Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba
na Sheria Prof. Sifuni Mchome akiwahutubia Wajumbe wa Baraza la
Wafanyakazi la TUMESHERIA wakati wa Uzinduzi wa Baraza hilo.

Katibu wa TUGHE wa Mkoa wa Manyara
Bw. Yakubu salim akifafanua jambo wakati wa Mkutano wa Baraza la
Wafanyakazi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania.

Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa
Bi. Jane mbura akifafanua jambo wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Baraza la
Wafanyakazi wa TUMESHERIA iliyofanyika Ngorongoro.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na
Sheria Prof. Sifuni Mchome (katikati) akufuatilia mada katika Hafla ya
Uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi la TUMESHERIA.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na
Sheria (katikati) katika Picha ya Pamoja na Wajumbe wa Baraza la
Wafanyakazi na Menejimenti ya TUMESHERIA baada ya Uzinduzi
Na Karimu Meshack, Ngorongoro
Uongozi wa Tume ya Kurekebisha
Sheria Tanzania yatakiwa kuwaendeleza watumishi wake kitaaluma ili
kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao na kuweka mpango
maalum wa kutambua mchango wa watumishi wao katika maendeleo ya Tume na
Taifa kwa ujumla.
Maelekezo hayo yametolewa na
Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Profesa Sifuni Mchome wakati akizindua
Baraza jipya la Wafanyakazi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania
katika Mkutano wa 14 wa Baraza hilo uliofanyika jana katika ukumbi wa
Mikutano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
“Watumishi ni rasilimali muhimu
kuliko zote kwani ndiyo inayowezesha rasilimali nyingine ziwe na
thamani, kwa maana hiyo kuna umuhimu mkubwa sana kwa Menejimenti ya Tume
kuwawezesha na kuwaendeleza watumishi wake kitaaluma kulingana na kada
zao” alisema Prof. Mchome.
Aidha, Prof. Mchome aliliasa
Baraza la Wafanyakazi la TUMESHERIA kuweka mzingira mazuri yanayomruhusu
mwajiri kuwajengea uwezo watumishi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
kunakuwa na Mpango wa Mafunzo ambao utafuatwa na kutekelezwa vizuri na
kwamba, watumishi watakaotekeleza majukumu yao vizuri, kuwepo na mpango
maalumu wa kutambua mchango wao kwa kipindi kinachokubalika ndani ya
Taasisi. Kwa kujali maslahi ya watumishi, ni dhahiri shahiri kwamba Tume
ya Kurekebisha Sheria Tanzania itapata matokeo chanya kutokana na
kuboreka kwa utendaji na ufanisi wa watumishi wake.
“Baraza la Wafanyakazi ni ushahidi
wa uwepo wa demokrasia mahala pa kazi kwakuwa ni chombo
kinachowashirikisha wafanyakazi kupanga, kusimamia na kutekeleza mipango
mbalimabili ikiwemo mafunzo ya watumishi hivyo ni lazima muweke
mzingira mazuri yanayomruhusu mwajiri kuwajengea uwezo watumishi wake
ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kunakuwa na Mpango wa Mafunzo ambao
utafuatwa na kutekelezwa vizuri. Watumishi watakaotekeleza majukumu yao
vizuri, hakikisheni kunakuwepo na mpango maalumu wa kutambua mchango wao
kwa kipindi kinachokubalika ndani ya Taasisi” alisisitiza Prof. Mchome.
Aidha, Prof. Mchome amewaasa
Baraza la Wafanyakazi la TUMESHERIA kuwa mshiriki na mdau mkubwa katika
kubuni mbinu mpya za uendeshaji na kukabiliana na changamoto mbalimbali
ili kuisaidia Taasisi na Serikali kwa ujumla kuboresha maslahi
wafanyakazi na uhusiano wa kiutendaji baina ya Watumishi na Menejimenti
badala ya kuwa chombo cha kupokea malalamiko ya wafanyakazi pekee.
“Mabaraza yanapaswa kusaidia kutoa suluhisho na fursa kwa wafanyakazi
kushiriki katika maamuzi mbalimbali na kuboresha uhusiano baina ya
Wafanyakazi na viongozi (menejimenti) pamoja na mazingira ya utendaji
kazi mahala pa kazi” alimalizia Katibu Mkuu huyo.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa
Tume ya Kurekebisha Sheria Bw. Casmir Kyuki alisema kwamba TUMESHERIA
imefanya tathmini ya mahitaji ya mafunzo na kuandaa Mpango wa Mafunzo
pamoja na Urithishwaji wa Madaraka (Succession Plan) kwa lengo la
kuwaongezea uwezo watumishi wake na kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika
kuipeleka Tanzania katika maendeleo ya uchumi wa kati na wa viwanda.
Bwana Kyuki alifafanua kwamba
katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2019, watumishi saba wa kada
tofautitofauti walihudhuria mafunzo yaliyohusu kufanya manunuzi kwa njia
ya mtandao (TANEPS) na Uandaaji wa wa Mipango na Bajeti pamoja na
mafunzo ya Uandaaji wa Mfumo Mpya wa Neno Kuu (Key Word Filling
Classification System) wa utunzaji wa kumbukumbu lengo likiwa ni
kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ndani ya Tume na
serikali kwa ujumla.
“katika kipindi cha Julai hadi
Desemba, 2019, watumishi saba katika kada tofautitofauti walihudhuria
mafunzo ikiwa ni matokeo ya kufanya tathmini ya mahitaji ya mafunzo na
kuandaa Mpango wa Mafunzo pamoja na Urithishwaji wa Madaraka (Succession
Plan) kwa lengo la kuwaongezea uwezo watumishi wetu na kumuunga mkono
Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika kuiletea Tanzania
maendeleo ya uchumi wa kati na wa viwanda”. Alisema Bw. Kyuki.
Mkutano wa 14 wa Baraza la
Wafanyakazi la TUMESHERIA unaofanyika kwa siku mbili katika Ukumbi wa
Mikutano wa Makao Mkuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na
mambo mengine, mada kuu nne zimewasilishwa na kuwapa fursa wajumbe
kuzijadili na kujiongezea uwezo na ufanisi katika utekelezaji wa
majukumu yao kwa mujibu wa sheria na kwa kuzingatia agizo la Rais Na. 1
la mwaka 1970. Mada hizo ni: Umuhimu wa Maadili katika Utumishi wa Umma;
Mabadiliko yaliyotokana na Kuunganishwa kwa Mifuko ya Pensheni;
nyingine ni: Utekelezaji wa Bajeti ya Tume kwa mwaka 2019/20 na Mwelekeo
wa Bajeti ya Tume kwa mwaka wa Fedha 2020/2012 na Mwongozo wa Kuandaa
Ikama na Bajeti ya Mishahara kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 na Mabadiliko
Mbalimbali ya Miundo ya Kiutumishi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...