Na Amiri kilagalila,Njombe
Timu ya wataalamu kutoka Benki ya Dunia na Ofisi ya Rais TAMISEMI imekagua mwenendo wa shughuli za ujenzi wa soko na stendi halmashauri ya mji wa Njombe ikiwa ni hatua za mwishoni kuelekea kumalizika kwa programu hiyo inayofadhiliwa na benki ya Dunia na kukagua mapendekezo ya mradi mpya wa barabara zinazotarajiwa kuingizwa kwenye mpango katika Programu zijazo.
Changamoto kubwa iliyobainika katika utekelezaji wa miradi hiyo ni kuchelewa kwa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani(VAT Exemption) ambao umesababisha wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kununua vifaa vya ujenzi na gharama ya VAT na wakati mwingine kukwama kwa shughuli za ujenzi kutokana na changamoto hiyo.
Akiwasilisha taarifa ya mwenendo wa utekelezaji wa miradi hiyo Mchumi wa halmashauri ya mji wa Njombe Emma Lunojo amesema, halmashauri iliamua kufanya utekelezaji wa miradi ya soko na stendi kufuatia uchakavu wa miundombinu iliyokuwa ikitumika jambo lililopekea uwepo wa kero kwa watumiaji wakiwemo wafanyabiashara na wasafiri.
Vile vile amesema kufuatia ujenzi wa miradi hiyo mpaka sasa wananchi wa mji wa Njombe wameendelea kunufaika kwa namna mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongeza fursa za ajira, kuongezeka kwa thamani ya ardhi katika maeneo ya mradi na halmashauri kuweza kujiongezea mapato kupitia kuongezeka kwa vyanzo vya makusanyo.
Wakizungumza mara baada ya kutembelea miradi hiyo timu hiyo ya wataalamu imesema,licha ya kuwa miradi hiyo inazisaidia halmashauri kuongeza mapato ni vyema kuangalia miradi itakayowawezesha wananchi kuongeza kipato, kuboresha hali ya maisha, kuboresha maeneo ambayo hayajajengwa au kupangwa ili kuweza kuinua hadhi ya maeneo hayo na kupambana na umaskini jambo ambalo limekuwa ni kipaumbele kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya Benki ya Dunia.
Halmashauri ya mji Njombe ni moja kati ya halmashauri 18 zinazotekeleza mradi wa uboreshaji na uimarishaji miji (ULGSP) ambapo kwa sasa inatekeleza mradi wa ujenzi wa stendi na soko la kisasa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...