Naibu Katibu Mkuu Dkt. Dorothy Gwajima, akizungumza na timu ya Afya ya Manispaa ya Songea hawapo pichani

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,
Dkt. Jairy Khanga, akizungumza eneo la Zahanati ya Mtakanini katika
Halmashauri ya Namtumo mkoani Ruvuma.

Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya
Mtakanini, Magreth Pastory akitoa ufafanuzi juu ya maamuzi waliyoyafikia
na kamati ya kituo katika kukiendeleza kituo hicho na mipango iliyopo.

Naibu Katibu Mkuu akiwa
ameambatana na baadhi wa Wajumbe kutoka TAMISEMI na Mkoa wakikagua Jengo
ambalo lilikuwa linabishaniwa juu ya hatma yake.
(Picha na OR-TAMISEMI)
……………
Na. Atley Kuni, Namtumbo: RUVUMA
Serikali
imezitaka Halmashauri ambazo zilipelekewa fedha kwaajili ya ujenzi na
upanuzi wa Vituo vya Afya pamoja na Zahanati kuacha mara moja mipango
yakubomoa baadhi ya majengo yaliyokuwepo hapo awali na badala yake
wayafanyie tathmini ya kina na ikiwezekana wayafanyie maboresho.
Rai hiyo
imetolewa mkoani Ruvuma na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI,
anayeshughulikia Afya, Dkt. Dorothy Gwajima akiwa njiani akitokea Mikoa
ya Songwe na Rukwa alipokwenda kwa shughuli za kikazi kukagua miradi
mbali mbali ya afya kwenye mikoa hiyo.
Dkt. Gwajima,
amefikia hatua hiyo akiwa katika Zahanati ya Mtakanini iliyopo katika
Halmashauri ya Namtumbo mkoani Ruvuma, ambapo Zahanati hiyo ilipelekewa
kiasi cha shilingi milioni 400 kwaajili ya upanuzi wa kituo hicho lakini
tayari ilikuwa imesha anza ujenzi wa jengo la uzazi.
Halmashauri hiyo
baada yakupokea fedha, yalitokea malumbano yakutokuelewana kwa baadhi ya
viongozi wa eneo hilo na kutaka kubomoa jengo hilo kwa madai kuwa
lilikuwa tofauti na ramani zilizo tolewa na ofisi ya Rais TAMISEMI kwa
ujenzi wa vituo vya afya na zahanati.
“Kuyatelekeza
majengo ambayo yalisha jengwa hapo awali au kuyabomoa bila kufanya
tathmini ya kina itakuwa nikupoteza fedha za serikali, hivyo wito wetu
Ofisi ya Rais TAMISEMI, tunaielekeza Mikoa na Halmashauri kama kuna
majengo yalishajengwa waanze kwakuyafanyia tathmini na yanayoweza
kurekebishika basi yafanyiwe hivyo na sio kuyatelekeza au kuyabomoa”,
alisema Dkt. Gwajima.
Kwa upande wake
Mratibu wa ujenzi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Shaban Sonda,
alisema Zahanati hiyo ya Mtakanini ilipokea fedha hizo ili kufanya
upanuzi wa kituo lakini kwakuwa tayari walikuwa na jengo la uzazi ni
vema fedha hizo zifanye maboresho sambamba na kujenga majengo mengine
yaliyo kusudiwa ikiwapo jengo la upasuaji.
Akizungumza
wakati wa ziara hiyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt. Jairy Khanga
alisema, Mkoa huo ulipokea kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya
upanuzi wa Zahanati za Mtakanini, Matimila pamoja na Magagula, ambapo
amedai kuwa, nguvu kubwa itaelekezwa kwenye majengo ya Wodi ya uzazi,
upasuaji pamoja na maabara lakini pia nyumba za watumishi kulingana na
mahitaji kwa kila Zahanati.
Kwa mujibu wa
Mganga mfawidhi wa kituo cha Mtakanini, Tabibu Magreth Pastory, alisema
kituo cha Mtakanini kwa sasa kinahudumia zaidi ya watu 300 hivyo upanuzi
wa kukifanya kuwa kituo cha Afya umekuja kwa wakati muafaka.
Ofisi ya Rais
TAMISEMI, imeendelea kuboresha miundombinu ya Afya na huduma zake kote
nchini, shabaha ikiwa nikuhakikisha nchi inakuwa na watu wenye afya
njema watakao shiriki ujenzi wa taifa kwa shughuli za maendeleo na
kuifikisha nchi katika uchumi wa kati ifikapo 2025.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...