*Unajumuisha viongozi wa dini,
Serikali, wanasiasa na wadau wa afya
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
Serikali inatambua nguvu kubwa waliyonayo viongozi wa dini katika jamii na itaendelea
kutoa ushirikiano wa dhati katika kuyatekeleza na hatimaye kufikia malengo
yanayotarajiwa katika mwitikio wa UKIMWI Tanzania.
“Serikali inaunga mkono tamko na
maazimio mliyoyafikia leo hii na itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati katika
kuyatekeleza na kufikia malengo yanayotarajiwa katika mwitikio wa UKIMWI
Tanzania. Sote tunatambua nafasi na nguvu mlizonazo viongozi wetu wa dini
katika jamii,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Machi 10,
2020) kwenye ukumbi wa Msekwa, Bungeni jijini Dodoma wakati akizungumza na
viongozi wa dini, wabunge, na wadau mbalimbali wa mashirika ya WAVIU kwenye
uzinduzi wa kampeni ya kushirikisha viongozi wa dini kutokomeza unyanyapaa ili
kufikia malengo ya kitaifa ya mwitikio wa UKIMWI nchini.
Kampeni hiyo inayoitwa “Hebu Tuyajenge, Tufikie 95-95-95: Tanzania
bila Unyanyapaa Inawezekana, Viongozi wa Dini Tuongozee njia” inalenga kuhamasisha
umma wa Watanzania waungane kutokomeza unyanyapaa dhidi ya VVU na UKIMWI
Tanzania.
Akizungumza na
viongozi hao, Waziri Mkuu amesema ana imani kubwa watalisimamia vizuri suala la
unyanyapaa na ukatili wa kijinsia kwa kuwa jamii inawasikiliza, inawaheshimu na
kuwaamini sana wao kuliko inavyowasikiliza wanasiasa au hata wanavyosikiliza na
kuamini vyombo vya habari.
“Tambueni kwamba mnayo kazi
kubwa ya kufanya katika kuhakikisha unyanyapaa na ukatili wa kijinsia unakwisha
kabisa katika jamii yetu. Niendelee kuwaomba viongozi wetu wa dini kupitia
ibada katika madhehebu yenu, vyombo vyenu vya habari, jumuiya, makongamano
mbalimbali, taasisi zenu za elimu na afya, tuhakikishe tunatoa ujumbe wa kutia
hamasa, elimu na upendo ili hatimaye wanaume, vijana na watoto wengi wazifikie
huduma za VVU sambamba na kutambua haki na usalama wa mtoto.”
Amesema Serikali
inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli,
itaendelea kutekeleza na kuboresha huduma za za afya ikiwa ni pamoja upimaji wa
Virusi Vya UKIMWI, matibabu ya magonjwa nyemelezi pamoja na kupiga vita unyanyapaa
wa aina zote kwa WAVIU.
Amesema
Tanzania inaungana na nchi nyingine duniani zinazoamini katika kutokomeza unyanyapaa
na ubaguzi wa aina zote lengo likiwa ni kutokomeza ubaguzi uwe wa kiitikadi au
kijamii. “Kwa pamoja tuungane kukemea vitendo vya unyanyapaa na ubaguzi kutokana
na madhara makubwa kwa watu wetu na Taifa kwa ujumla wake.”
Amesema
licha ya dini zote kukemea ubaguzi na unyanyapaa, bado unyanyapaa, ukatili wa
kijinsia hasa kwa watoto vimeshamiri katika jamii. “Watu wanaoishi na Virusi vya
UKIMWI (WAVIU), hukumbwa na kadhia ya unyanyapaa katika jamii zetu. Kadhalika,
watoto wa umri mdogo nao wanatendewa ukatili mkubwa sana kama vile kunajisiwa
na kutelekezwa,” amesema.
“Vitendo
vya namna hii hudhoofisha jitihada za kutokomeza maambukizi ya VVU kwani
huwafanya watu kuogopa kujitokeza kupima VVU. Mtu huhofia kwamba ikijulikana
ana maambukizi atabaguliwa na hivyo, kuishi maisha ya mateso yatokanayo na
msongo wa mawazo na aibu ya kunyanyapaliwa.”
Katika
kongamano hilo la siku moja, Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki
Mbeya na Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC); Askofu Mark Walwa Malekana
wa Kanisa la Waadventista wa Sabato (SDA); Askofu Alinikisa Cheyo wa Kanisa la
Morovian na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo (CCT); Askofu Peter Konki wa Umoja
wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) na Mufti wa Tanzania, Sheikh
Abubakar Zuberi (BAKWATA) walitoa ahadi zao za kuunga mkono kampeni hiyo
kupinga unyanyapaa kwa kutumia ibada na taasisi zilizo chini yao na kisha kutia
saini Tamko Rasmi la Viongozi wa Juu wa Taasisi za Dini kuhusu ushiriki wao
katika mwitikio wa UKIMWI nchini.
Mapema, kongamano hilo lilipokea shuhuda kutoka kwa Mchungaji
Prof. Gideon Byamugisha (61) wa kutoka Uganda, Mbunge kutoka Zambia wa chama
cha United Party for National Development (UPND), Bi. Princess Kasune (45) na
Bi. Pundensiana Mbwiliza (25), mfanyabishara ya mikoba ya vitenge kutoka
Mwanza, Tanzania ambao wameishi na VVU kwa kati ya miaka 10 - 25 na wamekuwa
mstari wa mbele kuvunja ukimya kuhusu hali zao na kupiga vita unyanyapaa.
Naye Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muunguno wa Tanzania,
Mhe. Job Ndugai alisema uamuzi wa
kujuisha viongozi wa dini kwenye masuala ya kitaifa ulianza mwaka jana jijini Mwanza
ambako waliowaomba viongozi wa dini wawasidie kuihamasisha jamii kuhusu tatizo
la ugonjwa wa kifua kikuu.
“Tuliona kuwa
kuweka msisitizo kwenye Kifua Kikuu peke yake haitoshi; tukaona ni vema tushirikiane
nao tena ili watusaidie kusukuma uelewa miongoni mwa jamii kuhusiana na suala hili
la VVU,” alisema.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wa dini wakati
alipowasili kwenye ukumbi wa Msekwa jijini Dodoma, Machi 10, 2020 kuzindua Kampeni ya Kitaifa ya Viongozi wa Dini na Bunge katika kuongeza jitihada za kupunguza unyanyapaa dhidi ya Ukimwi.
Kushoto ni Spika wa Bunge, Job Ndugai, wa tatu kushoto ni Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,
Jenista Mhagama,Watano kushoto ni Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai na
wa sita kushoto ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Kampeni ya
Kitaifa ya Viongozi wa Dini na Bunge katika kuongeza jitihada za
kupunguza unyanyapaa dhidi ya Ukimwi kwenye ukumbi wa Msekwa jijini
Dodoma, Machi 10, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...