Charles James, Globu ya Jamii
WAZIRI Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye amekabidhiwa rasmi kadi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) leo hii jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally.
Sumaye amekabidhiwa kadi hiyo leo baada ya kutangaza kurejea CCM Februari 10 mwaka huu akitokea Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kile alichoeleza kutoridhishwa na mwenendo wa chama hicho kikuu cha upinzani.
Akizungumza wakati akimkabidhi kadi, Dk Bashiru amesema kurejea kwa Sumaye ni faida kubwa kwa CCM kutokana na uzoefu alionao ndani ya chama hicho lakini pia serikalini alipohudumu kama Waziri Mkuu kwa miaka 10 katika serikali ya awamu ya tatu.
Dk Bashiru amesema ni jambo la busara pia kuona mstaafu kama Sumaye akiamua kuchukulia kadi yake Makao Makuu ya Nchi badala ya Manyara ambapo ndipo anapotokea jambo linaloonesha kwamba CCM ni chama cha watanzania wote.
" Mzee Sumaye amesema alitaka kuchukulia kadi yake hapa kwa sababu hata ile ya kwanza aliipatia hapa. Hii ni heshima kubwa ambayo Mstaafu ameamua kuionesha kwa Dodoma, sasa wana-CCM wa Makao Makuu mtumieni mzee huyu katika kuimarisha chama chetu.
Lakini pia kitendo cha kuchukulia kadi hapa badala ya mkoani kwake Manyara ni kielelezo cha kwamba chama chetu ni chama cha watanzania na kila mmoja ana haki ya kuchukua kadi popote anapopataka, tulinde heshima hii ya chama chetu," Amesema Dk Bashiru.
Akizungumzia ugonjwa wa Corona ambao umekua gumzo duniani kwa sasa, Dk Bashiru ameagiza Umoja wa Vijana wa Chama hicho (UVCCM), kupita maeneo yote yenye mkusanyiko ikiwemo sokoni, mnadani na stendi na kutoa elimu kwa watanzania ili waweze kujikinga na maambukizi.
Amewataka wanachama wa CCM kuhamasisha wananchi kufuata ushauri wote wa kitaalamu ambao umekua ukitolewa na wataalam wa afya pamoja na maelekezo yanayotolewa na viongozi wa serikali katika kipindi hiki.
" Nimeona baadhia ya maeneo ya sokoni kama Mwananyamala hakuna vitakasa mikono wala hatua zozote zinazochukuliwa lakini maeneo kama Mlimani City kuna vifaa vyote hadi Kipimo cha joto, ndugu zangu huu ugonjwa hauchagui tajiri wala maskini, tuchukue tahadhari," Amesema Dk Bashiru.
Kwa upande wake Sumaye amemshukuru Dk Bashiru kwa heshima kubwa aliyompa ikiwemo kumpokea wakati akirejea tena CCM lakini pia na leo kuja kumkabidhi kadi hiyo ya uanachama.
" Niwashukuru wote mliojitokeza kushuhudia kukabidhiwa kwangu kadi, nitatumia uzoefu wangu kuzidi kukiimarisha chama chetu ili tuzidi kuwatumikia watanzania ambao wametuamini na kutupa ridhaa ya kuwatumikia.
Wakati naondoka CCM nilisema naondoka sina chuki na mgombea, sina chuki na viongozi wake, lakini sasa mtu anauliza kama ulikua huna chuki kwanini uliondoka? Haya yote nitakuja kuyaeleza siku nyingine, " Amesema Sumaye.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM, Dk Bashiru Ally (kulia) akimkabidhia kadi ya uanachama wa chama hicho Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye leo jijini Dodoma. Anaeshuhudia katikati ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma.
Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akizungumza na baadhi ya viongozi wa kamati ya siasa ya Mkoa wa Dodoma na wandishi wa habari leo wakati wa tukio la kumkabidhi kadi ya uanachama Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.
Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akizungumza na wandishi wa habari na baadhi ya viongozi wa chama hicho leo jijini Dodoma katika tukio la kumkabidhi kadi ya uanachama Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.
Waziri
Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye akila kiapo cha kuwa mwanachama wa CCM
baada ya kukabidhiwa kadi ya chama hicho na Katibu Mkuu, Dk Bashiru Ally
leo jijini Dodoma
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye akizungumza na wandishi wa habari baada ya kukabidhiwa kadi ya CCM leo jijini Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...