Mkazi wa Mbagala Rangi tatu jijini Dar es Salaam, Abuu Kimboko (43) akitoka katika kahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo mara baada ya kusomewa mashitaka ya kukabiliwa na tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya aina ya Heroine na utakatishaji fedha.
Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii.
MKAZI wa Mbagala Rangi tatu jijini Dar es Salaam, Abuu Kimboko (43) pichani amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya aina ya Heroine na utakatishaji fedha.
Akisoma hati ya mashtaka, mbele ya Hakimu Mkazi, Salum Ally, Wakili wa Serikali, Elia Athanas akisaidiana na Tuly Helela, amedai kati ya Desemba Mosi na 29, 2019 huko Mbagala Zakhem wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, Kimboko alijihusisha na biashara ya dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 273.45.
Imeendelea kudaiwa kuwa, katti ya Desemba Mosi na 29, mwaka jana maeneo ya jiji la Dar es Salaam, mshitakiwa alijipatia sh. 990,000 huku akifahamu kuwa fedha hizo ni mazalia ya biashara ya dawa za kulevya.
Hata hivyo, mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi hadi itakapopata kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, upelelezi wa kesi hiyo uko mbioni kukamilika hivyo, aliomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 28, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na mshitakiwa alirudishwa rumande kwa sababu haina dhamana kisheria.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...