Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umetakiwa kuongeza
jitihada katika kuwaelimisha wananchi kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Afya
na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kuimarisha mifumo ya
utoaji huduma kwa njia ya mtandao.
Agizo hilo limetolewa na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana,
Ajira na wenye Ulemavu, Andrew Massawe, alipotembelea ofisi za OSHA
zilizopo Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo alifanya kikao na menejimenti
ili kupata mrejesho wa utekelezaji wa maelekezo na miongozo mbali mbali
ambayo ofisi yake imekuwa ikiyatoa katika kuboresha huduma kwa wananchi.
“Katika kipindi hiki ambacho serikali inaweka msukumo mkubwa katika ujenzi
wa uchumi wa viwanda, tunataka mageuzi haya ya viwanda yaende
sambamba na uzingatiaji wa viwango vya Usalama na Afya mahali pa kazi ili
kuepuka madhara yanayoweza kutokeaa endapo suala hili muhimu
halitazingatiwa,” alisema Massawe na kuongeza:
“Mmezungumzia pia kuhusu kupanua wigo wa kazi zenu hizi katika maeneo
mengi ya nchi; hilo nalo ni jambo la msingi japokuwa tunataka kuweka
msisitizo katika utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao (automation) lakini
tunahitaji kuwa na ofisi walau katika maeneo yote muhimu. Hivyo tunatakiwa
kujenga mahusiano mazuri na taasisi nyingine katika Wizara ili tuweze
kutumia majengo yaliyopo kwa pamoja kwasababu hatuhitaji kujenga au
kukodisha majengo kila mahali.”
Maagizo hayo ya Katibu Mkuu yalitolewa baada ya kupokea taarifa fupi ya
utekelezaji ya maagizo ya Wizara kutoka kwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA,
Khadija Mwenda, ambapo pamoja na kuelezea utekelezaji mzuri wa maagizo
na miongozo mbali mbali ya serikali, alielezea mpango wa kufungua ofisi za
Kanda ya Magharibi mkoani Tabora itakayohudumia mikoa ya Tabora,
Kigoma, Rukwa na Katavi.
Aidha, katika taarifa hiyo, Mwenda ilielezea jinsi ambavyo taasisi yake
imefanikiwa katika matumizi ya mifumo mbali mbali ya serikali ikiwemo
mifumo ya malipo serikalini ya GePG, MUSE pamoja na mfumo Ununuzi na
Ugavi serikalini wa TANePS.
Katibu Mkuu alisema: “Nimeridhishwa na utekelezaji wa mambo mbali mbali
tuliyowaagiza hususan matumizi ya mifumo mbali mbali ya serikali.”
OSHA ni taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira, Vijana na wenye
Ulemavu ambayo husimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama
Mahali pa Kazi ya mwaka 2003. Kupitia sheria hii, OSHA husajili maeneo ya
kazi na kuyafanyia ukaguzi kuhakikisha kwamba yanazingatia viwango vya
kiusalama na afya na hivyo kuwakinga wafanyakazi dhidi ya magonjwa na
ajali zitokanazo na mazingira ya kazi.
Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Andrew Massawe, akiongoza kikao baina yake na menejimenti ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) alipotembelea ofisi za taasisi hiyo hivi karibuni kufuatilia utekelezaji wa maelekezo na miongozo ambayo ofisi yake imekuwa ikiitoa.
Wajumbe wa menejimenti ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) wakimfuatilia Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Andrew Massawe, katika kikao alichokiendesha alipotembelea ofisi za Wakala za jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...