Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
WAZIRI
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwele (Mbunge)
amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini Mhandisi
Deusdedit Kakoko kusimamia kwa ukaribu mfumo wa ukusanyaji wa mapato
unaofanywa Mamlaka hiyo kwa kuwa hela inayopatikana ni kubwa tofauti na
inayoashikwa na kupelekwa kwa Serikali.
Akizungumza
leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa bodi ya wakurugenzi wa
Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Waziri Kamwele amesema
kuwa;
"Makusanyo
yaliyo kwenye mfumo ni tofauti na hard copy (yaliyoandikwa), hela
inayopatikana ni kubwa tofauti na inayoshikwa na kupelekwa serikalini,
Mkurugenzi TPA lifanyie kazi suala hilo" ameeleza Waziri Kamwelwe.
Amesema
kuwa bodi hiyo ya wakurugenzi lazima ihakikishe Mamlaka hiyo inafikia
malengo waliyoweka na kuwataka zaidi kusimamia ukusanyaji wa mapato kwa
njia za mfumo wa kieletroniki na hiyo ni sambamba na mapato hayo
kuendana na yanayoandikwa na kuwasilishwa;
"
Tujipongeze kwa kuwa Mamlaka hii imeongoza kwa kutoa gawio kwa serikali
mwaka huu, tumetoa shilingi bilioni 480, tujitahidi katika ukusanyaji
wa mapato na kutoa gawio la shilingi trilioni moja kwa serikali mwaka
ujao, mapato yanavuja simamieni na kuendeleza mifumo ya TEHAMA ili
ufanye kazi vizuri na kuondoa kila namna ya uvujishaji wa mapato hayo"
Amesema.
Aidha
amesema kuwa katika kutekeleza sera ya Serikali ya kujenga uchumi wa
viwanda ifikapo 2025 hawana budi kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo
uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam unaendelea ili ukamilike kama
ilivyopangwa na hiyo ni pamoja na kununua mitambo mikubwa sambamba na
kuimarisha ulinzi na usalama hasa katika bandari za mipakani.
Vilevile ameitaka bodi hiyo kuendelea na kampeni za kimasoko ili kuhimili ushindani na kuongeza wateja wenye mizigo na meli.
"Tulikuta
na wachimbaji wa madini na wamiliki wa meli duniani, meli ni nyingi
sasa katika bandari yetu; bodi iweke mkakati maalumu wa meli kupakua
mizigo kwa muda muafaka bila kupoteza Mapato" amesema.
Waziri
Kamwele pia ameitaka bodi hiyo pia kusimamia ujenzi wa bandari zote
katika Maziwa makuu na bahari ya Hindi pamoja na upanuzi wa bandari na
kukarabati bandari nyingine za mwambao wa bahari hususani Tanga na
Mtwara.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania
(TPA) Mhandisi. Deusdedit Kakoko amesema kuwa Mamlaka hiyo itaendelea
kuhakikisha ujenzi na uboreshaji wa miundombinu katika bandari zote
unasimamiwa ipasavyo na hiyo ni pamoja na kusimamia ulinzi na usalama
hasa katika bandari za mipakani.
Mhandisi
Kakoko ameeleza kuwa utafutaji wa masoko ni jambo la msingi lenye
kuhitaji ushindani na hiyo ni pamoja na kutumia mifumo ya TEHAMA;
sambamba na kuboresha bandari bubu ambazo zipo 437 kote nchini ambapo
bandari zenye faida zitarasimishwa ili wananchi waende sehemu sahihi
zaidi na kudhibiti matumizi mabaya ya bandari hizo.
Vilevile
Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi TPA Profesa. Iggnas Rabaratuka
ameishukuru Serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano kwa ushirikiano wa kujenga taifa na kusema kuwa maagizo
waliyopewa yatakuwa dira katika utekelezaji wao.
Amesema
kuwa suala la utekelezaji wa matumizi ya mfumo wa TEHAMA katika
ukusanyaji wa mapato utachukua mwaka mmoja pekee ili mapato yafanyike
katika mfumo huo hali itakayopelekea kuongezeka kwa kasi ya ukusanyaji
wa mapato.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...