Na Karama Kenyunko- Michuzi Tv.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeuamuru upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi haraka wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili, Ofisa Elimu kwa Umma wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti (26) na mwenzake, ili shauri hilo liweze kuendelea katika hatua nyingine.

Katika kesi hiyo, Magoti, anashtakiwa pamoja na mtaalamu wa masuala ya Tehama, Theodory Gyan (36), ambapo wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka ya kutakatisha fedha ambazo ni Sh.  milioni 17, 354,535 na wako rumande kwa sababu mashitaka yanayowakabili hayana dhamana kisheria.

Mapema leo Aprili 15,2020 wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai  mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Janeth Mtega kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na ameongeza kuwa alifanya mawasiliano na wapelelezi kama mahakama ilivyoelekeza kukamilisha upelelezi na kwamba wameahidi kukamilisha upelelezi kwa sababu maeneo yanayopelelezwa ni mengi.

Baada ya taarifa hiyo, Wakili wa Utetezi, Jeremiah Ntobesya amedai upelelezi wa kesi hiyo umechukua muda mrefu na makosa yenyewe ni kama yalishafanyiwa upelelezi kabla ya kushitakiwa....,"Mheshimiwa naomba upande wa mashtaka wakamilishe upelelezi mapema ili ianze kusikilizwa na washitakiwa wapate haki ya kusikilizwa kisha mahakama itoe maamuzi kutokana na ushahidi kwani kama upande wa mashitaka utakamilisha upelelezi haraka ndivyo mahakama itatoa maamuzi haraka", amedai Ntobesya.

Akijibu hoja hiyo,  wakili Simon alidai watafanyia kazi maombi ya upande wa mashtaka na tarehe itakayofuata watakuja na majibu.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Mtega aliuamuru upande wa mashitaka kukamilisha upelelezi haraka ili shauri liendelee katika hatua nyingine kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 29, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Washitakiwa hao wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Februari Mosi, 2019 na Desemba 17, 2019 ndani ya jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine ya Tanzania kwa pamoja na watu ambao hawapo mahakamani kwa makusudi walishiriki makosa ya kiuhalifu ya kumiliki programu ya Kompyuta iliyotengenezwa mahususi kufanya kosa la jinai na kuwawezesha kujipatia kiasi cha Sh 17,354,535.

Katika  shtaka la pili, inadaiwa  katika tarehe tofauti kati ya Februari Mosi, 2019 na Desemba 17, 2019 ndani ya jiji na Mkoa wa Dar es Salaam kwa pamoja washitakiwa hao na mengine ambao hawapo mahakamani walimiliki programu ya kompyuta iliyotengenezwa mahususi kwa ajili ya kutenda makosa ya jinai.

Pia inadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi, 2019 na Desemba 17, mwaka huu, ndani ya jiji la Dar es Salaam washtakiwa hao kwa pamoja walijipatia jumla ya Sh 17,353,535 wakati wakijua mapato hayo yametokana na mazalia ya kosa la kushiriki genge la uhalifu.

Washtakiwa hao hawakuruhusiwa kujibu chochote kwakuwa mahakama hiyo aina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi mpaka ipate kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mshitaka nchini (DPP).


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...