NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar
Dk.Abdulla Juma Mabodi,akifungua Kongamano la Wiki ya Kachorora la
kuadhimisha miaka 20 toka kuanzishwa kwa Maskani ya CCM ya Kachorora
iliyopo Mwembe Shauri Zanzibar.
AFISA Mwandamizi kutoka Afisi Kuu
ya UVCCM Zanzibar Ndugu Shara Ame Ahmed, akitoa mada ya dhana ya
kuanzishwa kwa Maskani, katika kongamano la wiki ya Kachorora
lililofanyika katika ukumbi wa Kituo cha kulelea Wazee Sebleni Zanzibar.
MJUMBE wa Maskani ya Kachorora
Ndugu Suleiman Omar ‘Ganzi’ akitoa nasaha juu ya umuhimu wa Wanachama wa
CCM kuwarithisha Watoto itikadi na fikra za ukombozi kabla na baada ya
Mapinduzi ili wakue wakijua historia halisi ya nchi.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar
Dk.Abdulla Juma Mabodi,akiwa na Wana Maskani ya Kachorora pamoja na
Maskani mbali mbali zilizoalikwa katika hafla hiyo, wakifuatilia kwa
makini mada mbali mbali zinazowasilishwa katika kongamano hilo la Wiki
ya Kachorora, lililofanyika ukumbi wa Sebleni Wilaya ya Amani kichama
Zanzibar.
***********************************
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu
wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi,amesema
siasa za ulaghai na uchochezi wa vurugu zinazofanywa na upinzani
visiwani Zanzibar, hazitozuia ushindi wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2020.
Amesema Chama
cha Mapinduzi kitapata ushindi wa kihistoria kwa majimbo ya Unguja na
Pemba ambao haujawahi kutokea toka kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi
nchini mwaka 1992.
Kauli hiyo
ameitoa wakati akifungua kongamano la wiki ya Kachorora lililofanyika
katika ukumbi wa Kituo cha kulelea Wazee Sebleni Wilaya ya Amani kichama
Zanzibar.
Alisema ushindi
huo utapatikana kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ya mwaka
2015/2020 kwa wananchi wote mijini na vijijini , ambao kila mwananchi
kwa sasa ananufaika na huduma muhimu za kijamii zilizoimarishwa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alieleza kuwa
hakuna chama cha siasa chochote duniani kilichopata kibali na ridhaa ya
kuongoza dola kupitia njia ovu za vurugu,vitisho na uongo badala yake
vyama vinavyoongoza dola ni vile vilivyokuwa karibu na wananchi kutokana
na uhodari wa kutekeleza kwa vitendo matakwa ya wananchi.
Dk.Mabodi,
alifafanua kuwa CCM itaendelea kuweka vipaumbele vya kuisimamia serikali
itekeleze kwa vitendo sera za maendeleo kwa wananchi,huku wapinzani
wakiendelea kujinadi na kupiga porojo zisizokuwa na tija kwa wananchi.
“Chama cha
Mapinduzi hakitishwi na hakiogopi taasisi yoyote ya kisiasa wala kundi
la watu , kwani ni chama imara na chenye historia kubwa barani Afrika na
Duniani kote hivyo hao walioanza kujitokeza kuleta uchochezi tunawaonya
waache kuchafua nchi vinginevyo watajuta kwa uovu wao.
Nawambia kwamba
ushindi wetu ni lazima kama Ibara ya 5 ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977
toleo jipya la 2017 inavyoelekeza, sasa tuwaone na uchaguzi huu watakuja
na uongo upi kwani uchaguzi uliopita waliiba kura na kuvuruga uchaguzi
na uchaguzi wa marudi wakasusia.”,alisema Dk.Mabodi.
Kupitia kongamano
hilo alivitaka vyombo vya Ulinzi na Usalama nchini kutekeleza wajibu
wao kwa kudhibiti uvunjifu wa amani na utulivu, ulioanza kuvunjwa na
baadhi ya wanasiasa wanaotamka kauli za uchochezi bila kuchukuliwa hatua
za kisheria.
Alisema Chama cha
Mapinduzi kwa muda mrefu kimekuwa na uvumilifu wa kisiasa kwa kuheshimu
sheria,miongozo na kanuni za Uchaguzi na nchi lakini hakitokuwa tayari
kuona baadhi ya wanasiasa wanaibuka na kuhamasisha vurugu.
“Itafikia wakati
uvumilivu wetu utakuwa na kikomo kama vyombo vya ulinzi na usalama
mtashindwa kuwadhibiti hao wanaofanya vurugu wakiweka mguu wa kushoto na
sisi tutaweka mguu wa kulia, nchi haitakalika na hatutaki kufikia huko
bali tushindane kwa hoja na sera za kimaendeleo.”, alisisitiza Naibu
Katibu Mkuu huyo.
Aliwambia
wanachama wa CCM walioshiriki katika Kongamano hilo kuwa wanatakiwa
kuwahamasisha wananchama wenzao na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa
wingi kushiriki katika zoezi la uandikishaji wa daftari la wapiga kura
linalotarajiwa kuanza Januari 18 kisiwani Pemba.
Alisema ushiriki
wa Wana CCM katika zoezi hilo la Daftari la wapiga kura ni sehemu muhimu
ya kuandaa mazingira ya ushindi wa CCM kwani ndio chimbuko la
kupatikana wapiga kura watakaofanikisha ushindi wa CCM uchaguzi mkuu
ujao.
Katika maelezo
yake Dk.Mabodi,aliwataka Wabunge, Wawakilishi na Madiwani kufanya
mikutano ya Hadhara katika maeneo yao na kueleza kwa kina namna
walivyotekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020.
Akizungumzia
umuhimu wa maskani Dk.Mabodi, alisema maskani ni sehemu ya kueneza
itikadi na kupanga Mapinduzi ya kiuchumi yenye kuleta maendeleo
endelevu.
Alisema viongozi
namba moja ndani ya Chama cha Mapinduzi ni mabalozi wa mashina na
maskani hivyo ni lazima viongozi washuke katika ngazi hizo kufahamu
mahitaji yao na kupokea ushauri wa kujenga chama.
Aliwapongeza Wana
Maskani ya kachorora kwa ubunifu wao wa kuandaa kongamano la kujadili
masuala muhumu ya kujenga chama sambamba na kuzialika maskani zingine
ili kuendeleza umoja na mshikamano.
“Maskani ya
kachorora ni kati ya maskani kubwa tatu Tanzania zilizofanya mambo
makubwa nchini na zenye historia ya chimbuko la kueneza itikadi na
miongozo imara ndani nan je ya chama chetu”, alisema.
Dk.Mabodi,
aliwapongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dk.Ali Mohamed Shein pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt.John Pombe Magufuli kwa uchapakazi wao mzuri
Naye Katibu wa
Maskani ya Kachorora ndugu Samia Leonard Shirima,alisema lengo la
kufanya kongamano hilo ni kutoa elimu ya juu ya masuala mbali mbali
yanayotekezwa na CCM pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha,alisema
makani hiyo inasherehekea miaka 20 toka kuanzishwa kwake hivyo inafanya
shughuli mbali mbali za kijamii zikiwemo kufanya usafi,kutembelea
viongozi wastaafu na wazee wa Chama cha Mapjnduzi.
Katika kongamano
hilo la siku moja zilizotolewa mada tatu zikiwemo unyanyasaji wa
kijisia, dhana ya kuanzishwa kwa maskani pamoja na Mafanikio ya awamu ya
saba.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...