WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameonya tabia ya baadhi ya wenyeviti wa vijiji wanaofanya biashara ya ardhi waache na badala yake amewataka wajihusishe katika kutekeleza majukumu yao ya msingi.
Ameyasema leo(Jumatano, Machi 4, 2020) wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Bokwa wilayani Kilindi akiwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Tanga.
Waziri Mkuu amesema tabia ya baadhi ya wenyeviti wa vijiji kujihusisha na biashara ya uuzaji wa ardhi inachangia kuwepo kwa migogoro, hivyo amewataka wasijihusishe na masuala hayo.
“…Wanaouza ardhi za vijiji bila ya kuwa na vibali vya halmashauri wachukuliwe hatua kwa sababu ndio wanaosababisha migogoro ya ardhi. Viongozi acheni tabia ya kuwaingiza wananchi kwenye migogoro.”
Pia, Waziri Mkuu ameonya tabia ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima.“Haikubaliki na haiingii akilini katika hali ya kawaida mtu amelima shamba lale la chakula alafu mwingine anaenda kuingiza mifugo haikubaliki.”
Waziri Mkuu ameongeza kuwa “kama unadhani mahindi ndio chakula bora cha ng’ombe wako lima ulishe mifugo. Hakuna Mtanzania aliyeko juu ya sheria kama kuna mtu ameua kwa kulinda ng’ombe wake, Mkuu wa Wilaya fanya uchunguzi wa jambo hilo na hatua zichukuliwe.”
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi waliodai kuwa kuna mkulima ameuawa na mfugaji kutokana na mgogoro uliotokea wakati mfugaji alipoingiza mifugo kwenye shamba la mkulima.
Akizungumzia kuhusu mgogoro wa mpaka kati ya wilaya ya Kilindi (Tanga) na Kiteto (Manyara) amesema suala hilo iachiwe Serikali kwani tayari imeshaanza kulishughulikia.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema wilaya ya Kilindi itajengewa hospitali ya wilaya ili kuwapunguzia wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Pia, Waziri Mkuu aliwataka wananchi waendelee kuiamini Serikali yao na kwamba changamoto mbalimbali zinazowakabili zikiwemo za upatikanaji wa huduma za maji, umeme na miundombinu ya barabara zitafanyiwa kazi.
Kadhalika, Waziri Mkuu amezindua mradi wa maji wa Bokwa na amesema kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati mizuri inayolenga kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo na wilaya ya Kilindi.
Waziri Mkuu amesemaSerikali kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao.
Awali, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa kituo cha afya cha Mswelo kilichopo kwenye kata ya Kwediboma, ambapo amesema awali Serikali ilitoa sh. milioni 300 kwa ajili ya ujenzi huo na itaongeza sh. milioni 200 ili kituo hicho kikamilike.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...