Na Ripota wetu,
Kasulu.
Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu imetenga eneo la uwekezaji lenye ukubwa wa
hekta 35,000 kwa ajili ya kilimo cha miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari.
Eneo hilo kwa sasa amepewa mwekezaji wa kampuni ya Kigoma Sugar Co. Ltd
chini ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambacho kina mamlaka ya kusimamia
Uwekezaji nchini.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Simon Anange (aliyevaa
Fulana rangi ya damu ya Mzee)akifafanua jambo katika kikao cha pamoja na
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Geoffrey Mwambe
(aliyevaa shati la bluu) na ujumbe wake kutoka katika kituo hicho walipowasili
Mkoani Kigoma kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya Uwekezaji Mkoani humo.
Mwekezaji wa Kampuni ya Kigoma Sukari anatarajia kuendesha shamba hilo kwa
kulima miwa na kujenga kiwanda cha sukari mapema mwaka huu kitakachokuwa na
uwezo wa kuzalisha tani 110,000 za Sukari kwa mwaka, hatua itakayosaidia
kupunguza pengo la upatikanaji wa bidhaa hiyo nchini linalokadiriwa kufikia
tani 320,000 kwa mwaka.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)
Bw. Geoffrey Mwambe (Mwenye shati rangi ya bluu) na Mkuu wa Wilaya ya
Kasulu Kanali Simon Anange (mwenye fulana rangi ya damu ya mzee) wakisisitiza
jambo wakati wakiangalia ramani ya eneo lililotengwa na wanavijiji wa
vijiji saba vya Wilaya ya Kasulu kwa ajili ya uwekezaji, wengine ni maafisa wa
Kituo cha Uwekezaji Tanzania na Katibu Tawala wa Mkoa huo.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Simon Anange alisema eneo hilo limetolewa
na Wanavijiji wa Vijini saba vya Nyamidaho, Kumtundu, Nyarugusu, Heru
ushingo, Kigadye, Kitanga na Kiyugwe vyote vikipatikana kwenye Kata tatu za
Nyamidaho, Kitanga na Heru ushingo, vikiunganisha shamba hilo kuwa moja
Wilayani Kasulu Mkoa wa Kigoma.
Mkuu huyo wa Wilaya alikuwa akitoa taarifa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo
cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Geoffrey Mwambe, aliyefanya ziara ya kikazi
mkoani Kigoma kwa ajili ya kukagua Maendeleo ya Uwekezaji mkoani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma Kanali Simon
Anange akisisitiza jambo kwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania Bw.
Geoffrey Mwambe (hayupo pichani) aliewasili Wilayani humo kwa ajili ya
kuangalia maendeleo ya Uwekezaji.
"Baadhi ya Vijiji kwa hiyari yao wameamua kutoa maeneo ya Uwekezaji,
hii ni hatua muhimu na ya kupongezwa sana, shamba hili lenye ukubwa wa hekta
zaidi ya a elf 35 linapitiwa na miundombinu yote muhimu kwa Uwekezaji ikiwepo
barabara, reli itakayounganisha nchi za Tanzania na Burundi, umeme wa gridi ya
Taifa kutoka Nyakanazi hadi Kidahwe Mkoani Kigoma unaotarajiwa kujengwa ifikapo
mwakani, pamoja na mto Malagalasi utakaotumika kumwagilia mashamba ya
miwa"alisema Kanali Anange.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Simon Anange (aliyevaa
Fulana rangi ya damu ya Mzee)akimwonyesha Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha
Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Geoffrey Mwambe (aliyevaa shati la bluu) eneo la
shamba la Uwekezaji ilayani humo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)
Bw. Geoffrey Mwambe alisema hatua iliyofikiwa na wanavijiji hao ni ya
kupongezwa na kwamba (TIC) inaunga mkono juhudi hizo.
"Sisi Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) tunaunga mkono juhudi za
wanavijiji hawa na tunawapongeza sana,nawahakikishia tutalisimamia eneo hili na
Uwekezaji utakaofanywa hapa utakuwa wa manufaa kwa wananchi kwa kuwa nia ya
Serikali ni kuifanya Kasulu kuwa kitovu cha uzalishaji wa sukari kwa Mkoa wa
Kigoma"alisema Bw. Mwambe.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)
Bw. Geoffrey Mwambe akiangalia mto Malagalasi unaopita kwenye shamba la uwekezaji
Wilayani humo, mto huo utatumika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji wa miwa
kwa ajili ya uzalishaji wa Sukari.
Kiwanda cha sukari Kigoma kitakachojengwa
kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 110,000 za sukari ambazo zikiingia sokoni
zitapunguza pengo la upatikanaji wa Sukari nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...