SHIRIKA la Fedha duniani (IMF) limetoa taarifa ya mwenendo wa ukuaji wa uchumi kwa Tanzania na kwa mujibu wa taarifa hiyo IMF imeelzwa kufurahishwa na ukuaji wa uchumi, kupungua kwa mfumuko wa bei, kutengeneza ajira pamoja na  kuongezeka kwa uwekezaji unaofanywa na Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi katika sekta za elimu na afya.

Taarifa hiyo iliyotolewa Machi 05 mwaka huu imeeleza, timu ya  IMF wakiongozwa na Enrique Gelbard walitembelea Tanzania kuanzia Februari 20 hadi Machi 04 mwaka huu na baada ya kujadili masuala kadha wa kadha wamekuja na taarifa hiyo iliyobeba vipengele vitano ikiwa ni pamoja na  uchumi wa Tanzania kukua kila mwezi na kufikia kiwango cha asilimia 6.

Pia taarifa hiyo imeeleza kuwa shirika la Fedha Dunia (IMF)  limefurahishwa na ushirikiano kutoka kwa Waziri wa Fedha Dkt. Philip Mpango, Gavana wa Benki kuu ya Tanzania Profesa. Florens Luoga pamoja na wafanyakazi wa Serikali kutoka katika  mabenki na sekta nyingine za maendeleo zilizohusisha wawekezaji binafsi na mamlaka za umma na kueleza kuwa wanataraji kujadili ripoti ya nne makala ya mashauriano mwezi Mei mwaka huu.

Akitoa muhtasari wa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari leo jijini Arusha,Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Utafiti na Sera za Uchumi kutoka Benki kuu ya Tanzania (BOT) Dkt.Suleiman Missango amesema kuwa taarifa ya IMF imeeleza mwenendo na ukuaji wa uchumi wa nchi pamoja na mwelekeo wake.

"Taarifa hii imeeleza kuwa uchumi wetu umekua ukifanya vizuri,  wamesema kuwa uchumi wa Tanzania kwa mwaka 2019/2020 umekua kwa asilimia 6 na kueleza kuwa uchumi utakua zaidi ya hapo"
Ameeleza.

Amesema kuwa uchumi wa nchi kwa mwaka 2019/2020  umekua kwa asilimia 6 na wanamategemeo ya uchumi huo kukua kwa asilimia saba kwa siku za mbeleni na hiyo ni kutokana na uwekezaji unaofanywa na Serikali na sekta binafsi ambapo miradi mbalimbali ikiwemo nishati, miundombinu pamoja na uwekezaji mkubwa katika sekta za elimu na afya ambao umekuwa ukiendelea kufanyika.

Kuhusiana na mfumuko wa bei Dkt. Missango amesema taarifa hiyo imeeleza kuwa mfumuko wa bei kwa mwaka jana  ulikua asilimia 3.5 na mwezi Januari ulifikia asilimia 3.7 na kueleza kuwa mfumuko wa bei utaendelea kuwa mdogo zaidi kama taarifa hiyo ilivyoeleza.

Aidha amesema kuwa taarifa hiyo ya IMF imeeleza kufurahishwa na mwenendo wa biashara unaofanywa na Tanzania kwa kushirikiana na nchi za nje, kwani  umeleta tija ikiwemo uhifadhi wa fedha za kigeni ambapo Tanzania ina fedha za ziada za kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi miezi mitano.

Kwa upande wa sekta ya fedha taarifa hiyo imeelezwa kuridhishwa na mwenendo wa matumizi na mapato ya Serikali na kushauri juhudi zaidi kuendelea kufanyika ili kuboresha zaidi.

Vilevile IMF imeeleza kuridhishwa na  mwenendo wa sekta ya afya na kushauri juhudi zaidi ziendelee kufanyika huku wakipongeza sekta ya elimu na maji katika uboreshwaji unaoendelea kufanyika.

Dkt. Missango amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika Kuhakikisha uchumi wa nchi unakua zaidi na hiyo ni pamoja na matumizi bora ya mapato ya Serikali.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Utafiti na Sera za Uchumi kutoka Benki kuu ya Tanzania (BOT) Dkt.Suleiman Missango

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...