Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imetumia zaidi ya  shilingi bilioni 1.2 kwa mwaka 2019 kwa ajili ya kulipa gharama za matibabu ya moyo kwa wagonjwa wanaotoka katika familia maskini na  wasiokuwa na uwezo wa kulipia gharama hizo.

Hayo yamesemwa leo na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Agnes Kuhenga wakati akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya  kupokea msaada wa vifaa tiba pamoja na dawa kutoka Ubalozi wa China kupitia Timu ya madaktari kutoka nchini humo wanaofanya   kazi hapa nchini.

 Agnes ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Utawala na Fedha alisema asilimia 10 hadi 15 ya wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo hawana kadi za bima ya afya na hawana uwezo wa kulipia gharama za matibabu. Wagonjwa wa aina hiyo wanapata huduma za matibabu kwa Taasisi   kugharamia matibabu yao.

“Januari mwaka huu hadi siku hii ya leo tarehe 19/12/2019  tumetumia zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa ambao hawakuwa na uwezo wa kuchangia gharama za matibabu. Ninaiomba mifuko ya bima za afya iweze kutoa elimu kwa watanzania  ili wajiunge na bima hizo ambazo zitawapunguzia wananchi gharama ya kulipia fedha za matibabu pindi watakapougua”, alisema Agnes.

Akizungumzia kuhusu  msaada huo Agnes aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa misaada mbalimbali ya huduma za afya wanayoitoa katika Taasisi hiyo na kwa upande wa vifaa tiba pamoja na dawa walizozitoa alisema zitatumika kwa wagonjwa  wasiokuwa na uwezo wa kuchangia gharama za matibabu.

Kwa upande wake mwakilishi wa Balozi wa Jamhuri ya watu wa China hapa nchini Yuan Lin alisema msaada wa vifaa tiba pamoja na dawa walizozitoa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kupitia madaktari wa Kichina wanaofanya kazi hapa nchini unathamani ya shilingi milioni 15.

“Ninaamini msaada huu ambao ni moja ya kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na China katika sekta ya afya utasaidia katika matumizi ya kila siku ya Hospitali na utachangia katika kutoa huduma ya matibabu kwa wagonjwa”, alisema Lin.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tiba Shirikishi Dkt. Delilah Kimambo alisema uhusiano wa Taasisi hiyo na Serikali ya watu wa Jamhuri ya China ulianza miaka mingi iliyopita ambapo hata  Jengo la Taasisi hiyo lilijengwa kwa msaada wa Serikali hiyo.

Alisema Taasisi hiyo pia imekuwa ikipokea madaktari kutoka nchini China ambao wanatoa  huduma za matibabu ya moyo pamoja na kufanya kambi maalum za matibabu ya moyo pia madaktari na wauguzi kutoka JKCI wanakwenda nchini humo  kwa ajili ya kupata utaalamu zaidi wa magonjwa ya moyo.

Dkt. Delillah alisema, “Tunajivunia kuwepo kwa madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo watatu katika Taasisi yetu ambao wametoka nchini China. Madaktari hawa wamekuwa msaada mkubwa kwetu na kwa wagonjwa tunaowatibu katika kutoa huduma za matibabu ya moyo ikiwemo upasuaji kwa watoto na watu wazima”,.

Selikali ya Jamhuri ya watu wa China  kila baada ya miaka miwili huwatuma madaktari kwa ajili ya kufanya kazi ya kutoa huduma ya matibabu hapa nchini ambapo kwa mwaka   2018  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete iliwapokea madaktari bingwa wa moyo watatu kwaajili ya kufanya kazi ya Matibabu ya Moyo katika Taasisi hiyo. 
 Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Agnes Kuhenga pamoja na kiongozi wa timu ya madaktari kutoka Jamhuri ya watu wa China wanaofanya kazi hapa nchini Dkt. Quin Chengwei wakiweka saini makubaliano ya  makabidhiano ya dawa na vifaa tiba vyenye  thamani ya shilingi milioni 15 zilizotolewa na Ubalozi wa China kupitia madaktari hao kwa ajili ya wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kuchangia gharama za matibabu wanaotibiwa katika Taasisi hiyo. Hafla fupi ya makabidhiano hayo ilifanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa  Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
 Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Agnes Kuhenga pamoja na kiongozi wa timu ya madaktari kutoka Jamhuri ya watu wa China wanaofanya kazi hapa nchini Dkt. Quin Chengwei wakibadilishana  makubaliano ya  makabidhiano ya dawa na vifaa tiba vyenye  thamani ya shilingi milioni 15 zilizotolewa na Ubalozi wa China kupitia madaktari hao kwa ajili ya wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kuchangia gharama za matibabu wanaotibiwa katika Taasisi hiyo. Hafla fupi ya makabidhiano hayo  ilifanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa  Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Agnes Kuhenga akipokea baadhi ya dawa na vifaa tiba kutoka kwa mwakilishi wa balozi wa Jamhuri ya watu wa China  Yuan Lin  vyenye  thamani ya shilingi milioni 15 vilivyotolewa  na Ubalozi huo kupitia  timu ya madaktari wa kichina wanaofanya kazi hapa nchini. Hafla fupi ya makabidhiano hayo ilifanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa  Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam. Picha na JKCI

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...