Na MZEE WA ATIKALI  ✍️✍️✍️


1. Usuli:

Rais wa kwanza wa Tanganyika na Tanzania, marehemu Mwalimu JK NYERERE na Rais wa kwanza wa Kenya, marehemu Mzee JOMO KENYATTA, walikuwa na kawaida ya kuhudhuria kabumbu viwanjani, mara moja moja, kunapokuwa na mchezo wa Kimataifa.

Hata hivyo, Mwalimu NYERERE aliacha kwenda uwanjani siku ya Jumanne, tarehe 4.7.1972 na Mzee KENYATTA aliacha kwenda uwanjani siku ya Jumapili, tarehe 12.12.1965.

Je, nini kilipelekea Marais hawa kukata mguu kwenda viwanjani kushuhudia mitanange?.


2. RAIS JK NYERERE

2.1 TAIFA STARS Yakipiga na Timu ya Taifa ya Sudan

Mwaka 1972, katika kunogesha shamrashamra za kusheherekea sikukuu ya Sabasaba, chama cha soka nchini, FAT, kiliialika timu ya Taifa ya Sudan kupambana na timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Jumanne ya tarehe 4.7.1972 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dsm.

2.1.1 TAIFA STARS Yapiga Kambi Kurasini

Katika kujiandaa na mtanange huo, Taifa Stars iliweka kambi hoteli ya Jeshi la Wokovu, Kurasini, ikinolewa na kocha Mkorea, PAK YUNG TANG.

2.1.2 Rais NIMEIRY Awa Mgeni Rasmi

Mgeni rasmi kwenye mtanange huo alikuwa ni aliyekuwa Rais wa Sudan kuanzia mwaka 1969 hadi 1985, marehemu JAFFAR MOHAMAD AL-NIMEIRY, aliyefariki tarehe 30.5.2009. Rais wa Tanzania, Mwalimu JK NYERERE, pia alihudhuria.

2.1.3 TAIFA STARS Yaingia Uwanjani kwa miguu!

Siku ya mechi ilipofika, maelfu ya manazi wa kabumbu jijini, walijanaza vilivyo uwanja wa Taifa.

Wachezaji wa Taifa Stars  waliingia uwanjani kwa miguu wakiwa wamevaa kiraia kwa kupitia upande wa Kusini wa uwanja wa Taifa! Mashabiki wengi walipigwa butwaa kwani walizoea kuwaona wachezaji hao wakiingia kwa basi kupitia mlango mkubwa.

2.1.4 TAIFA STARS Yaingia Dimbani Bila Jezi:

Kituko cha Karne kilitokea timu hizo zilipokuwa zikiingia uwanjani. Wachezaji wa Taifa Stars waliingia bila jezi rasmi, wakiwa wamevaa bukta tu huku vifua vikiwa wazi!.

Wapenzi wengi wa soka walihisi kuwa hayo huenda yalikuwa ni masharti ya mganga!.

2.1.5 Rais NIMEIRY Aikagua TAIFA STARS Ikiwa vifua wazi

Mgeni wa heshma, Rais NIMEIRY, akatimiza wajibu wake wa kuzikagua timu hizo ambapo alianza na Taifa Stars waliokuwa vifua wazi.

ABRAHAMAN JUMA, kapteni wa YANGA, waliokuwa Mabingwa nchini mwaka huo, ambaye pia ndiye  alikuwa kapteni wa Taifa Stars, alimtambulisha Rais NIMEIRY kwa wachezaji wa Taifa Stars.

2.1.6 Picha ya Kihistoria ya TAIFA STARS

Picha iliyopigwa siku hiyo wakati wa ukaguzi wa wachezaji hao, ni picha ya kipekee na ya kihistoria. Picha hiyo inamuonesha ABRAHAMAN JUMA akimtambulisha Rais NIMEIRY kwa beki hodari wa YANGA wakati huo na Taifa Stars, marehemu HASSAN "WA MOROCCO" GOBBOS ambaye anaonekana akimpa mkono Rais NIMEIRY. Kushoto kwa GOBBOS ni KITWANA MANARA "POPAT", Na. 9 wa YANGA na Taifa Stars, aliyeweka rekodi ya kuichezea Taifa Stars kwa miaka mingi (16) kuliko wachezaji wote katika historia ya Kabumbu nchini (1960-1976). Kulia kwa GOBBOS ni beki kisiki cha mpingo, MOHAMED CHUMA "Chinga-Boy" kutoka Mtwara, ambaye anaaminika ndiye beki bora kabisa Na.3 kuwahi kutokea nchini na aliyeweka historia ya kuagwa kwa heshma kuliko wachezaji wote wa Taifa Stars alipotundika viatu mwaka 1975!. Anaeyeonekana kwa mbali ni ABDALLAH KIBADEN KING, mshambuliaji mahiri wa Mnyama SIMBA@ WEKUNDU WA MSIMBAZI na Taifa Stars.

2.1.7 TAIFA STARS Yaupiga Mpira Mwingi

Licha ya kucheza wakiwa  vifua wazi, wachezaji wa Taifa Stars walionesha Uzalendo wa hali ya juu kwa kulipigania Taifa lao ambapo walionesha kandanda la hali ya juu sana.

2.1.8 TAIFA STARS Yashinda 3-1

Taifa Stars iliicharaza timu ya Taifa ya Sudan kwa mabao 3-1.

2.1.8.1 SEMBULI Atupia Kambani Mabao 2

GIBSON SEMBULI, Mshambuliaji mahiri Na.9 wa YANGA na TAIFA STARS, alifunga magoli mawili ya kwanza.

Tanzania haijawahi kuwa na mchezaji mwenye mashuti kama SEMBULI hadi leo. SEMBULI, aliyekuwa na mwili wa mpira, alikuwa ni mtu wa miraba minne mwenye misuli iliyojaa vyema kimichezo.

Makipa wengi Afrika  Mashariki walikuwa wakimuogopa na kukwepa mashuti yake baada ya kumvunja mkono kipa "MACHAPATI" aliyejaribu kurukia "mashine" iliyo urumishwa na SEMBULI na kukimbizwa hospitali alikowekewa POP!.

SEMBULI, alifunga goli la kwanza katika dakika ya 65 kirahisi baada ya ngome ya Timu ya Taifa ya Sudan kujichanganya. Goli la pili, ambalo lilishangiliwa mno na uwanja mzima, lilifungwa na SEMBULI katika dakika ya 68. SEMBULI, akiwa katikati ya uwanja, aliachia gruneti lililokwenda kupiga besela na kumwacha nyanda wa Sudan adakie kwa macho!. Kwa hakika, hilo ni moja ya mabao bora kabisa kuwahi kufungwa kwenye Shamba la Bibi!.

Bao la 3 liliwekwa kimiani dakika ya 79 na ABDALLAH KIBADEN "KING" "MPUTA", Mshambuliaji mahiri kabisa wa SIMBA na Taifa Stars ambaye ni mmoja wa washambuliaji  bora kabisa kuwahi kutokea nchini. Hadi mwisho wa mchezo Taifa Stars 3, Sudan 1.

2.1.9  "YALE MAMBO YETU" Ndiyo Yalipelekea TAIFA STARS Kucheza Vifua Wazi!

Je, ni kwanini Taifa Stars ilicheza vifua wazi siku hiyo?.

Bongolanders wengi, kwa miaka mingi, wamekuwa kila mmoja akielezea tukio hilo ajuavyo yeye. Lakini, ukweli wa 100% wa kuhusu nini kilichosababisha Kaduna hiyo, ulibainishwa na aliyekuwa Meneja wa Uwanja wa Taifa mwaka 1972, Mh. CHABANGA HASSAN DYAMWALE ambaye, bila kupepesa macho, kutikisa pua wala
kuchezesha maskio, tarehe 10.10.2006 aliweka mambo hadharani. Mh. DYAMWALE alitiririka kama ifuatavyo:

"Jezi za Taifa Stars zilikuwa zimepelekwa kwa MGANGA ili Taifa Stars ishinde mechi hiyo. Siku ya mechi, yaani tarehe 4.7.1972, Meneja wa Taifa Stars alimfuata mganga huyo lakini kwa bahati mbaya hakumkuta. Kwakuwa Meneja huyo alikuwa amekwenda kwa Mganga huyo na basi la timu, ikabidi wachezaji wa Taifa Stars watembee kwa miguu toka kambini hotel ya Jeshi la Wokovu, Kurasini hadi uwanja wa Taifa. Ndiyo maana timu yetu ya Taifa ilicheza vifua wazi siku hiyo na kuwa aibu kubwa kwa Taifa".

2.1.10 Mwalimu Aagiza Kupatiwa Maelezo ya Fedheha hiyo

Mara tu baada ya mchezo, Mwalimu aliyekuwa amefadhaika sana, licha ya ushindi mnono wa mabao 3-1, aliagiza kupatiwa mara moja sababu iliyopelekea aibu hiyo.

Toka siku hiyo, Mwalimu hakukanyaga tena uwanjani kwenda kushuhudia Kabumbu hadi anafariki dunia tarehe 14.10.1999 huko Uingereza!.



3. RAIS JOMO KENYATTA

3.1 Harambee Stars Yakipiga na Black Stars

Siku ya jumapili ya tarehe 12.12.1965, ilikuwa ni siku ya kusheherekea uhuru wa Kenya uliopatika tarehe 12.12.1963. Chama cha soka nchini humo kikaialika Timu ya Taifa ya Ghana (Black Stars) iliyokuwa Mabingwa wa Afrika wakati huo.

Mtanange huo ukapigwa Jamhuri Park stadium, kuanzia saa 10 jioni.

3.1.1 Wakenya Wafurika Uwanjani

Siku hiyo, maelfu ya Wakenya walitia timu uwanjani hapo toka asubuhi ingawa mechi ilikuwa inapigwa kuanzia saa 10 jioni. Kufika muda huo wa mechi, uwanja ulikuwa umejaa hadi pomoni!.

3.1.2 Rais KENYATA mgeni rasmi

Rais KENYATTA ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika mechi hiyo iliyohudhuriwa pia na Baraza lote la Mawaziri liloketi jukwaa kuu pamoja na Rais KENYATTA.

3.1.3 Mchezaji Mfungwa Atolewa Gerezani Achezee Harambee Stars

Kenya ilijitayarisha vilivyo kwa mtanange huo wa kukata na shoka. Mh. Rais KENYATTA akatoa amri mshambuliaji mahiri wa Harambee Stars, NICODEMUS ARUDHI, aliyekuwa akitumikia kifungo kwa unyang'anyi, aruhusiwe kutoka Lupango ya Kamiti ili aje kulitetea Taifa lake.

ARUDHI akaletwa Uwanjani akiwa na pingu kisha akaungana na wenzake. ARUDHI alikuwa bandido ambaye alikuia kuuawa kwa kupigwa shaba na polisi mwaka 1983 alipokutwa na silaha na kutaka kukimbia.

3.1.4 Harambee Stars Yaanza Kwa Mkwara mzito

Katika dakika ya 3 tu ya mchezo, bandido ARUDHI akafanya yake na kuipatia Harambee Stars bao la kuongoza. Uwanja mzima ulilipuka kwa shangwe na nderemo huku Rais KENYATTA akipagawa na kunyanyua fimbo yake nyeusi juu kwa madoido na furaha!.

3.1.5 Harambee Stars Yautafuta Mpira kwa Tochi

Baada ya bao hilo, "Black Stars" walionesha ni kwanini wao walikuwa Mabingwa wa Afrika wakati huo.

"Black Stars" waliupiga mpira mwingi mno ambapo walikuwa wakipasiana huku wachezaji wa Harambee Stars wakipoteana kabisa uwanjani na mvua ya magoli ikaanza kumiminika.

KOFI PARE, mshambuliaji mahiri wa "Black Stars", aliichachafya vilivyo ngoma ya Harambee Stars ambayo ilishindwa kabisa kumkaba. PARE akatupia kambani bao 4. Mshambuliaji mwingine wa timu hiyo, OSEI KOFI nae akatupia za kwake 4. Hadi kufikia mapumziko, scoreboard ilisomeka "8-1"!.

3.1.6 Rais KENYATTA Ataka Mkimbiaji KEINO Awasaidie Harambee Stars!

Ilipofika mapumziko na kuona maji yamekorogeka, Rais KENYATTA aligeuka nyuma na kuliuliza Baraza lake la Mawaziri kwanini Mwanariadha nguli KIPCHOGE KEINO asiitwe kuisaidia Harambee Stars kuwakimbiza Black  Stars,  ambapo alisema: "Waaaaaapi Kipchoge Keino akimbie na hii mutu ya Ghana?"

Waziri wa Michezo akamjibu kuwa yule ni mwanariadha sio mwanasoka, hivyo hilo halitawezekana. Rais KENYATTA akan'gaka-: "Tatizo ni nini? Keino si ni Mukenya, na Harambee stars si ni ya Kenya? Iko mbaya gani kucheza ili kutetea Taifa lake?".

3.1.7 Rais KENYATTA Aingia Mitini

Baada ya kuona kiwango duni cha Harambee Stars na baada ya kuelimishwa kuwa mwanariadha KEINO hataweza kucheza, Rais KENYATTA aliyefura kwa hasira, akaondoka uwanjani bila hata kuliaga Baraza la Mawaziri!.

3.1.8 Harambee Stars Yakianza Kipindi cha 2 kwa Mkwara

Kama ilivyokuwa kipindi cha 1, Harambee Stars ilikianza kipindi cha 2 kwa mkwara mzito na bandido ARUDHI, katika dakika ya 48, akatupia kambani bao la 2.

3.1.9 "Black Stars" Yaimiminia mvua ya magoli Harambee Stars

"Black Stars" iliongeza magoli mengine 5 ambapo PARE alifunga 2. Hadi mwisho wa mchezo "Black Stars" ikawa imeitandika Harambee Stars mabao 13-2.

3.1.10 Mechi Hiyo Iliweka Rekodi Zinazodumu Hadi Leo

3.1.10.1 Timu ya Taifa ya "Black Stars" haijawahi kupata ushindi mwingine mnono kama huo;

3.1.10.2 Timu ya Taifa ya Kenya haijawahi kufungwa tena magoli mengi kama hayo;

3.1.10.3 KOFI PARE aliweka rekodi ya kucheka na nyavu mara 6 katika mchezo mmoja wa "Black Stars", rekodi kuntu ambayo haijavunjwa hadi leo.

4. Rais KENYATTA Aahidi Kutokanyaga Tena Uwanjani

Kesho yake, Rais KENYATTA aliahidi kutokanyaga tena uwanjani kushuhudia kabumbu kutokana na Harambee Stars kumuaibisha yeye na Taifa kwa jumla, tena kwenye siku ya kusheherekea uhuru!.

Rais KENYATTA hakuwahi kukanyaga tena uwanjani kushuhudia soka hadi alipofariki akiwa usingizini, tarehe 22.8.1978.

5. MWISHO

Haya ndio matukio ya kufedhehesha yaliyowafanya Marais hawa wawili kutokanyaga tena viwanjani kushuhudia mitanange ya kabumbu.

Na MZEE WA ATIKALI  ✍️✍️✍️

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...