*RITA ilianzisha kitengo cha kuandika na kuhifadhi Wosia baada ya kuona changamoto ni nyingi katika usimamizi wa mirathi ambazo marehemu hakuacha wosia hivyo mirathi hizo huchukua muda mrefu kumalizika na kuchelewesha haki na usawa kwa warithi halali wa marehemu hasa mwanamke na watoto.
*Mwanamke ni nguzo imara katika familia hivyo nguzo hiyo inapokosa pahali pa kusimamia huanguka kirahisi na hata kuathiri familia kwa kiasi kikubwa. Hatahivyo kumekuwa na changamoto nyingi za kuwepo kwa masuala ya kutokuwa na haki na usawa linapokuja suala la ugawaji wa mali za marehemu katika familia kwani watu wengi wamekuwa na mtazamo hasi katika suala zima la kummilikisha mwanamke mali za marehemu pasipokutambua kuwa yeye ni msimamizi mkubwa wa mali hizo kwa faida ya familia.
*Wosia ni tamko analotoa mtu wakati wa uhai wake akieleza mahali atakapozikwa na jinsi anavyotaka mali yake igawanywe kwa warithi wake mara baada ya kifo chake. Kuna aina mbili za wosia nazo ni wosia wa maandishi na wosia wa matamshi au mdomo. Hatahivyo utaratibu wa kuandika wosia unatofautiana kulingana na sheria ya mirathi inayotumika.
*Jamii imetakiwa kuondoa dhana potofu ya kuwa kuandika wosia ni uchuro kwani suala hilo halina uhalisia wowote bali ni ulinzi wa haki ya familia lakini pia Wosia ni suala la kisheria ambapo utunzaji wake ni moja ya kazi zilizoainishwa kwenye sheria hivyo si uchuro kwasababu kifo hupangwa na Mungu pekee.
Faida za kuandika Wosia ni kama zifuatazo;
-Kuepusha mke au watoto /mume kunyan`gwa mali.
-Inakuwezesha kumchagua msimamizi wa mirathi.
-Kuepusha migongano/migogoro katika familia, ndugu au jamaa.
-Unakupa uhakika wa maisha bora ya baadae ya warithi wako kulingana na mali ulizonazo.
-Kupunguza gharama/usumbufu wakati wa kuendesha mirathi.
*Huduma hii ya kuandika na kuhifadhi wosia inapatikana katika viwanja vya Halmashauri ya mji wa Bariadi. Mbali na hapo huduma hii hutolewa katika Ofisi za Wakala ambayo ina Wanasheria wa Serikali waliobobea katika masuala ya Wosia na Mirathi kwa ujumla ambapo hutunzwa kwa umakini na usiri mkubwa. Gharama za kuandika na kutunza wosia huo ni nafuu kulingana na mali za muhusika.
*Akitoa ushauri kwa jamii Bi.Mandawa alisema kuwa jamii ni lazima ibadilishe mtazamo wake hasi na kumpa kipaumbele mwanamke pale anapoteuliwa kusimamia mali za marehemu hivyo wananchi lazima watambue kuwa ni jambo jema na la busara mtu kuandika wosia ili kuandaa mustakabali wa maisha ya warithi wake angali akiwa hai ili kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima katika familia na jamii kwa ujumla pamoja na kuleta usawa na haki kwa maendeleo ya baadae.
*Asilimia kubwa ya jamii zetu za kiafrika mwanamke amekuwa akinyanyasika sana katika suala zima la usimamizi wa mali halali za marehemu mume wake akichukuliwa kama kiumbe dhaifu kisichokuwa na uwezo wa kusimamia na kulinda mali hizo kwa maendeleo ya baadae ya familia yake jambo ambalo halina ukweli wowote na linapaswa kupingwa vikali ili kukomesha ukatili huo katika jamii kwani mwanamke ana uwezo mkubwa wa kusimamia mali kwa usawa na haki pale tu anapopewa nafasi ya kufanya hivyo. Kama ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inavyosema kuwa "Kizazi cha usawa kwa maendeleo ya Tanzania ya sasa na baadaye".
*RITA inashiriki katika maadhimisho ya siku ya wanawake ambapo kitaifa inafanyika katika viwanja vya Halmashauri ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu . Huduma zitolewazo katika banda la RITA ni kuandika na kuhifadhi wosia pamoja na elimu kwa umma kuhusu Usimamizi wa mirathi, Usajili wa miunganisho ya wadhamini ,Kuasili watoto, Usajili wa ndoa na talaka pamoja na vizazi na vifo. Hivyo wananchi wanakaribishwa kutembelea banda la RITA ili kufaidika na huduma hizo. Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Mhe. Makamu wa Rais Serikali ya awamu ya tano, Bi. Samia Suluhu.
Imetolewa na;
Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini – RITA
Mwanasheria wa Serikali Mwandamizi
Janeth Mandawa
06/03/2020.
(Simiyu)
Afisa Usajili Msaidizi, Leocadia Temu akionesha fomu ya kuandika wosia kwa Katibu Tawala mkoa wa Simiyu, Ndg. Jumanne Sagini alipotembelea banda la RITA.
Afisa Usajili Msaidizi, Leocadia Temu akitoa maelezo ya kina kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuandika wosia.
Waziri wa afya maendeleo ya jamii, jinsia, watoto na wazee, Ummy Mwalimu akikabidhi cheti Shukrani ya kushiriki msafara wa kupinga ukatili wa kijinsia "Twende Pamoja" kwa Afisa Usajili Msaidizi, Janeth Mandawa kutoka RITA katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Halmashauri ya mji wa Bariadi, Simiyu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...