Na Said Mwishehe,Michuzi Globu ya jamiii
SIMBA baba lao! Ndivyo unavyoweza kuzungumzia kutokana na kabumbu safi na lenye ufundi wa hali ya juu waliloonesha katika mchezo wao dhidi ya timu ya Mbao FC ya jijini Mwanza na kuibuka na ushindi wa bao 2-1.
Katika mchezo huo wa Simba na Mbao ambao umechezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini humo ulikuwa wa vuta nikuvute huku kila timu ikicheza mpira wa ushindani mkubwa na kadri dakika zilizovyosonga mbele ndivyo utamu wa mchezo ulivyozidi kunoga.
Simba ambao walikuwa ugenini katika mchezo huo walionesha kusakata soka safi ambapo kila mchezaji kuanzia safu ya ulinzi ,kati na ushambuliaji walionekana hitaji lao kwenye mchezo huo ni alama tatu ili kuendelea kujikita kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na alama 38 baada ya ushindi wa leo dhidi ya Mbao.
Bao la kwanza la Simba lilipatikana dakika ya 44 baada ya kiungo wa pembeni Hassan Dilunga kupiga shuti kali la mguu wake wa kushoto ambalo lilimshinda mlinda mlango wa Mbao na kuingia nyavuni moja kwa moja .
Hivyo hadi wanakwenda mapumziko ya dakika 45 za kwanza walikuwa wakiongoza kwa goli moja.
Kipindi cha pili kilianza kwa kila timu kusoma mchezo wa mwenzake. Muda Mwingi wachezaji wa Simba walionekana kutumia akili zaidi katika mchezo huo.Pamoja na mashambulizi hayo, wachezaji wa Mbao nao muda wote walikuwa imara zaidi hasa kwenye safu ya ulinzi na hivyo Simba kuwa na wakati mgumu kupenya ngome ya Mbao.
Kadri dakika zilivyosonga mbele Simba waliendelea kujipanga na hatimaye kupata bao la pili kupitia kwa mchezaji wake Jonas Mkude dakika ya 46 na hivyo kujihakikishia alama tatu.
Hata hivyo Mbao FC nao walirudi mchezoni na kujipanga vema hasa safu ya ushambuliaji na kufanikiwa kupata goli moja kupitia mshambuliaji wao Waziri Junior katika kipindi hicho cha pili .
Hivyo hadi dakika 90 zinamalizika Simba 2 na Mbao FC 1.Kwa matokeo hayo Simba wameendelea kujikita kileleni mwa Ligi hiyo kwa kujikusanyia alama 38 huku wakiendelea kuwaacha wapinzani wao Yanga kwa mbali.
Baada ya mchezo huo Simba wataendelea kubakia jijini Mwanza kwa ajili ya mchezo wao mwingine unaotarajia kufanyika Jumapili ya wiki hii dhidi ya timu ya Alliance ya jijini humo.
Kwa kukumbusha tu Simba wamecheza.mchezo wa leo wakiwa wametoka kupoteza mchezo wao dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro katika fainali ya Kombe la Mapinduzi ambapo Mtibwa waliibuka mabingwa kwa kuifunga simba goli moja na kufanikiwa kutawazwa mabingwa wapya wa michuano hiyo .
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...