Fundi Sanifu Madini kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Marko Massaba (katikati) akihakiki madini yaliyopokelewa kutoka mikoani kwenye soko hilo mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kushoto) akibadilishana mawazo na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) kwenye Soko la Kimataifa la Madini la Dar es Salaam wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwenye soko hilo tarehe 15 Machi, 2020. Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Ally Maganga (katikati) akielezea shughuli zinazofanywa na Soko la Kimataifa la Madini la Dar es Salaam kwawajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini mara kamati hiyo ilipofanya ziara kwenye soko hilo tarehe 15 Machi, 2020.
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imepongeza uanzishwaji na utendaji wa Soko la Kimataifa la Madini la Dar es Salaam na kueleza kuwa kuanzishwa kwake kumepunguza kwa kiasi kikubwa mianya ya utapeli.
Hayo yamesemwa leo tarehe 15 Machi, 2020 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula kwenye majumuisho mara baada ya kamati hiyo kufanya ziara kwenye soko hilo ikiwa ni sehemu ya ziara yake kwenye miradi inayosimamiwa na Wizara ya Madini.
Ziara hiyo ilishirikisha Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mlabwa, AfisaMadini Mkazi wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Ally Maganga, wataalam kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini.
Alisema kuwa, kabla ya kuanzishwa kwa Soko la Madini kulikuwepo na matukio ya utapeli kwenye biashara ya madini jijini Dar es Salaam hali iliyosababisha wafanyabiashara wengi wa madini kupata hasara kubwa huku Serikali ikikosa mapato yake.
Katika hatua nyingine, Kitandula aliitaka Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Tume ya Madini kuendelea kuboresha soko hilo huku ikitatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo wafanyabiashara wa madini wanaoendesha shughuli zao kwenye soko hilo.
Aidha, aliitaka Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Tume ya Madini kuwahakikishia usalama wafanyabiashara wa madini wanaosafirisha madini kutoka mikoani kwenda
kwenye soko hilo.
Wakati huohuo Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alisema kuwa Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Tume ya Madini inaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza kwenye masoko ya madini lengo likiwa ni kuhakikisha yanakuwa na mchango mkubwa kwenye ukusanyaji wa maduhuli.
Pia Nyongo aliwapongeza wafanyabiashara wa madini kwa kuwa wazalendo na kufuata Sheria ya Madini na kanuni zake kwenye utendaji wa shughuli zao.
Awali akiwasilisha taarifa yake kwa Kamati hiyo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Ally Maganga alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwa soko hilo Julai 17, 2019 hadi Februari, 2020 liliweza kufanya biashara ya madini ya vito yenye uzito wa karati 4,887 yenye thamani ya shilingi bilioni 1.8 na madini ya dhahabu yenye uzito wa kilogramu 46.7 na thamani ya shilingi bilioni 5.06.
Aliongeza kuwa, katika kipindi husika Serikali kupitia Tume ya Madini ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 382.6 ikiwa ni tozo za mrabaha wa madini na ada ya
ukaguzi.
Alisisitiza kuwa Soko la Madini limekuwa la kipekee kwa kupokea madini yanayotokea katika masoko mengine ndani ya nchi ambapo katika kipindi husika kiasi cha kilogramu 651.089 cha madini ya dhahabu kimepokelewa na wahusika kusafirisha madini hayo nje ya nchi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...