Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
VIJANA wametakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya umma ikiwa ni pamoja na kupiga Vita vitendo vya rushwa na kuwa wawajibikaji wa mfano ili kulipeleka mbele taifa katika nyanja za kimaendeleo ya jamii na taifa.
Akizungumza katika hafla ya mahafali ya tano ya chuo cha Takwimu ambapo wahitimu 116 wametunukiwa shahada mbalimbali, Waziri wa Fedha wa Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Balozi Ramia Abduwawa amewataka wahitimu hao kufanya kazi kwa kuzingatia maadili bila rushwa, na kueleza kuwa maendeleo yanaletwa na vijana hivyo hawana budi kujitoa na kujenga nchi kwa kuzingatia maadili ya umma.
Vilevile Balozi Ramia amewataka watoto wa kike kusoma kwa bidii na kusoma kozi hizo ambazo zimekuwa na wanawake kwa uchache wa wanafunzi wa kike.
" Wahitimu wanaume ni asilimia 60 na wanawake asilimia 40, wahitimu wanawake mkawashawishi wengine na wanaume mkawashawishi wanaume kuwaacha wanawake wasome wasiwapotezee muda" Ameeleza Balozi Ramia.
Aidha amempongeza Waziri wa fedha Dkt. Philipo Mpango, bodi ya ushauri wa kikanda za uchumi ikiwemo SADC na jumuiya ya umoja wa Afrika Mashariki kwa kuendelea kuwa sehemu ya kufanikisha maendeleo ya Chuo hicho.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki Dkt. Frank Augustine Mkumbo amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Chuo hicho Kanda ya Afrika 1965 kimekuwa kikishirikiana na Serikali kutoka nchi 19 pamoja na jumuiya mbalimbali ikiwemo SADC na wamekuwa wakitoa wahitimu wenye uwezo mzuri wa kushindana katika soko la ajira na kujenga uchumi wa nchi.
Amesema kuwa baada Serikali kukipandisha hadhi Chuo hicho wahitimu wamekuwa mabalozi bora katika kutumia takwimu sahihi, wakati sahihi na zenye tija kwa jamii, na ameishukuru Serikali kwa kuajiri walimu wa kutosha ambao wamekuwa wakitoa maarifa yenye tija kwa jamii na hiyo ni pamoja bodi za mikopo kutoka Serikali ya Tanzania bara na Visiwani na kuwaomba kuendelea kuwadhamini wanafunzi hao wasomao takwimu rasmi katika Chuo hicho.
Amesema kuwa wameanza mchakato wakuandaa programu tano kwa mwaka wa masomo 2020/2021 zitakazoendana na takwimu ili kukidhi soko la ajira.
Pia Mwenyekiti wa bodi ya ushauri wa kikanda ambaye pia ni mtakwimu
Mkuu wa Serikali Dkt Albina Chuwa amesema wamekuwa na kikao kazi kilichofanyika nchini Tunisia katika kuimarisha na kuendeleza Chuo hicho.
"Miaka mitano iliyopita imeleta manufaa makubwa kupitia shahada na Astashahada katika sekta nzima ya takwimu nchini na bara la Afrika kwa ujumla" Ameeleza.
Amesema kuwa sekta hiyo ni muhimu hasa katika masuala ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kupunguza umaskini na hiyo ni kwa kushirikiana Serikali katika kuyafikia malengo ya kupunguza umaskini ifikapo 2030 na kufanya biashara huru katika nchi washirika.
Pia amesema kuwa vijana wana nafasi kubwa katika kuyafikia malengo ya Afrika ya 2063 na hii itafanikiwa kwa kuimarisha uongozi ili kuyafikia malengo hayo pamoja na kuimarisha biashara kwa na kutumia takwimu na taarifa za sasa ili kujiimarisha leo na kuendelea mbele.
Vilevile amewapongeza wahitimu na kuwataka kuzingatia kazi kwa kutoa takwimu sahihi kwa wakati sahihi na zenye mazao bora na kufanya kazi kwa uadilifu.
Baadhi ya wahitimu wakivaa kofia ikiwa ishara ya kutunukiwa shahada zao.
Mtakwimu mkuu wa Serikali na Mwenyekiti wa bodi ya ushauri kikanda Dkt. Albina Chuwa akizungumza katika hafla hiyo ambapo amewashauri wahitimu kuwa mabalozi bora wa chuo hicho kiutendaji na maadili, leo jijini Dar es Salaam.(Picha na Emmanuel Massaka wa Michuzi Tv)
Mkuu wa Chuo cha Takwimu Kanda ya Afrika Dkt. Frank Mkumbo akizungumza katika hafla hiyo ambapo ameeleza kuwa wana mpango wa kuongeza kozi tano zaidi ili kukidhi na kushindana zaidi katika soko la ajira leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Balozi Ramia Abduwawa akizungumza wakati wa mahafali ya tano ya chuo cha Takwimu Kanda ya Afrika, ambapo amesema kuwa vijana ndio Taifa la kesho linalotegemewa, hivyo lazima wafanye kazi kwa kuzingatia maadili, leo jijini Dar es Salaam.(Picha na Emmanuel Massaka wa Michuzi Tv)
Viongozi na baadhi ya wahitimu wakiwa katika picha ya pamoja.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...