Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Ushiriki Tanzania na Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) Rose Reuben akizungumza kuhusiana na maadhinisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Taasisi mbalimbali za usawa kuangazia uchaguzi Mkuu.
Afisa Kituo cha Haki za Binadamu Getrude dyabene akitoa maelezo kuhusiana na haki Binadamu kuzinagatiwa wakati uchaguzi mkuu.
Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Bob Wangwe akitoa maelezo kuhusiana siku ya Wanawake Duniani.
Na Chalila Kibuda,Globu ya Jamii.
MTANDAO wa Ushiriki Tanzania (UT) umeziomba taasisi za serikali zinazohusika na masuala ya uchaguzi, kuwashirikisha makundi maalum wakiwamo wanawake, vijana na wenye ulemavu kujadili kwa pamoja mchakato shirikishi wa uchaguzi utaofanyika mwaka huu.
Hayo yamesemwa na viongozi wa Ushiriki Tanzania (UT) ambao unajumuisha Asasi 23 zinazogusa masuala ya kisiasa, sheria, haki za wanawake, wenye ulemavu na vijana kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo Kilele chake Machi 8.
Akizungumzia na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Makamu Mwenyekiti wa UT ambaye ni Mkurugenzi wa Chama cha Wanawake Tanzania (TAMWA), Rose Reuben amesema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na taasisi nyingine za serikali zinapaswa kuketi pamoja na kuyashirikisha makundi hayo maalumu kuanzia ngazi za awali.
Reuben amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu, yanaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 25 baada ya mkutano wa Beijing hivyo wanapaswa kujikumbusha mafanikio yaliyofikiwa katika harakati za kumkomboa mwanamke ikiwamo ushiriki wake kisiasa na katika meza za maamuzi.
Amesema ripoti ya Taasisi ya Uongozi ya mwaka 2015 inaonyesha kuwa, kwa mara ya kwanza, tangu tupate uhuru, Tanzania imepata Makamu wa Rais, wa kwanza mwanamke, Samia Hassan Suluhu.
Pia alisema idadi ya wabunge wanawake walioshinda viti ilikuwa 238 kati ya wagombea wote 1250. Wakati huo, mwaka 2010, bunge la Tanzania lilikuwa na wanawake wabunge 125 kati ya wabunge wote 339.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa, licha ya mafanikio bado Tanzania na nchi nyingine nyingi duniani hazijafikia ushiriki wa 50 kwa 50 katika nyanja za siasa ambapo harakati bado zinaendelea.
Amesema hivyo UT inahamasisha ushiriki wa wanawake katika kugombea, kupiga kura katika ngazi za juu za maamuzi.
Naye Mwenyekiti wa UT, Israel Ilunde amesema, kuwa wamekuwa wakishughulikia masuala 9 muhimu katika kuhakikisha Wanawake ,Vijana na watu wenye ulemavu wanashiriki na kushirikishwa kikamilifu katika masuala ya umma likiwemo la Uchaguzi na ushiriki wa wanawake kisiasa.
Ilunde alitaja baadhi ya masuala hayo ni pamoja na kuwa na bajeti bora kwa ajili ya elimu ya mpiga kura inayoweza kuwafikia makundi hayo.
Amesema kuna maboresho ya shughuli za vyombo vya ulinzi wakati wa uchaguzi kuwa jicho la haki za binadamu.
“ vituo vya kupigia vinatakiwa kuboreshwa ili watu wenye ulemavu waweze kushiriki vema wakati wa zoezi la upigaji kura .
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...