Waziri Ummy, akieleza jambo
wakati akiwa katika ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya
katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora
Dkt. Honoratha Rutatinisibwa akitoa taarifa ya hali ya Afya katika Mkoa
wa Tabora wakati wa ziara ya Waziri Ummy katika Mkoa huo.

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.@umwalimu akikagua uboreshaji miundombinu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, pindi alipofanya ziara katika Mkoa huo.

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.@umwalimu akiongea na baadhi ya wanawake waliofika kupata huduma za Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora,


Wananchi wa Tabora wakisikiliza
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy
Mwalimu akiwasilisha Salam kutoka kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt.@MagufuliJP kwa wananchi hao.
…………………………………………
Na Rayson Mwaisemba WAMJW- TABORA
Serikali kupitia Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imedhamiria kuboresha huduma
za Rufaa katika Hospitali za Rufaa za mikoa kwa kuhakikisha inaboresha
kwa kujenga miundombinu ya majengo ya dharura na ajali.
Hayo yamesemwa, na Waziri wa
Afya, Mh. Ummy Mwalimu wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji
huduma za Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora.
” Sisi kama Serikali,
tumedhamiria kuboresha huduma za Rufaa katika Hospitali za Rufaa za
Mikoa, kwa kuhakikisha tunaweka miundombinu, hususan jengo la dharura na
ajali “. alisema Waziri Ummy Mwalimu.
Hata hivyo, Waziri Ummy alisema
Serikali imedhamiria kuboresha huduma za Afya kwa wananchi, kwa kutenga
takribani Bilioni 8.8 kwa ajili ya ujenzi wa zaidi ya Vituo vya Afya 13,
huku akieleza kuwa Hospitali za Wilaya za Sikonge na Uyui nazo
zinaendelea kujengwa hali itakayosaidia kupunguza mzigo kwa Hospitali ya
Mkoa.
“Sisi kama Serikali tumedhamiria
kuboresha huduma za Afya, kuanzia miundombinu, Serikali tunajenga vituo
vya Afya zaidi ya 13, ambayo takribani Bilioni 8.8 zimeshaingizwa na
vingine nimeanza kutoa huduma lakini tunajenga Hospitali mbili za Wilaya
ambazo ni Sikonge pamoja na Uyui” alisema
Licha ya kupunguza kiwango cha
maambukizi ya ugonjwa wa Malaria nchini, Waziri Ummy ameagiza kupitia
Maafisa Afya kutoa elimu kwa wananchi ili kutokomeza mazalia ya mbu
waenezao Malaria, huku akisisitiza kuwa ni lazima Halmashauri kununua
viuadudu vya kuangamiza viluilui katika mazalia ya mbu.
Mbali na hayo, Waziri Ummy
aliipongeza timu ya Afya ya Mkoa kwa jitihada inazozichukua katika
kuimarisha usafi wa mazingira hususan katika ujenzi na matumizi ya vyoo
bora jambo litalosaidia kupunguza magonjwa ya kuhara, magonjwa ya tumbo
na Kipindupindu.
“Ujenzi na matumizi ya vyoo Bora
ndani ya mwaka mmoja mmetoka Asilimia 53.7 mpaka asilimia 59, lakini pia
tumepunguza kaya ambazo hazina vyoo kabisa kutoka asilimia 7 mpaka
asilimia 2” alisema.
Kwa upande mwingine, ameagiza
asilimia 2 ya watu wasiokuwa na vyoo kutafutwa ili kuhakikisha wanajenga
vyoo na kuvitumia kwa usahihi, huku akisisitiza wasiofanya hivyo ndani
ya muda wa makubaliano wachukuliwe hatua za kisheria, alisisitiza.
Pia, Waziri Ummy alisema kuwa
katika Mkoa wa Tabora vifo vya akina mama wajawazito vimepungua kutoka
wajawazito 99 mpaka wajawazito 60 kwa mwaka huku akisisitiza Watoa
huduma kuendelea kujituma ili kuhakikisha usalama wa mama na mtoto.
Aliendelea kusema, Wanawake ambao
wanajifungulia katika vituo vya kutolea huduma za Afya katika Mkoa wa
Tabora ni zaidi ya Asilimia 100%, huku kitaifa ikiwa ni asilimia 63,
hivyo ametoa Wito kwa wanawake kuendelea kujifungulia katika vituo vya
kutolea huduma za Afya.
“Tumeona kwamba Wanawake ambao
wanajifungulia katika vituo vya kutolea huduma za Afya katika Mkoa wa
Tabora ni zaidi ya 100%, wakati kitaifa tunazungumizia asilimia 63
kwahiyo hongereni sana kwa kupunguza vifo, kutoka wajawazito 99 mpaka
60” alisema.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...