MEYA wa Jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita amewasilisha maombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akiomba Mahakama itoe amri ya kusitisha mchakato wa kung'olewa kwenye nafasi hiyo hadi maombi yake ya msingi yatakaposikilizwa.
Mwita ambaye anawakilishwa na Wakili Hekima Mwasipu amewasilisha maombi hayo leo Januari 8,2020 dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Halmashauri ya Jiji hilo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Maombi hayo ambayo yanalenga kuwazuia Mkuu wa Mkoa na Halmashauri kujihusisha katika mchakato wa kumng'oa kwenye nafasi ya Umeya wa jiji hilo yamewasilishwa chini ya hati ya dharula na yametajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega.
"Tunaomba Mahakama izuie mchakato huo au hata kama kutakuwa na kikao chenye ajenda hiyo isizungumziwe na Mkuu wa Mkoa pamoja na Halmashauri wazuiliwe kufanya mchakato huo. Mahakama isipofanya hivyo mleta maombi (Mwita) hatapata haki yake ya kusikilizwa,"alidai Mwasipo.
Akijibu hoja hiyo, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Gabriel Malata amedai kesi hiyo imekuja kusikilizwa chini ya hati ya dharura na kwamba hawajui kama kuna kitu chochote kinachoweza kutokea kuhusu kung'olewa kwa mleta maombi (Meya), huyo hivyo, aliiomba mahakama kukataa maombi hayo kwa gharama.
Amedai hakuna mazingira ya moja kwa moja yanayoashiria kwamba kwenye kikao kitakachofanyika kutakuwa na ajenda inayohusu kumtoa katika nafasi hiyo meya huyo.
Hata hivyo, jopo la mawakili wa serikali tayari limewasilisha mapingamizi kupinga maombi ya msingi yaliyopo mahakamani hapo. Kesi hiyo itatolewa maamuzi kesho Mtega Januari 9,mwaka 2020
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...