Katibu Tawala Mkoa wa Songwe David
Kafulila akizungumza na Waratibu Elimu kata na Wasimamizi wa Sekta ya
Elimu Mkoa wa Songwe ambapo amesema atawachukulia hatua kali za
kinidhamu waratibu wazembe.

Waratibu Elimu kata na Wasimamizi wa Sekta ya Elimu Mkoa wa Songwe wakimsikiliza Katibu Tawala Mkoa wa Songwe David Kafulila (Hayupo pichani) wakati wa kikao cha kutathmini Maendeleo ya Sekta ya Elimu kwa mwaka 2019 na kupanga mikakati ya kuboresha elimu kwa mwaka 2020.
************************************
Waratibu Elimu
kata na Wasimamizi wa Sekta ya Elimu Mkoa wa Songwe waliobainishwa
katika ripoti ya uchunguzi wa hali ya sekta ya Elimu kuwa ni wazembe
katika kusimamia maendeleo ya elimu watachukuliwa hatua kali za
kinidhamu.
Katibu Tawala
Mkoa wa Songwe David Kafulila amesema hayo jana wakati wa kikao na
Waratibu Elimu Kata na Maafisa Elimu ili kutathmini maendeleo ya Sekta
ya Elimu kwa mwaka 2019 na kupanga mikakati ya kuboresha elimu kwa mwaka
2020.
“Tuliwapa kazi
wadhibiti ubora ya kufanya uchunguzi kwanini Mkoa wetu haufanyi vizuri
kielimu na ripoti yao imebainisha uwepo wa uzembe wa waratibu elimu Kata
katika usimamizi, sasa nitachukua hatua kali kwa waratibu elimu wote
wazembe.”, amesema Kafulila.
Kafulila amesema
Waratibu Elimu kata wote walisaini Mkataba ambao uliwataka kusimamia
Sekta ya elimu na kuhakikisha kiwango cha elimu kinapanda lakini pia
serikali imewawezesha posho na usafiri lakini wapo baadhi yao ambao
wameshindwa kutekeleza majukumu yao.
“Serikali imewapa
posho na Waratibu Elimu Kata lakini baadhi yao wamebainishwa katika
ripoti kuwa wanafanya kazi kwa kuogopana na kuendekeza urafiki,
hawawachukulii hatua walimu na wakuu wa shule ambao hawatimizi majukumu
yao, hao hatuwezi kuwavumilia.”, amesisitiza Kafulila.
Naye Mwenyekiti
wa Wadhibiti Ubora wa Elimu Mkoa wa Songwe Mwalimu Jackson Lwafu amesema
walitathmini kwanini baadhi ya shule katika Mkoa wa Songwe zimeshuka
kielimu na walibaini kuwa usimamizi dhaifu umechangia kwa kiasi kikubwa.
Lwafu amesema
endapo wasimamizi wa Elimu Mkoa wa Songwe watatambua majukumu yao na
kuyasimamia, maendeleo ya sekta ya Elimu Mkoa wa Songwe yatakuwa mazuri.
Mratibu Elimu
Kata ya Mkukwe Wilayani Songwe Mwalimu Judith Mwasoke amesema taarifa ya
wathibiti ubora inasikitisha kwakuwa ili kuwe na mafanikio lazima
taratibu zifuatwe hivyo suala la kuoneana aibu na kuogopana halifai na
waratibu Elimu Kata wenye tabia hiyo waache.
Afisa Elimu wa
Halmashauri ya Mji wa Tunduma Mtafya Wilson amesema kwa mwaka 2020
watahakikisha walimu wanafundisha vipindi vyote pamoja na kuwasimamia
Waratibu Elimu Kata wanatimiza wajibu wao.
Afisa Elimu Mkoa
wa Songwe Juma Japhet Kaponda amesema Matokeo ya darasa la saba mwaka
2019 hali haikuwa nzuri kwakuwa Mkoa ulipanda ufaulu kwa asilimia 1.65
kwa kuwa na ufaulu wa asilimia 75 na Mkoa ukishika nafasi ya 21
ukilinganisha na ufaulu wa mwaka 2018 wa asilimia 73 na nafasi ya Mkoa
wa Songwe ilikuwa 17.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...