Charles James, Globu ya Jamii
KATIKA kuchukua tahadhari ya maambukizi ya ugonjwa wa Corona kwenye maeneo mbalimbali, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imehairisha sherehe za ufunguzi wa mashindano ya kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu zilizokua zifanyike leo jijini Dodoma.
Akizungumza leo katika uwanja wa Jamhuri ambapo mashindano hayo yanafanyika, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof James Mdoe kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Prof Joyce Ndalichako ametangaza kusitisha shughuli hizo.
Prof Mdoe amesema wizara imechukua hatua hiyo ikiwa ni kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa huo kwa kuepuka mkusanyiko mkubwa kama ambavyo Wizara ya Afya kupitia Waziri wake Ummy Mwalimu ilitoa tahadhari kwa wananchi, taasisi na mashirika kuchukua hatua dhidi ya ugonjwa huo.
" Kwa niaba ya Waziri wa Elimu Prof Ndalichako nitangaze kusititisha uzinduzi huu lakini shughuli za maonesho na mashindano zitaendelea kama tulivyokua tumepanga awali.
Tunachokwepa ni huu mkusanyiko wa pamoja wa na watu wengi wakati wa uzinduzi, hivyo niwaombe tuendelee na mashindano yetu kama kawaida na majaji watakua wakipita kuandika maksi zao na mwisho mshindi lazima apatikane na tumjue," Amesema Prof Mdoe.
Kwa upande wake Dk George Dilunga ambaye ni Mtaalamu wa magonjwa ya dharura kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa amewataka wananchi kuendelea kuchukua hatua ikiwemo kunawa mikono kwa maji na sabuni pamoja na kuwahi kituo cha afya pindi wanapoona dalili kama za ugonjwa wa Corona.
Mashindano ya MAKISATU yanafanyika kwa siku tano katika jiji la Dodoma ambapo makundi saba yatashindana na kumpata mshindi ambaye atajinyakulia kitita cha Sh Milioni Tano.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bunge wakiongozwa na Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia wakipata maelezo mafupi kwenye banda la Benki ya CRDB walipokua wakitembelea mabanda leo kwenye maonesho na mashindano ya MAKISATU.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof James Mdoe akitangaza kusitisha sherehe za ufunguzi wa mashindano ya kitaifa ya Sayansi, teknolojia na ubunifu ikiwa ni kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa wa Corona. Mashindano hayo yameanza leo jijini Dodoma.
Dk George Dilunga ambaye ni Mtaalamu wa magonjwa ya dharura kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo jijini Dodoma akitoa elimu ya namna ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Corona katika viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma leo kwenye mashindano ya kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...