Na Karama Kenyunko, Michuzi Globu ya jamii
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema haiwezi kuzuia Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita kuondolewa kwenye nafasi yake kwa sababu hakuna uthibitisho juu ya uwepo wa kikao cha kumuondoa madarakani wala hasara atakayoipata iwapo ataondolewa.

Akisoma uamuzi huo leo Januari 10, 2020 mahakamani hapo,  Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega  amesema Wakili wa mwombaji, Hekima Mwasipu alipokuwa akiwasilisha maombi hayo alikuwa na wajibu wa kuthibitisha kwa undani uwepo wa kumwondoa meya Mwita madarakani.

"Ni lazima Mahakama ipewe maelezo kuhusu uwepo wa kikao cha kumwondoa  katika nafasi yake  ya Umeya ili mahakama hiyo iweze kufikia maamuzi ya kutoa haki... kwa hiyo, Mahakama hii inatupilia mbali hoja za kutaka muombaji (Mwita) kubaki madarakani kwa sababu hoja za Wakili wa muombaji hazina miguu ya kusimamia kwa kushindwa kufata vigezo ikiwemo kueleza uwepo wa kikao cha kutaka kumtoa madarakani na hasara ambayo angeipata," amesema Hakimu  Mtega.

Hata hivyo, Hakimu Mtega wakati akiendelea kusoma uamuzi ghafla alisimama kusoma kwa takribani dakika 13  kabla hajaendelea tena, ambapo alitumia hoja kuu mbili kutoa uamuzi huo ikiwemo je, muombaji alikuwa na wajibu wa kuthibitisha hasara atakayoipata endapo mahakama haitatoa amri ya kusema abaki kwenye nafasi yake na kama kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa  au kusikilizwa.

Amesema, ili kitu kibaki katika nafasi yake inatakiwa kuwepo kwa zuio la awali  kuwezesha  kitu hicho kubaki katika nafasi yake na kisiondoshwe na kwamba kwa maoni yake Wakili wa muombaji alikuwa na wajibu wa kuthibitisha uwepo wa kikao cha kumuondoa madarakani Mwita na alipaswa kutoa uthibitisho.

"Alipaswa kueleza sababu za kutaka muombaji abaki kwenye nafasi yake, pia ilibidi ajiulize je, muombaji atapata hasara yoyote endapo mahakama itashindwa kutoa uamuzi, hivyo hoja hizo zilipaswa kutolewa mahakamani," amesema.

Akizungumzia hoja ya kesi kutajwa, Hakimu Mtega amesema kesi hiyo ilikuja  Januari 8, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na si kusikilizwa  kwani bado mawakili walikuwa katika hatua ya kubadilishana nyaraka lakini wakili wa wajibu maombi ambaye ni Naibu Wakili Mkuu wa Serikali,  Gabriel  Malata alipotoka kwa kutaka mahakama iendelee na usikilizwaji wakati kesi hiyo imekuja kwa  kutajwa.

Amesisitiza kuwa  katika kesi ya media ni lazima mahakama ihakiki taratibu zote za usikilizaji wa shauri zinafuatwa kwa  mawakili kubadilishana nyaraka ambazo ni hati ya kiapo, hati ya kiapo kinzani na majibu ya hati ya kiapo kinzani ndipo kesi ianze kusikilizwa na kwamba shauri la msingi namba 3/2020 itasikilizwa Januari  13, mwaka huu.

Katika kesi ya msingi, Mwita  anapinga mchakato wa kuondolewa kwenye nafasi yake ya umeya umekiuka utaratibu, kudaiwa kupendelea madiwani wa chama chake katika uundaji wa kamati mbalimbali bila kumshirikisha Mkurugenzi wa Jiji,  kutumia mali (gari) la ofisi vibaya na kushindwa kufanya matumizi ya hisa za  Shirika la Usafiri Dar es Salaam  (UDA).

 Aliyekuwa Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita, akiingia katika mahakama ya hakimu mkazi kisutu jijini Dar es Salaam leo, kabla ya ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutupilia mbali maombi yake ya kutetea nafasi yake ya Umeya wa Jiji la Dar es Salaam.
  Aliyekuwa Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita akiteta jambo na mmoja wa wafuasi wake leo katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
  Aliyekuwa Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita, akitoka katika mahakama ya hakimu mkazi kisutu jijini Dar es Salaam leo, mara baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutupilia mbali maombi yake ya kutetea nafasi yake ya Umeya wa Jiji la Dar es Salaam.
Aliyekuwa Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita kushoto akiwa na diwani wa kata ya Kimanga Manase  Mjemawakitoka mahakamani wakiwa wameshikana mikono mara baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutupilia mbali maombi ya Mwita ya kutetea nafasi yake ya Umeya wa Jiji la Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...