Afisa Tehama wa Mahakama Kuu Tanga, Bi. Amina Ahmad akielezea utekelezaji na usimikaji wa Mfumo wa Kielektroniki wa Maktaba ya Mahakama Kuu Tanga (E- Library).
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Francis Kabwe akisoma taarifa ya Kanda hiyo.
Mhe. Jaji Kiongozi akizungumza na wananchi waliofika Mahakama Kuu Kanda ya Tanga kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.
Mhe. Jaji Kiongozi (wa katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama Kuu Kanda ya Tanga. Kushoto kwake ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda Tanga Mhe. Amiri Mruma akifuatiwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Francis Kabwe. Kulia kwake ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Edson Mkasimongwa akifuatiwa na Mtendaji wa Mahakama Bw. Ahmed Selemani Ng’eni.


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi ameupongeza uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya ya utekelezaji wa Mahakama Mtandao (E- Judiciary ) licha ya kupata bajeti ndogo.

Aidha, Jaji Kiongozi huyo amempongeza Afisa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Bi. Amina Ahmad kutokana na jitihada zake za kutumia vyema taaluma yake kubuni na kuanzisha mifumo ya kielektroniki ya ndani kwa ajili ya kusaidia utunzaji na uhifadhi salama wa majalada ya mashauri na nyaraka mbalimbali za kiutendaji.

Afisa Tehama huyo alibuni mifumo hiyo kwa kupitia mifumo ya “Tanga Record Centre”, E- Office, E-Library na Receive & Return File Database (Double R).

Vile vile alimpongeza Afisa huyo kwa kuwezesha kusimikwa (Installation) kwa mifumo ya matangazo kwa umma (Public Announcement system) na uoneshaji wa orodha ya mashauri kwenye Televisheni (Case Broadcasting system).

Alipongeza utendaji wa pamoja (Team work) uliojengwa na watumishi wa Kanda ya Tanga chini ya uongozi na usimamizi wa Jaji Mfawidhi, Mhe. Amiri Mruma.

Mhe. Jaji Kiongozi aliyasema hayo baada ya kupokea taarifa ya Kanda iliyosomwa kwake na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Tanga, Mhe. Francis Kabwe, na baadae kujionea shughuli na utendaji wa mifumo ya kielekroniki kupitia ratiba ya ziara yake ya siku moja aliyoifanya tarehe 10 Desemba mwaka huu.

Katika ziara hiyo alionyesha kuridhishwa na utendaji wa kanda hiyo na kusema kuwa, inastahili kuwa ya kimkakati kwa mafunzo ya vitendo kwa viongozi wapya hasa kwa kuzingatia kwamba iko jirani na Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA).

Dkt Feleshi aliutaka uongozi huo kuwatambua, watumishi wanaothubutu kuonesha ubunifu kutokana na vipaji vyao waeleweke na kuenziwa ili waendelee kuwa hazina ya Mhimili wa Mahakama badala ya kukatishwa tamaa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...