaye wakaunda Kampuni ya African Stars Entertainment Tanzania (ASET).
Luiza Mbutu ni nani?
Luiza Mbutu wakati wote awapo jukwaani huonekana mithiri ya msichana mdogo mwenye uso wenye tabasamu lenye furaha muda wote wakati akiimba na kunengua.
Licha ya haiba pamwe na umbo lake dogo hulitumia ipasavyo kulipambisha jukwaa ikisaidiana na wanenguaji wenzake wa bendi ya Twanga Pepeta, humuongezea sifa lukuki.
Luiza ameeleza siri ya kutozeeka na kuchuja, ni kutokana na kutotumia vilevi na kufanya mazoezi. “Kutotumia vilevi ndio mambo yanayonifanya nionekane hivi nilivyo, kingine ni mazoezi. Mimi naimba, na kucheza, kwahiyo kucheza ni sehemu ya mazoezi” alisisitiza Luiza.
Mama huyu alianza kuonekana kwenye Luninga miaka ya 1990, alipokuwa akicheza na kuimba pamoja na mwanamuziki Chemundugwao, wimbo wa “Tulitoka wote Mahenge”
Wakati huo alijulikana kwa majina ya Luiza Nyoni, lakini baada ya kuolewa na Faiara Mbutu, ambaye pia ni muungurumishaji mashuhuri wa gitaa la besi, sasa anajulikana kama Luiza Mbutu.
Katika maisha ya ndoa yao, wamefanikiwa kupata mtoto wa kiume ajulikanaye kwa jina la Brain.
Wasifu wa Luiza unaonesha kuwa alizaliwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, jijini Dar es Salaam. Alipotimiza umri wa kuanza shule, alipelekwa katika shule ya Msingi ya Mkamba, Kilombero nje kidogo ya mji wa Morogoro, ambako alisoma tangu darasa la kwanza hadi la tatu.
Baadaye alihamishiwa katika shule ya msingi ya Mzinga, iliyopo Morogoro mjini na kusoma darasa la sita.
Luiza alimalizia darasa la saba katika shule ya msingi ya Mushono, iliyopo Arumeru mkoani Arusha.
Baada ya kumaliza elimu hiyo, alikwenda kujiunga na elimu ya sekondari katika shule ya Mabibo jijini Dar es Salaam.
Mbutu aliendeleza elimu yake kwa kujiunga na masomo ya utunzaji wa stoo katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kilichopo jijini
Dar es Salaam, akaishia kwenye kiwango cha Stashahada.
Hiyo ilitokana na kuwa kila alipokuwa akiongeza hatua, Karo nazo zilikuwa zikiongezeka wakati huohuo alikuwa akijisomesha mwenyewe pasipo msaada mwingine.
Hata hivyo aliweza kusomea masomo ya Kompyuta katika Chuo cha Msimbazi Centre, ambako aliishia hatua ya kuandaa kurasa za magazeti.
Fikra na mawazo yake yalikuwa ni kufanya kazi ya muziki, Luiza aliamua kwenda kujiunga katika masomo ya muziki yaliyokuwa yakitolewa na Kanisa la Katoliki la Mtakatifu Joseph, jijini Dar es Salaam.
Hapo alisoma msomo hayo hatua ya kwanza hadi ya tatu.
Kwa mujibu wa maelezo yake, kipaji chake cha kuimba kilianzia tangia akiwa shule. Alipofika darasa la nne akawa mwimbaji kwenye kwaya ambayo aliendelea na huduma hiyo.
Luiza Mbutu alisema kwa sasa ameacha kuimba kwaya, lakini anaweza kurejea kwenye kwaya kwa kuwa anaipenda sana.
Pamoja na yeye kuanza kuimba muziki wa dansi mwaka 1997, kwenye bendi ya Magoma Moto. Pia dada yake wa kwanza aitwaye Modesta Nyoni aliimba kwenye bendi ya Kalunde ya Deo Mwanambilimbi.
Hivyo mabinti hao wawili kati ya saba wa familia ya mwanajeshi Nyoni, ndio pekee waimbaji. Modesta ana watoto wake Rose na Joseph, ambao wamerithi mikoba hiyo ya uimbaji wakifanya kazi katika hoteli tofauti.
Sifa kubwa ya Luiza Mbutu ni ile ya kutokuhama kwenda bendi nyingine kama wafanyavyo wengine. Tangu alipoingia katika bendi ya Twanga Pepeta, mwaka 1988 akitokea Magoma Moto Sound, hajawahi kuhama hata mara moja.
Bendi ya Magoma Moto Sound ilikuwa ikimilikiwa na mwenye hoteli ya Travertine, iliyopo Magomeni Mapipa jijiini Dar es Salaam.
Aidha Luiza alieleza sababu za kutotaka kuhama kwenye bendi hiyo, kwakuwa anapenda kuishi kwa kujifunza kutokana na baadhi ya wanamuziki ambao wakihama, baada kipindi kifupi hurejea tena katika bendi yao ya Twanga.
Amefafanua kuwa mwanamuziki anapohama hupoteza mashabiki, wengine kupotea kabisa katika tasnia ya muziki.
“Sikulitaka hilo niliamua kuwa kwenye bendi moja ambayo nimetulia nayo ukizingatia makubaliano yangu ya kimaslahi ninayapata, basi nimeridhika nayo.
Changamoto zipo kwenye bendi, lakini hupaswi kuzikimbia kwa kuwa hazikosekani hata kwenye nyumba tunazoishi, hiyo ndiyo siri ya kukaa Twanga Pepeta kwa miaka 20 mfululizo.” alitamka Luiza.
Katika kulelekea onyesho la bendi hiyo African Stars kutimiza miaka 20 ya mtindo wao wa Twanga Pepeta lililofanyikia Oktoba 20, 2018, jijini Dar es Salaam, Luiza alikumbuka mambo kadhaa aliyowahi kuyashuhudia kwenye bendi hiyo.
“Mimi ninamshukuru Mungu kwa kuniweka hai mpaka leo, kwa sababu kuna wenzetu wengi tulikuwa nao, lakini wametangulia mbele za haki.
Tungelipenda tunapokwenda kusherehekea miaka 20 ya Twanga , wangelikuwepo ila Mungu kawapenda zaidi, kwahiyo naomba Mungu awape pumziko la milele, amina” anasema Luiza Mbutu.
Alitamka kuwa tatizo jingine kubwa lililowakumba hadi kufika siku waliyotarajia kwenda kutimiza miaka 20 ya Twanga, ni lile la wanamuziki kuhama na kuifanya bendi iyumbe, lakini anadai kuwa huwezi kuzikwepa changamoto hizo kwenye bendi au makundi.
Pamoja na mafanikio aliyoyapata kutokana na bendi hiyo, hakusita kuusifia uongozi wa kampuni ya African Stars Entertainment Tanzania (ASET)
“Ninaukushukuru sana uongozi African Stars ‘Twanga Pepeta’ chini ya Mkurugenzi Asha Baraka, kwa kuendeleza kuidumisha bendi yao tangu ilipoanzishwa, Twanga Pepeta ambao ni mtindo wa bendi hiyo ndiyo ilitimiza miaka 20, lakini African Stars kama bendi ina muda mrefu zaidi” alisema Luiza.
Mambo mengine ambayo anayakumbuka walipokuwa wakielekea miaka 20 ya Twanga Pepeta ni kupata fursa ya kutembelea mbalimbali binafsi au na bendi yake.
“Safari hizo zimenifanya nijifunze na pia nimeweza kutembea na kuona vitu vingi, hivyo kupitia hilo kwangu ni kitu kizuri sana” alisisitiza Luiza.
Pamoja na mengine mengi kwa upande wa vitu vibaya ambavyo ilikuwa ni kushuhudia wanamuziki wanahama, akidai kuwa kilikuwa kikimpa mshtuko sana.
“ Nakumbuka marehemu Ramadhani Masanja ‘BanzaStone’ aliondoka Twanga na kwenda TOT, wakati huo tulikuwa tunaandaa albamu ya pili ya ‘Jirani’ akahama, haikuwa vyema japo alitupa funzo”
Luiza ghafla uso wake ulibadika na kuwa wenye huzuni kubwa alipokumbuka jambo jingine kubwa sana kwake ambalo hataweza kulishau ni kumpoteza kiongozi wao marehemu Abuu Semhando.
Semhando alikuwa Kiongozi,Babu, Meneja, Katibu wa bendi, aliyekuwa akituunganisha vizuri kati ya wanamuziki na uongozi wa bendi”. Aliseme Luiza.
Abuu Semhando alifariki dunia baada ya kupata ajali mbaya ya Pikipiki akitokea kazini usiku jijini Dar es Salaam.
Luiza Mbutu hadi sasa akipanda jukwaani huonekana ni mwenye furaha, mchangamfu akiwaongoza wanenguaji wenzake licha ya umri wake kuwa mkubwa, bado yupo kwenye ‘game’.
Kongole kwako kupitia makala hii, tunakutakia kila la heri katika kuliendeleza gurudumu ulilokabidhiwa.
Mwisho.
Mwandishi wa makala hii anapatikiana kwa namba: 0784331200, 0713331200, 0736331200 na 0713331200.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...