Charles James, Michuzi TV

PAUL Labile Pogba. Ni fundi haswa uwanjani, ni mchezaji ambaye kila Timu na kocha yeyote angetamani ammiliki kama mchezaji wake.

Atakupa ubora mkubwa uwanjani, atakuza biashara ya Jezi zako na kuongeza idadi ya mashabiki.

Ni sahihi kusema Pogba ni miongoni mwa wachezaji wenye mvuto wa kibiashara hivi sasa na ni miongoni mwa mastaa wa soka wenye nyota Kali pia.

Kama hufahamu kinachoendelea hivi sasa kuhusu Labile Pogba wacha nikujuze kwamba mwamba amekataa ofa mpya iliyowekwa mezani na Manchester United.

Mwanzoni ilionekana hafurahishwi na mbinu za kocha Jose Mourinho, alivyotimuliwa na kuletwa Ole Gunnar bado Pogba ameendelea kuonesha msimamo wake wa kutaka kusepa.

Tatizo ni nini? Pesa? Hapana. Uhakika wa namba? Hapana. Pogba uhakika wa kucheza upo tena mkubwa tu. Nini tatizo? Hii ndio hoja ya msingi.

Kabla ya mitikisiko ya Pogba kutaka kuondoka Golikipa wa Manchester United, David de Gea nae alitikisa kiberiti cha kutaka kuondoka kwa muda mrefu.

De Gea hakua anahitaji mshahara mkubwa kama United walivyodhani, na yeye alichoshwa na maisha ya Old Trafford. Alihitaji changamoto mpya.

Na hata sasa licha ya kusaini mkataba mnono bado anataka kuondoka hafurahii tena maisha ya United. Amechoka.

Kwahiyo kinachofanywa na Pogba hivi sasa ni muendelezo wa kile ambacho kilianzishwa na De Gea.

Bahati mbaya mashabiki na Uongozi wa United hawataki kuukubali ukweli kwamba mastaa wa timu Hiyo wamechoka kuendelea kuwepo hapo walipo.

Gwiji la fasihi duniani, Chinua Achebe amewahi kusema, " Ukitaka kujua mvua imekunyeeshea kiasi gani basi ni lazima ukumbuke tone la kwanza lilikudondokea wapi,"

United wanapaswa kukumbuka tone la kwanza liliwadondokea wapi. Maana hakuna kinachowatesa kama kuona wachezaji wakiwa hawana furaha na maisha ya Klabu yao.

Duniani kama utataja Klabu za ndoto za wachezaji wengi basi ni Real Madrid, Manchester United na Barcelona.

Leo inakuaje hawa akina Pogba wairingie Klabu yenye mataji mengi Uingereza? De Gea anaanzaje kuwadengulia mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu ya England?

Timu yenye thamani kubwa England inaanzaje kuangaika kubembeleza wachezaji wawili watatu kusaini? Ni lazima tukubaliane kwamba lipo tatizo sehemu.

Turudi katika msemo wa Chinua: Tone la kwanza la mvua lilianza kuwadondokea United mchana ule wa Mei 8, 2013.

Hapa ndipo matatizo yote yalipoanzia, ubabe wao ulitia nanga hapa, hizi jeuri zote zimesababishwa na kuondoka kwa Kocha Alex Ferguson.

Baada ya Ferguson kustaafu United walishindwa kuishi bila mzee huyu, wangeishije bila kocha aliyewapa mataji zaidi ya 30 katika kipindi cha miaka 27? Hakika ni ngumu.

Na kosa lao ni kukataa kujenga upya timu, ukiangalia aina ya wachezaji ambao Fergie alikua nao sio 'quality' ya wachezaji wanaotakiwa hivi sasa kwenye soka la ushindani.

Ferguson alikua na kikosi chake cha kawaida sana. Valencia, Ashley Young, Phil Jones, Smalling hii ndo ilikua aina ya wachezaji wake ambao leo kesho mashabiki wa United wanawaona mitumba ila walibeba ubingwa na Babu.

Kubadilisha makocha mara kwa mara kumewaathiri pia, toka aondoke Fergie wameajiri makocha wanne tofauti.

Mbaya zaidi wanawapa tageti ya ubingwa kila kocha anaekuja wakidhani ni rahisi. Soka limebadilika wanapaswa kuwekeza upya kwenye mfumo wa uendeshaji ili kurudisha mafanikio yaliyopotea.

Wakiendelea kuamini wao ni Timu kubwa watabaki kumaliza msimu bila taji na wachezaji mastaa wataondoka maana hakuna mchezaji asietaka kutwaa ubingwa.

Pogba anasisitiza kuondoka kwa sababu anaanza mwaka wa tano sasa na haoni dalili za kubeba ubingwa wa Ligi Kuu wala taji la Ulaya.

Mipango chini ya kocha Ole Gunnar haimuoneshi mafanikio mbele. Anaitizama United kama Timu ya kawaida mbele ya Liverpool na Manchester City msimu ujao.

Kwanini aendelee kubaki sehemu isiyo na mvuto na mataji? Kwanini asiende Madrid au kurudi Juventus akabebe mataji.

TUFIKIE MWISHO

Manchester United ni Klabu kubwa, wanahitaji kuyarudisha mafanikio yao ili kuvutia nyota wengi kujiunga nao.

Kipindi cha Ferguson walifanikiwa kwa sababu ya ushawishi aliokua nao kocha mwenyewe na 'status' ya Klabu ilijieleza.

Leo hii ni mwaka wa sita hawajabeba Kombe la Ligi Kuu, wanapita taratibu katika njia ambayo Liverpool wameteseka nayo kwa miaka 29 sasa bila EPL.

Njia pekee ya kurudisha mafanikio katika Dunia ya sasa siyo kuwekeza pesa nyingi. Inawabidi wajitoe mhanga na kukubali kuanza upya.

Wakidhani wana pesa na ukubwa wa Timu yao wakaendelea kusajili wachezaji wenye majina makubwa wakitegemea watapata mataji basi ndivyo watakavyozidi kulichimba kaburi lao wenyewe.

Wakubali kuanza moja. Watafute Kocha ambaye anaweza kujenga Timu kutokea chini, wamvumilie bila kumpa presha ndani ya miaka mitatu minne watarudisha ubabe wao.

Wanaweza kutetereka kibiashara lakini Hiyo ndio njia pekee ya kurudisha umwamba wao kwenye Ligi Kuu na UEFA, tofauti na hapo akina Pogba wataendelea kuwaringia sana tu.

Liverpool walianza hivyo hivyo ikawachukua miaka 29 kuanza kurudisha makali yao. Arsenal huu ni mwaka wa 16 hawajui ladha ya EPL.

Ukienda Italia, AC Milan toka wanyeeshewe na mvua wameshindwa kukumbuka tone la kwanza liliwadondokea wapi.

Kuendelea kuamini mafanikio yao yataletwa na Ole Gunnar ni kujitekenya na kujicheka wenyewe. Kuzidi kuwa na Ed Wood kama Mkurugenzi wa Michezo ni tatizo lingine lenye uhusiano na kirusi. Period!

0683 015145

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...