Katibu Mkuu Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo
ya Jamii Dkt. John Jingu akizungumza na Wakuu wa vyuo vya elimu ya juu
waliokutana kujadili namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia katika
vyuo vya elimu ya juu kilichofanyika jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt.Francis Michael
akitoa mada kwa Wakuu wa vyuo vya elimu ya juu kilichohusu namna ya
kupambana na ukatili wa kijinsia katika vyuo vya elimu ya juu
kilichofanyika jijini Dodoma.

Mkuu wa Uelimishaji kutoka Taasisi
ya Kupambana na Kutokomeza Rushwa TAKUKURU Bw. Asseri Mandari akitoa
mada kuhusu jitihada za Taasisi hiyo katika kupambana na rushwa ya ngono
katika sehemu za kazi na katika Sekta ya elimu hasa elimu ya juu katika
kikao kilichofanyika jijini Dodoma kilichohusu namna ya kupambana na
vitendo vya ukatili wa kijinsia katika vyuo vya elimu ya juu.


Baadhi ya Wakuu
wa vyuo vya elimu ya juu wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa
zikitolewa katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma kilichohusu namna
ya kupambana na ukatili wa kijinsia katika Taasisi na Vyuo vya elimu ya
juu nchini.Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii Dkt. John
Jingu amekemea matukio ya vitendo vya ukatili wa kijinsia katika Vyuo vya elimu
ya juu hasa vitendo vya rushwa ya ngono.
Dkt. Jingu ameyasema hayo jijini
Dodoma wakati akifungua kikao kilichowakutanisha Wakuu wa vyuo vya elimu ya juu
kilichohusu namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia katika maeneo ya Vyuo vya
elimu ya juu.
Dkt. Jingu ameongeza kuwa tatizo la
ukatili wa kijinsia limekuwa likishamiri katika Vyuo vya elimu ya juu kwani
imeripotiwa kuwa wahadhiri wengi wamekuwa wakitumia madaraka yao
kuwalazimisha wanafunzi kufanya nao ngono kwa lengo la kuwafaulisha mitihani.
Amesema kuwa sio wanafunzi pekee
wanaokumbana na vitendo hivyo ila hata wafanyakazi wanaofanya kazi katika Vyuo
vya elimu ya juu wanakubwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia hivyo nguvu ya
ziada inahitajika katika kupambana na vitendo hivyo vyuoni.
"Tumeshuhudia uwepo wa matukio
ya ukatili wa kijinsia katika vyuo vyetu vya elimu ya juu hasa rushwa za ngono
hili sio sawa tunatakiwa kulikemea kwa nguvu zote" alisema Dkt Jingu.
Dkt. Jingu amesema kuwa katika
kuhakikisha tunapambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia Serikali na Wadau
wanatekeleza Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake
na Watoto ili kuhakikisha kuwa vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia nchini
vinatokomezwa kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.
Aidha Dkt. Jingu amewataka wakuu wa
vyuo hao kuhakikisha wanatoa elimu na maelekezo ili kujenga uelewa wa kupambana
na vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kwa wanafunzi wa kike kwa kwa ajili ya
kuepuka matakwa ya wahadhiri wanaotumia hila kuendekeza ukatili wa kingono vyuoni.
Pia Dkt. Jingu amewataka
Wakuu wa vyuo hao kuhakikisha wanatekeleza Agizo la Waziri Ummy Mwalimu la
kuanzisha madawati ya jinsia katika vyuo vyao ili kuwezesha kuondokana na
vitendo vya kikatili na kujenga mazingira yaliyosalama katika vyuo vyetu.
Kwa upande wake
Mkuu wa Uelimishaji kutoka Taasisi ya Kupambana na Kutokomeza Rushwa TAKUKURU
Bw. Asseri Mandari amesema kuwa Taasisi hiyo imejipanga kupamabana na tatizo
hilo kwa kuanzisha Kampeni inayaosema “Vunja
Ukimya Ondoa Rushwa ya Ngono” itakayosaidia kuondokana na vitendo vya
ukatili wa kijinsia hasa kuzuia rushwa ya ngono.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Jinsia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam Dkt. Lulu Mahai amesema kuwa Vyuo vya elimu ya juu vinawajibu mkubwa wa kuhakikisha wanatoa elimu kuhsu kupambana na vitendo vya kikatili kwa wanafunzi wa wafanyakazi na wanaamini baada ya kikao hiki watarudi na kuanzisha madawati ya jinsia na kamati mbalimbali zitakazosaidia kupambana na matukio ya ukatili wa kijinsia katika Taasisi na Vyuo vyote nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...