Waziri wa Nishati Dkt Medard
Kalemani (mwenye kipaza sauti) akizungumza na wananchi wa kijiji cha
Liuli wilayani Nyasa, mkoani Ruvuma, alipofika kuwawashia rasmi umeme,
Desemba 11, 2019.
**************************************
Veronica Simba – Ruvuma
Waziri wa Nishati Dkt Medard
Kalemani amewataka baadhi ya wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri za
wilaya ambao wamekuwa wakilalamika kuwa taasisi za umma katika maeneo
yao hazina umeme, waachane na malalamiko, badala yake watenge fedha za
kulipia huduma hiyo ili wapatiwe umeme.
Aliyasema hayo kwa nyakati tofauti Desemba 11, 2019 akiwa katika ziara ya kazi wilayani Nyasa na Songea, mkoani Ruvuma.
Dkt Kalemani alieleza kuwa, uzoefu
alioupata katika ziara zake sehemu mbalimbali nchini unaonesha kuwa
sababu ya taasisi nyingi za umma kutounganishiwa umeme ni viongozi wake
kutolipia huduma hiyo.
Alisema, wengi wamekuwa wakilalamika, lakini serikali inapofuatilia inagundua kuwa taasisi husika hazijalipia huduma hiyo.
“Wengi wao wanatenga fedha za ujenzi wa taasisi lakini wanasahau kutenga bajeti ya umeme halafu wanalalamika.”
Akitoa hamasa zaidi kwa viongozi
hao kutekeleza maelekezo yake, Dkt Kalemani aliwataka watumie fursa
iliyotolewa na serikali vijijini, ambapo gharama za uunganishaji umeme
zimeshushwa.
“Hata taasisi zitakazounganishwa
kwa mfumo wa njia tatu (three phase), bado gharama yake ni ndogo sana
ukilinganisha na inayotozwa mjini. Badala ya kulipia mamilioni, utalipia
laki na sehemu tu hivyo changamkeni.”
Katika ziara hiyo, Waziri aliwasha
umeme katika vijiji vya Liuli na Kihagala vilivyoko wilayani Nyasa
pamoja na vijiji vya Liganga na Nguvumoja vilivyoko wilaya ya Songea.
Aidha, pamoja na mambo mengine,
alisisitiza umuhimu wa taasisi za umma na miradi mbalimbali ya maendeleo
kupewa kipaumbele katika kuunganisha umeme ili ziweze kuwahudumia vema
wananchi.
Waziri aliwapongeza viongozi wa
maeneo hayo wakiwemo wabunge Stella Manyanya (Nyasa) na Jenista Mhagama
(Peramiho) pamoja na Wakuu wa Wilaya husika, Madiwani na wengine ngazi
ya halmashauri na vijiji, kwa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya umeme
bila kuchoka ili kuhakikisha wananchi wao wanafikiwa na nishati hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti,
baadhi ya viongozi hao, akiwemo Mbunge wa Nyasa Mhandisi Manyanya pamoja
na Mkuu wa Wilaya hiyo, Isabela Chilumba, wameipongeza Serikali kwa
kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme inayolenga kuboresha maisha ya
wananchi, hususan walioko vijijini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...