Katika mkutano wa Shirika la kazi Dunia (ILO) uliofanyika mwezi Julai 2019 ilielezwa kuwa ulimwengu wa ajira unapitia mabadiliko makubwa ambayo yanatokana na ubunifu wa kiteknolojia, mabadiliko ya demographia, tabia ya nchi na utandawazi.
Kutokana na mabadiliko hayo Shirika hilo liliamua kuwa na azimio la miaka mia moja ijayo ya ulimwengu wa (kazi) huku likiwataka nchi wanachama kuhakikisha kuwa watu wao wananufaika na mabadiliko hayo.
Kadhalika nchi wanachama zilitakiwa kuendeleza mahusiano ya kazi yaliyopo, ulinzi wa wafanyakazi, kuwezesha ukuaji wa uchumi jumuishi na kuhakikisha kunakuwa na kazi kwa watu wake, ajira za kudumu na kazi za staha.
Katika kutekeleza hilo ILO ilizitaka nchi hizo kuwekeza zaidi katika kuwajengea uwezo watu wake ili waweze kuendana na fursa nyingi zinazojitokeza kwa ajili ya ustawi wao.
Pia ILO ilizitaka nchi wanachama kuimarisha taasisi za kazi ili kudhibiti mikataba ya ajira, kupunguza umasikini, na kulinda ajira za baadaye kwa utu, usawa na kulinda uchumi.
Kadhalika kuwekeza katika maendeleo ya kazi endelevu na za staha na katika hili ILO ilisisitiza kuwa mabadiliko yanayoendelea yanaweza kuathiri uchumi na kazi hivyo mataifa yanapaswa kutoa kipaumbele kwa uwekezaji endelevu na wa muda mrefu ambao unatoa kipaumbele kwa binadamu na kulinda dunia.
Mbali na ILO kulimulika hilo suala mabadiliko hayo limekuwa ni tishio kwa ajira za wengi, wapo wanaodhani kuwa kwa siku zinavyozidi kwenda soko la ajira litazidi kuwa gumu kuliko sasa.
Jumanne Mtambalike ni Mkurugenzi na mwanzilishi wa Kampuni ya teknolojia iitwayo Sahara Ventures , yeye kwa taaluma ni mhandisi wa programu za Compyuta na sasa anasema teknolojia ndiyo kila kitu.
Anasema katika kada yake mtu apaswa kujifunza kila siku ili kuenza kuendana na kinachotokea ulimwenguni kwa kuwa teknolojia inabadilika kwa kasi naye anatakiwa kubadilika hivyo ni lazima atenge muda wa kujifunza.
Jambo zuri ni kwamba mambo mengine anaweza kuyapata mtandaoni na huko unaweza kujifunza vitu vipya kwakuwa kozi nyingi zisizo za kulipia lakini unaweza kujifunza vitu muhimu.
Anasema kutokana na mwenendo wa dunia hakuna budi kuwapa vijana ujuzi zaidi ya maarifa wanayoyapata shuleni, wanapaswa kuwa na fikra tunduizi na kuelewa namna ya kuchambua vitu sanjari na kufahamu namna ya kuwasiliana na kuchangamana na watu.
“Watu sasa wanapaswa kuwa na ujuzi wa vile vitu ambavyo kompyuta haiwezi kufanya, vitu ambavyo mashine haziwezi kufanya, hilo ndilo litakalowafanya waendelee kuonekana ni watu wa muhimu,” alisema.
Anasema miaka ijayo kazi nyingi zitachukuliwa na mapinduzi ya teknolojia lakini pia nyingine zinaweza kutengenezwa kupitia mapinduzi hayo suala la muhimu ni maandalizi ya kizazi ili kuweza kupata kazi hizo.
“Ukienda katika mtandao wa instagram sasa maelfu ya wanawake wanatumia jukwaa hilo kuendesha biashara zao, nafikiri sasa kinachohitajika sio ujuzi kwani kwa sasa kompyuta inaweza kufanya karibia kila kitu nadhani tunapaswa kufundisha zaidi ya mtalaa,” anasema Mtambalike
Mwingine ni Tulalana Bohela, mwanzilishi mwenza wa kampuni ya simulizi na teknolojia iitwayo Onastories anasema huwa anawaambia wanafunzi na wafanyakazi wenzangu kuwa google ni rafiki.
Anasema hatma ya kazi inakwenda kasi kwenye sekta tofauti akitolea mfano sekta ya uzalishaji ambayo ina nafasi kubwa katika kukuza uchumi lakini kuna kuhama kuelekea matumizi zaidi ya mashine kuliko watu na mashine zinajifunza na kufanya kazi kwa haraka, kuendana na mazingira kuliko mtu.
“Kwa kazi yangu mimi nafikiri mashine haiwezi kufanya kwa sababu inahusu zaidi mtu na roboti sidhani kama inaweza kufanya labda ipandikiziwe binadamu, tunapaswa kubuni shughuli ambazo haziathiriwi na mabadiliko hayo,” anasema.
Anaongeza kuwa kwa ujumla Tanzania bado ipo nyuma katika mapinduzi ya viwanda awamu ya nne na kuna wakati alizungumza na wanafunzi tofauti wakamwambia kuwa wanadhani kuwa mambo wanayojifunza shuleni ni mambo ya awamu ya pili ya mapinduzi ya viwanda.
“Nafikiri wanafunzi wanapaswa kuwa wanafundishwa namna mazingira yanavyobadilika, unaweza kufundisha mtu ujuzi wa ubunifu wa kutatua changamoto katika jamii, uwezo wa kujieleza, kujiamini, kupanga mikakati na sio kwa ajili ya waajiri wao bali wao wenyewe,”
Alisema hilo linapaswa kutiliwa mkazo zaidi kwa vijana ili wajua thamani yao ni kile wanachokizalisha kwa minajili ujuzi, fikra na ubunifu.
Aidha Utafiti mmoja uliofanyika nchini India mwaka huu na kuchapishwa na taasisi ya McKinsey Global unaonyesha kuwa mpaka ifikapo mwaka 2025 ajira milioni 45 zitakuwa zimepotea kutokana na mapinduzi ya teknolojia, hata hivyo utafiti huo unaonyesha kuwa zaidi ya ajira milioni 65 zitatengenezwa na mapinduzi hayo.
Vilevile ripoti ya jukwa la kimataifa la uchumi (WEF) ya mwaka 2018 unaonyesha kuwa kukuwa kwa teknolojia kutaondoa kazi zaidi ya milioni 75 hadi kufikia mwaka 2022 hata hivyo teknolojia itatengeneza kazi mpya milioni 133 katika kipindi kama hicho.
Ripoti hiyo iliyotokana na utafiti uliofanywa katika makampuni makubwa 313 duniani yanayotoa huduma tofauti inasema jambo hilo litatokana na namna ambavyo teknolojia itabadilisha namna ya ufanyaji wa kazi tofauti na ilivyokuwa awali.
“Takribani asilimia 50 ya kampuni zinatarajia mifumo ya teknolojia katika uzalishaji itapunguza nguvu kazi kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 22, mwaka 2018 asilimia 71 ya masaa ya kazi yanafanywa na binadamu huku asilimia zilizosalia zikifanywa na mashine. kufikia 2022 muda wa nguvu kazi utapungua hadi asilimia 58,” ilieleza ripoti hiyo.
Hata hivyo lengo la mabadiliko ya teknolojia ni kurahisisha shughuli mbalimbali na sio kuua ajira za watu na mpaka sasa tu teknolojia umeongeza kasi na ufanisi wa kufanya shughuli Fulani kwa kutumia mifumo ya kompyuta.
Mambo mengi hivi sasa yamerahisishwa mtu akiwa na simu ya mkononi ama kompyuta anaweza kufanya mambo mengi kwa urahisi akiwa sehemu moja kwa kubonyeza tu katika simu yake.Mfano huduma nyingi kama kuitisha usafiri, kufanya malipo ya miamala mbalimbali sasa inaweza kufanyika kwa kutumia simu ya mkononi kupitia huduma za kifedha zinazotolewa na kampuni za simu na taasisi za kifedha.
John Manase ambaye ni muhitimu wa shahada ya manunuzi na usambazaji anasema hofu ya ajira kutokana na teknolojia ni kubwa lakini kuna matumaini mapya kwani teknolojia hiyo imefungua fursa nyingine lukuki.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...