Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akipokea hundi ya kiasi cha Sh. Milioni
200, kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu
Tanzania (TOSCI), Bw. Patrick Ngwediagi, katikati ni Msajili wa Hazina,
Bw. Athumani Mbuttuka, wakati wa halfa ya kupokea gawio jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma wakati wa hafla
ya kupokea gawio la kiasi cha sh. Bilioni 12.12, kutoka kwa Taasisi
58 zilizotoa gawio kwa Serikali baada ya agizo la Mhe. Rais Dkt. John
Pombe Magufuli, alilolitoa Novemba 24, Ikulu jijini Dodoma.
Msajili wa Hazina, Bw. Athumani
Mbuttuka, akitoa taarifa ya kiasi cha fedha ambazo zimepokelewa kutoka
kwa Taasisi za Serikali ikiwa ni kuitikia agizo lililotolewa na Raisi wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa
Taasisi ambazo hazikuwasilisha gawio la Serikali Chamwino Ikulu jijini
Dodoma.
Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiteta jambo
na Msajili wa Hazina, Bw. Athumani Mbutuka, wakati wa halfa ya kupokea
gawio la kiasi cha Sh. Bilioni 12.12 kutoka kwa Taasisi 58 jijini Dodoma.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Benny Mwaipaja, akisoma
orodha ya Taasisi za Serikali ambazo zimetoa gawio la Serikali kwa
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (hayupo
pichani), jijini Dodoma
Sehemu ya Wawakilishi wa Taasisi
waliofika kwa ajili ya kutoa gawio la Serikali wakisikiliza hotuba ya
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (hayupo
pichani), wakati wa hafla ya kupokea gawio jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (katikati) akiwa katika
picha ya pamoja na Wenyeviti mbalimbali na Watendaji Wakuu kutoka
Taasisi za Serikali baada ya halfa ya kukabidhi gawio la kiasi cha Sh.
Bilioni 12.12 kutoka kwa Taasisi 58 jijini Dodoma. kutoka kushoto ni
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Adolf Ndunguru, kwa
niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, kulia ni Msajili wa Hazina, Bw.
Athumani Mbutuka
(Picha na Josephine Majura – WFM Dodoma).
………………
Na Peter Haule na Josephine Majura, WFM, Dodoma
Serikali imesema
Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika, Kampuni na Taasisi za Umma ambazo
hazitawasilisha gawio na michango yao kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali
ifikapo Januari 23 mwaka 2020, kabla ya saa 6 usiku, Bodi zitakuwa
zimevunjwa na watendaji wake kupoteza ajira zao.
Hayo yameelezwa
Jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango,
wakati akipokea gawio na michango kutoka Mashirika, Kampuni na Taasisi
za Umma 11, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli alilolitoa Novemba 24 mwaka huu lililozitaka taasisi
hizo kutoa gawio ndani ya siku 60.
Alisema
itakapofika saa sita usiku ya tarehe 23 Januari, 2020 kama hawajaleta
gawio wala michango ya kuingia kwenye mfuko Mkuu, Bodi hizo zimevunjwa,
Watendaji Wakuu wa hizo taasisi husika nao watahusika na akabainisha
kuwa hiyo ndiyo amri ya Serikali.
“Tukio la
Novemba 24, 2019 la kupokea gawio, mashirika yalikuwa 79 na Mhe. Rais,
alipokea hundi ya jumla ya Sh. trillion 1.05 na aliniagiza ndani ya siku
60, Taasisi, maashirika na kampuni 187 ambazo hazikutoa gawio siku hiyo
zitekeleze maagizo yake”, alieleza Dkt. Mpango.
Alisema kuwa
baada ya agizo la Rais, katika kipindi cha siku 18, Taasisi, Kampuni na
Mashirika 58 yametekeleza agizo ambapo jumla ya fedha zilizopokelewa
katika mfuko Mkuu wa Hazina ni Sh. bilioni 12.12.
Dkt. Mpango
aliyapongeza mashirika, kampuni na taasisi hizo kwa kuitikia wito huo
kwa kutoa fedha hizo ambazo amesema zitasaidia katika shughuli za
maendeleo ya nchi kwa njia ya ujenzi wa miradi na kuiwezesha nchi
kujitegemea.
Alisema kuwa
amefurahishwa na gawio na michango lakini amesema wanatakiwa kuongeza
kiwango hicho mwakani kwa kuwa Watanzania wanatakiwa kuona kuwa
waliopewa dhamana ya kusimamia mashirika yao wanatimiza wajibu wao.
Kwa upande wake
Msajili wa Hazina Bw. Athumani Mbutuka, amesema idadi ndogo ya kampuni,
mashirika na taasisi ya umma 71 kati ya 266 yaliyo katika orodha ya
Msajili wa Hazina yaliyochangia gawio na michango mingine wakati Mhe.
Rais Magufuli akipokea magawio hayo kwa niaba ya wananchi,
haikumfurahisha Kiongozi huyo wa Nchi.
Miongoni mwa
Taasisi zilizotoa mchango ni pamoja na Chuo cha kilimo- SUA, Chuo cha
Mipango na Maendeleo Vijijini- IRDB, Taasisi ya Taifa ya Usafirishaji –
NIT, Mfuko wa Misitu Tanzania- TFF, Chuo cha Ufundi Stadi- VETA,
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Taasisi ya Kudhibiti
ubora wa Mbegu Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...