Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akiwasilisha mapendekezo ya serikali ya mpango wa maendeleo wa Taifa na ya kiwango na ukomo wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2020/21.
Waziri Mkuu Mhe Kassism Majaliwa akiongoza kikao cha uwasilishaji wa taarifa ya mapendekezo ya serikali ya mpango wa maendeleo wa Taifa na ya kiwango na ukomo wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2020/21.
Waziri Mkuu Mhe Kassism Majaliwa akiongoza kikao cha uwasilishaji wa taarifa ya mapendekezo ya serikali ya mpango wa maendeleo wa Taifa na ya kiwango na ukomo wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2020/21.
Mbunge wa Jimbo la Mtama (CCM) Mhe Nape Nnauye akifuatilia uwasilishaji wa mapendekezo ya serikali ya mpango wa maendeleo wa Taifa uliosomwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango leo Jijini Dodoma.
Charles James, Michuzi TV
SERIKALI imesema mpango wa maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2020/21 ni kutekeleza vipaumbele vilivyoainishwa katika mpango wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2016/17 hadi 2020/21.
Vipaumbele hivyo ni viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu, uboreshaji wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji.
Vingine ni kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa Mpango ambalo eneo hilo limelenga kuboresha ufuatiliaji, tathimini na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa mpango ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo na taasisi za utekelezaji wa mpango.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango leo jijini Dodoma wakati akiwasilisha mapendekezo ya serikali ya mpango wa maendeleo ya Taifa na ya kiwango na ukomo wa bajeti ya serikali mwaka 2020/21.
Dk Mpango amesema miradi itakayotekelezwa katika eneo ka kukuza uchumi wa viwanda ni kujenga viwanda vingi vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini zikiwemo kilimo, madini na gesi asilia ili kukuza mnyororo wa thamani.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi asilia, uanzishwaji na utekelezaji wa kanda maalum za kiuchumi na kongane za viwanda pamoja na viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo, uvuvi na mifugo na kuongeza thamani ya madini.
" Kwenye kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu ni miradi inayotekelezwa kwenye eneo hilo ambayo imelenga kuboresha upatikanaji wa elimu, afya bora, ujuzi na huduma za maji safi na salama.
Pia tumepanga kuendeleza ujenzi na ukarabati sa miundombinu ikijimuisha miundombinu ya nishati, usafirishaji, ununuzi na ukarabati wa ndege, meli na vivuko. Hapa ndio unapoona tumeanzisha miradi ya kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere, kuboresha shirika la ndege kwa kununua ndege mpya 11 pamoja na ujenzi wa reli ya kisiasa ya Standard Gauge," Amesema Waziri Mpango.
Akizungumzia tathimini ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2019/20, Dk Mpango amesema jumla ya Sh trilioni 12.25 zilitengwa kugharamia miradi ya maendeleo ambapo Sh trilioni 9.24 zilikua fedha za ndani na Sh trilioni 2.51 ni fedha za nje.
Kuhusu mwenendo wa hali ya uchumi nchini, Waziri Mpango amesema mapendekezo ya serikali ya mpango wa maendeleo wa Taifa na kiwango cha ukomo wa bajeti ya serikali mwa mwaka 2020/21 ni ya mwisho katika utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2016/17 - 2020/21 wenye dhima ya kujenga uchumi wa viwanda katika kuchochea mageuzi ya uchumi wa watu.
" Mapendekezo yamezingatia ilani ya CCM ya 2015, katika kipindi hicho cha utekelezaji wa mpango mafanikio makubwa yamepatikana kupitia Rais Dk John Magufuli ambapo katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2019 pato la Taifa limekua kwa wastani wa asilimia 6.9 kwa mwaka.
Ukuaji huu umechochewa na sekta ya ujenzi kufuatia kuongezeka kwa uwekezaji hususani katika miundombinu ya barabara, reli na viwanja vya ndege na kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za maji, kuimarika kwa usafirishaji, uzalishaji wa madini na kuongezeka kwa mazao ya kilimo, " Amesema Dk Mpango.
Akizungumzia sera za mapato na matumizi kwa mwaka 2020/21, Dk Mpango amesema mapato ya serikali yanatarajiwa kuongezeka na hivyo kuwez kugharamia miradi mikubwa ya kimkakati.
Amesema serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia sheria ya bajeti sura 439, sheria ya fedha za umma sura 348 lengo likiwa kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi mikubwa ya kimkakati na muhimu.
Waziri Mpango amesema kwa kuzingatia sera za bajeti kwa mwaka 2020/21 Sh trilioni 34.88 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika. Mapendekezo ya kiwango cha ukomo wa bajeti ya 2020/21 yamezingatia mahitaji halisi ya ugharamiaji wa miradi mikubwa, ulipaji mishahara na deni la serikali pamoja na utekelezaji wa vipaumbele vya Taifa.
Kwa mwaka 2020/21 serikali imepanga kutumia jumla ya Sh trilioni 34.88 kaa matumizi ya kawaida na maendeleo, kati ya fedha hizo Sh trilioni 21.98 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh trilioni 12.90 kwa ajili ya maendeleo sawa na asilimia 37.0 ya bajeti yote.
Uwasilishaji wa taarifa hiyo umehudhuriwa na Waziri Mkuu, Mhe Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge, Mhe Job Ndugai, Mawaziri, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, Wabunge pamoja na Wandishi wa Habari.
Spika wa Bunge, Job Ndugai akitoa maelezo ya awali kabla ya Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango kuwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa na Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/2021.katikati ni Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa na Dkt. Mpango, tukio hilo limefanyika katika Ukumbi wa Msekwa Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akiwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa na Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/2021. tukio hilo limefanyika katika Ukumbi wa Msekwa Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai na Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson.
Katibu wa Bunge Ndugu Stephen Kagaigai (mwenye miwani) pamoja na baadhi wa mawaziri na wabunge wakifuatilia uwasilishwaji wa Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa na Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/2021 uliofanywa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango. tukio hilo limefanyika katika Ukumbi wa Msekwa Jijini Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...