Na. Edward Kondela
Wizara
ya Mifugo na Uvuvi imewapa vifaranga vya kuku 540 kikundi cha vijana
wajasiriamali ili kuhamasisha ufugaji utakaosaidia kuziba pengo la uhaba wa
nyama ifikapo mwaka 2022 pamoja na kukuza sekta ya kuku nchini.
Kaimu
Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo na Usalama wa Chakula na Lishe wa wizara
hiyo, Bw. Gabriel Bura amekabidhi vifaranga hivyo mwishoni mwa wiki kwa
wawakilishi wa kikundi cha vijana watatu wajasiriamali hafla ilifanyika Mbweni
jijini Dar es Salaam.
Bw.
Bura amesema hatua hiyo inatokana na mkutano uliofanyika kati ya Katibu Mkuu
Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel na wadau wa
tasnia ya kuku kilichoketi Machi 7 mwaka huu katika ofisi ndogo za wizara hiyo
zilizopo jijini Dar es Salaaam
Kwa
mujibu wa Bw. Bura, Prof. Gabriel alimsikiliza mdau mmoja mmoja, lakini
alishawishika zaidi na uwepo wa vijana wenye umri wa chini ya miaka 35
walioonyesha nia ya dhati ya kuwekeza katika tasnia ya ufugaji wa kuku.
Mbali
na hilo, Bw. Bura amesema hatua hiyo pia ni sehemu ya kutekeleza mpango
mkakati wa wizara hiyo ya kuhamasisha ufugaji wa kuku kwa vikundi vya vijana na
kina mama.
Aidha
amesema vijana hao wameonyesha uthubutu na wameonekana kupenda tasnia hiyo ili
kukabiliana na hali halisi ya soko la ajira akisema baadhi yao wamesomea fani
ya sheria na habari na mawasiliano.
Amefafanua
kuwa mpango wa kuwahamasisha ufugaji wa kuku katibu mkuu aliamua kuanza na
vijana watatu ambao watakuwa chachu kwa wenzao kujifunza.
Amesema
serikali imeamua kuwapatia vifaranga vya kuku 540, pamoja na vyakula vya mwezi
mmoja, chanjo, vilishio na vinywesheo ambapo msaada huo umegharimu Shilingi
milioni 6.1
Kwa
mujibu wa Bw. Bura, mpango kabambe wa miaka 15 wa kuendeleza sekta ya
mifugo umeonyesha kuwa kutakuwa na upungufu wa nyama unaokaridiwa tani ya
zaidi ya 100,000 ifikapo mwaka 2022 kadri kipato cha wananchi
kinavyoongezeka.
“Tumeona
huu upungufu wa nyama tunaweza kuufidia katika ufugaji wa kuu ambapo ndani ya
miezi 2 au 3 nyama inapatikana, ndiyo maana serikali imeamua kuongeza nguvu na
kuchukua hatua za uhamasishaji zaidi kwa vikundi vya vijana.
Ameongeza
kuwa hatua nzuri ya kuigwa kwa vijana hao kujihusisha na ufugaji ili kuondokana
ile dhana ya kuwa mchakato huo unafanywa na wazee na watu waliostaafu.
Amesema
wameanzia Mkoa wa Dar es Salaam, kisha watakwenda wilayani Mkuranga , mikoa ya
Mbeya , Morogoro na Dodoma akisema ni mchakato endelevu wa kutoa vifaranga kwa
vikundi vya vijana wajasiriamali.
Sarah
Urio ambaye ni msambazaji wa viranga hivyo kutoka kampuni ya AKM
Glitters, amewashukuru vijana kwa kuonyesha utayari na uthubutu wa kufuga kuku,
akisema licha ya kupewa vifaranga hivyo lakini uongozi wa kampuni hiyo utakuwa
bega kwa bega kwa kuwapa elimu ya namna ya kuendeleza mchakato huo.
“Tukishawapa
vifaranga na mahitaji husika hatutawaacha bali tutaendelea kutoa
ushirikiano katika mchakato huu. Tutawasimamia mwanzo hadi mwisho ili wafuge
kwa ufanisi,” alisema
Bi.
Leah Tesha ambaye anaunda kikundi hicho ameishukur serikali kwa kuwapatia
vifaranga hivyo akisema wametimiza ahadi yao na kwamba kuku hao itakuwa kama
ajira kwao kwa sababu suala hilo limekuwa changamoto hivi sasa.
Amesema
wameamua kuthubutu kwa kuandaa mpango mkakati waliouwasilisha katika
ofisi ya katibu mkuu wa wizara namna walivyojipanga katika mchakato wa ufugaji
wa kuku.
“Sisi
tumeonyesha njia ni fursa kwa vijana wengine wanaotembea na bahasha mkononi
wajitokeza kufuga kuku. Sisi ni mfano vijana wenzetu wanaweza kuiga na kuachana
na ile dhana wote lazima tupate kazi.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo na Usalama wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi akimkabidhi Bi. Leah Tesha vifaa kwa jili ya Salma Chihota vifaranga vya kuku.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo na Usalama wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi akimkabidhi Bi. Salma Chihota vifaranga vya kuku.
Picha ya baadhi ya vifaranga vilivyokabidhiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Bi. Leah Tesha mmoja wa vijana katika kikundi cha wajasiriamali wa kuku ili kuhamasisha vijana kujikita katika ufugaji huo
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...