Na. Edward Kondela
Serikali imesema itahakikisha afya ya mifugo nchini inazidi kuimarika kwa Tanzania kudhibiti magonjwa mbalimbali ya mifugo ukiwemo wa miguu na midomo unaoathiri ng’ombe (FMD), ili nchi iweze kuuza nyama na mifugo yake katika masoko mbalimbali ya kimataifa.
Akizungumza leo (12.03.2020) ofisini kwake jijini Dodoma, alipokutana na mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Mkoa wa Dodoma Dkt. Moses Ole-Neselle, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel amesema afya ya mifugo ina mchango mkubwa katika soko la kimataifa na kwamba nia ya serikali ni kuhakikisha inaondokana na tatizo hilo pamoja na upatikanaji wa chanjo.
“Tunataka kujihakikishia kwamba hakuna magonjwa ya miguu na midomo kwa ng’ombe wetu hapa nchini, ili nchi yetu iweze kuuza nyama na mifugo katika masoko mbalimbali ya kimataifa na kuongeza ajira na pato la taifa, ambapo kwa sasa sekta ya mifugo inachangia kwa silimia 7.6 Katika pato la taifa na ndoto yetu ni kufikia asilimia 15.” Amesema Prof. Gabriel
Aidha Prof. Gabriel ameishukuru FAO katika miradi yake kutoa chanjo 400,000 katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania kwa ajili ya kudhibiti ugonjwa wa mdondo kwa kuku, na kuwakumbusha wafugaji kuelewa kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi inafanya kila jitihada ili wadau wa maendeleo wanapokuja hapa nchini waelezwe mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwemo miradi yanye tija kwa wafugaji.
Ameongeza kuwa nia ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina ni kuinua sekta ya kuku ambayo haihitaji mtaji mkubwa ambapo amesema kwa takwimu Tanzania ina takriban kuku milioni 79.1 na nia ya wizara ni kuona idadi hiyo inaongezeka zaidi kwani ni sekta inayotoa mapato kwa haraka zaidi.
Amefafanua kuwa kwa sasa wadau wa kuku wamekuwa wakilalamikia zaidi kutokuwa na bei ya uhakika ya kuku pamoja na changamoto ya afya ya kuku ukiwemo ugonjwa wa mdondo ambapo amesisitiza serikali inazidi kuishkuru FAO kwa miradi mbalimbali inayohusu kuboresha afya ya kuku hapa nchini ili wafugaji wapate unafuu wa kugharamia mifugo yao kwa kuwa inapokuwa na afya njema itasaidia kupata mazao bora.
Prof. Gabriel amekumbusha pia takwimu za FAO kuwa mtu mzima kwa kawaida anahitaji kunywa maziwa lita 200 kwa mwaka lakini hapa nchini takwimu ya mwaka 2018 inaonesha wastani wa kunywa maziwa kwa mwaka ni lita 49 pekee, na kuwaasa watanzania kunywa maziwa kwa wingi yanayochakatwa hapa nchini ili kuvifanya viwanda hivyo viweze kuongeza uzalishaji zaidi.
Katika sekta ya nyama pia katibu mkuu huyo amebainisha taarifa ya FAO inafafanua kuwa mtu mzima anahitaji kula kilogramu 50 kwa mwaka lakini kwa mujibu wa taarifa ya mwaka 2017 wastani ilikuwa kilogramu 10 na mwaka 2019 ilikuwa kilgramu 15 kwa mwaka.
“Tunafanya kila linalowezekana kuhakikisha mifugo iwe katika afya nzuri ili watanzania wale nyama na kunywa maziwa salama ili pia nchi iweze kuingia katika masoko mbalimbali ya nyama na mifugo nje ya nchini.” Amebainisha Prof. Gabriel
Kuhusu magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu Prof. Gabriel wakati akizungumza na mwakilishi wa FAO mkoani Dodoma Dkt. Moses Ole-Neselle, amesema taarifa zilizopo ni kwamba asilimia 60 ya magonjwa ya binadamu yanatoka kwa wanyama hivyo serikali inahakikisha inapunguza magonjwa ya mifugo kwa kuweka mkakati mzuri wa kuondokana na tatizo hilo kwa kuboresha afya za mifugo ili kupunguza gharama za matibabu ya magonjwa hayo kwa binadamu.
Mpango huu unasaidia kuboresha maabra za mifugo nchini na usalama wa wanyama, maabara ikiwemo ya TVLA itaweza kusaidia hududma ya matibabua.
Aidha kuhusu utekelezaji wa mradi wa FAO wa utoaji mafunzo ya ufuatiliaji wa magonjwa kwa wataalam wa mifugo sehemu za kazi, Prof. Gabriel amesema mradi huo utasaidia kuboresha maabara za mifugo hapa nchini ikiwemo Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) ili kupata chanjo mbalimbali za mifugo.
Kwa upande wake mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Mkoa wa Dodoma Dkt. Moses Ole-Neselle amemwambia Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel, kuwa baadhi ya dawa zinazotumika kutibu mifugo ndiyo zinazotumika kutibu binadamu hali inayosababisha usugu wa vimelea vya magonjwa hivyo shirika hilo linaangalia namna ya utumiaji sahihi wa dawa hizo ili kuondokana na tatizo hilo.
Aidha amefafanua kuwa FAO imepata mradi wa kufanya utafiti wa kupata chanjo ya ugonjwa wa miguu na midomo kwa ng’ombe (FMD) ambapo kwa sasa mradi huo umechukua sampuli kutoka maeneo mbalimbali nchini ili iweze kufanya utafiti na kupata chanjo itakayoweza kutumika hapa nchini pekee.
Kuhusu ugonjwa wa mafua ya ndege Dkt. Ole-Neselle amesema FAO ina mradi pia unaoshughulikia tatizo hilo ili kuhakikisha ugonjwa huo haupo hapa nchini.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel na mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Mkoa wa Dodoma Dkt. Moses Ole-Neselle wamekuwa na mazungumzo hayo katika ofisi za wizara hiyo jijini Dodoma katika kuhakikisha FAO na Tanzania zinazidi kuimarisha ushirikiano kwenye kuboresha sekta ya mifugo nchini.
 Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Eliante Ole Gabriel (kushoto) akizungumza na mwakilishi wa FAO Mkoa wa Dodoma Dkt. Moses Ole-Neselle, katika ofisi za wizara hiyo jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akiagana na mwakilishi wa FAO Mkoa wa Dodoma Dkt. Moses Ole-Neselle, kwa kupungiana mikono ili kujikinga na maambukizi ya virus

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...