Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Tanzania imeendelea kuaminiwa kimataifa kufuatia jitihada mbalimbali inayofanya kwa ajili ya kupiga vita vitendo vya rushwa pamoja kuwekeza katika miradi mbalimbali inayolenga na kuboresha maisha ya wananchi, pamoja na kukuza uchumi wa nchi.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi alisema kuwa Machi 5, 2020 Shirika la Fedha Fedha Duniani (IMF) lilikamilisha taarifa yake ya tathmini kuhusu uchumi wa Tanzania.
“Katika taarifa hiyo IMF imesisitiza kuwa Uchumi wa Tanzania uko imara na wamefurahishwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni, mfumuko wa bei kuwa chini ya asilimia 5, mauzo ya bidhaa nje ya nchi kuongezeka, kuongezeka kwa kasi ya mabenki kutoa mikopo kwa sekta binafsi na kuwa na deni la taifa ni himilivu” alisema Dkt. Abbasi
“Katika kuonesha Tanzania inaaminika kimataifa, hivi karibuni tumesaini mikataba mitano na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), inayohusu utekelezaji wa miradi mitatu ya kimkakati kwa mkopo wa masharti nafuu ya Dola za Marekani milioni 495.59 ambayo ni sawa na TZS trilioni 1.14.” alisititiza Dkt. Abbasi
Aidha, alifafanua kuwa fedha hizo zitawezesha kutekeleza ujenzi wa miradi ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Msalato Jijini Dodoma kwa gharama ya dola za marekani milioni 271.63, ujenzi wa barabara ya Bagamoyo - Horohoro - Lungalunga – Malindi kwa kiwango cha lami yenye urefu wa km 120. 8 kwa gharama ya dola za marekani milioni 168.76 na dola milioni 55.2 kwa ajili ya Programu ya utawala bora na kuendeleza sekta binafsi.
- Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akiongea na waandishi wa habari, leo Machi 15, 2020 Jijini Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...