Ubalozi wa Tanzania nchini India wakishirikiana na Shirika la Ndege la Tanzania [Air Tanzania] waliandaa Kongamano la Biashara na Uwekezaji lililofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Mumbai ambapo wafanyabiashara wapatao 40 kutoka Tanzania, Maofisa kutoka Kituo Cha Uwekezaji [Tanzania Investment Centre] na “Air Tanzania” walikutanishwa na wafanyabiashara, wawekezaji na wasafirishaji wa bidhaa wa India wapatao 60. 

Pamoja na mambo mengine kongamano hilo lililenga kuwakutanisha wafanyabiashara, wawekezaji  na wasafirishaji wa bidhaa wa Tanzania na India ili kupanua wigo wa biashara kati ya Tanzania na India hususan, ununuzi wa bidhaa zinazozalishwa Tanzania kuja India. Wafanyabiashara wa Tanzania walipata fursa adhimu ya kubadilishana taarifa zinazohusu bidhaa zinazozalishwa kwa wingi Tanzania kwa minajili ya kupata  masoko zaidi ya bidhaa hizo na kuongeza idadi ya mizigo inayosafirishwa na ‘Air Tanzania’ kutoka Dar es Salaam kuja Mumbai.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda alieleza, pamoja na mambo mengine, kuwa Kongamano hilo litasaidia wafanyabiashara wa Tanzania kukutana na wenzao wa India na kuanzisha uhusiano wa kibiashara unaotarajiwa kufungua masoko zaidi ya bidhaa zao nchini baada ya wadau hao kupata maelezo ya kutosha kuhusu bidhaa wanazozalisha nchini na faida zake.

 Kwa ujumla, India ina soko kubwa la bidhaa. Hivyo,matarajio ni kuona  kiwango cha bidhaa kutoka Tanzania zinazouzwa India kinaongezeka zaidi hususan, baada ya kurejeshwa tena kwa ndege za Shirika la Ndege, Tanzania, kati ya Dar es Salaam na Mumbai mwezi Julai 2019.  Balozi Luvanda alitoa rai kwa wafanyabiashara hao kutumia usafiri wa ‘Air Tanzania’ kwa kuwa ni wa uhakika, wa muda mfupi zaidi na pia bei yake ni nafuu. Aidha, Mhe. Luvanda aliwaomba wafanyabiashara hao kuongeza ushirikiano na Tanzania katika utalii, hasa ikizingatiwa kuwa India inatoa watalii zaidi ya milioni 20 kwa mwaka kutembelea nchi mbalimbali duniani. 
Akimwakilisha Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania, Patrick Ndekana alieleza historia ya Shirika hilo na hali ilivyo kwa sasa. Aidha, Bwana Ndekana aliwaeleza washiriki wa Kongamano kuwa Shirika hilo limejipanga kuhakikisha usafiri wa uhakika, bora na salama kwa kuwa  linamiliki ndege mpya na za kisasa.

Vilevile, Bwana Ndekana alifafanua shabaha ya kuitisha Kongamano kuwa ilitokana na wadau mbalimbali kama vile wasafairishaji wa bidhaa kukosa taarifa za fursa za usafirishaji zilizopo kwenye shirika hilo. Hivyo, alieleza matarajio ni kuwa wadau hao wataweza kutumia zaidi usafiri wa Shirika hilo baada ya Kongamano hilo mahsusi. 

Akiwasilisha mada kuhusu biashara na uwekezaji nchini Tanzania, Afisa kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania [TIC], Bwana Nestory Kissima alieleza kuwa Tanzania imefanya mabadiliko makubwa katika sera zake za kuvutia biashara na uwekezaji na amewaomba wafanyabiashara waliohudhuria kongamano hilo kuchangamkia fursa za biashara zilizopo Tanzania hususan, katika ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya asili ya biashara kama vile mkonge, pamba, korosho,madini,matunda mbalimbali kama vile parachichi, na nafaka mbalimbali pamoja na ununuzi wa mazao hayo ambayo yanahitajika sana nchini India. 

Bwana Kissima alieleza kuwa, kwa kiasi kikubwa mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini Tanzania yameboreshwa ikiwa ni pamoja na Serikali kufanyia kazi changamoto mbalimbali zilizokuwepo kwa wawekezaji na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi. Jitihada hizo zinafanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli za kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati kupitia uwekezaji kwenye viwanda na miradi ya kimkakati ifikapo 2025.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...