Na Charles James, Michuzi TV
KATIBU Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof Adolf Mkenda amesema kuna haja ya kuweka usawa kati ya wanawake na wanaume ili kupiga hatua zaidi na kupata maendeleo.
Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dodoma wakati alipokua akizindua ripoti ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) inayohusu ripoti ya maendeleo ya watu kwa mwaka 2019 ikionesha wanawake kutopiga hatua katika pato la mtu mmoja mmoja pamoja na kuwa nyuma kielimu ukilinganisha na wanaume.
Prof Mkenda amesema kuna haja ya kuweka usawa na lengo la kutoa ripoti hiyo ni kuweka wazi watu waone nafasi iliyopo kati ya wanawake na wanaume na ametolea mfano bungeni ambapo viti vya wanawake ni asilimia 37 hivyo nguvu ya ziada inahitajika ili kufikia hamsini kwa hamsini.
" Ripoti imeonyesha kwa upande wa wanafunzi wanaomaliza elimu ya Sekondari imeongezeka kwa kiasi kikubwa kwa wanaume kuliko wanawake ambapo inaonyesha wanawake imeongezeka kwa asilimia 11.9 na wanaume asilimia 16.9, ni wazi jitihada ya ziada inapaswa kuchukuliwa ili kufikia hamsini kwa hamsini," Amesema Prof Mkenda.
Awali mratibu wa ripoti za Maendeleo ya binadamu kutoka UNDP, Amon Manyama akitoa taarifa ya ripoti hiyo amesema ripoti ya mwaka 2018 inaonyesha pato la mwanamke kwa siku ni 2,436 huku mwanaume ikiwa ni 3,175 wakati kwa upande wa elimu ya msingi inaonyesha wanaume wameongezeka kuandikishwa kwa asilimia 8.0 huku wanawake ni asilimia 5.6.
Nae Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe Anthony Mtaka amesema ripoti hiyo inaoyesha wanafunzi wanaomaliza elimu ya vyuo vikuu imepanda na changamoto ni uhaba wa ajira .
“ Niwatolee mfano wenzetu wa China walifanya mapinduzi kwa kugeuza vyuo vikuu vyao takribani 600 kuwa vyuo vya ufundi hivyo hata sisi kuna haja kubwa sana ya kubadilisha mfumo tuondokane na digrii na kuwa na vyuo vya ufundi ili kuendana na kasi ya Mhe Rais Magufuli ya kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025," Amesema RC Mtaka.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof Adolf Mkenda akizindua ripoti ya Maendeleo ya watu iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia maendeleo duniani (UNDP) leo jijini Dodoma.
Washiriki mbalimbali wakifuatilia majadiliano mbalimbali kwenye uzinduzi wa ripoti ya maendeleo ya watu iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo iliyozinduliwa leo jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof Adolf Mkenda.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof Adolf Mkenda akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti ya maendeleo ya watu leo jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof Adolf Mkenda (katikati) akionesha ripoti iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa duniani linaloshughulikia maendeleo (UNDP) iliyozinduliwa leo jijini Dodoma. Kulia ni Mstahiki Mega wa Dodoma, Prof Devis Mwamfupe na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...