Na Woinde Shizza, Arusha
WATU wawili wamefariki dunia kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha kwa siku tatu mfululizo katika wilaya ya Arumeru huku nyumba zaidi ya 50 kuharibika kutokana na mvua hizo.
Akitoa taarifa za hali ya mwendendo wa mvua hizo mara baada ya kufanya ziara na kushiriki shughuli za uokoaji, Mkuu wa wilaya ya Arumeru Jery Muro amesema kuwa mvua hizo zimeleta madhara makubwa kwani zimesababisha vifo vya watu wawili ambao wamefariki dunia leo Alhamisi April 23 Katika Halmashauri ya Meru mkoani Arusha.
Muro amewataja waliofariki dunia kutokana na mvua hizo kuwa ni Terevaeli Mirisho Nasari Mwenye umri wa miaka 65 Mkazi wa kitongoji cha meto kijiji cha mulala kata ya songoro, ambapo amefariki dunia Asubuhi baada ya maporomoko ya Udongo kutoka mlimani kuvunja ukuta wa chumba alichokuwa amelala na tayari mwili wake umepatikana na kupelekwa katika hospitali ya Mount Meru.
Aidha ametaja kifo kingine cha mtoto alietambuliwa kwa jina la Tumaini Simon Mwenye umri wa miaka 3 wa kijiji cha Valeska Kitongoji cha Mwamko, ambae amesombwa na mafuriko ya maji wakati akiwa katika harakati za kuokolewa na Mzazi wake ambapo Mzee simon alifanikiwa kuokoa mtoto mmoja na mwingine kufariki dunia na mwili wa mtoto tumaini umepatikana na taratibu za mazishi zinaendelea.
Amebainisha Katika Mvua hizo Nyumba zaidi 50 zimeharibiwa huku zingine zikianguka kutokana na maji kuwa mengi.
Ameongeza kuwa tayari ameshaziagiza kamati za maafa zinazoongozwa na wakurugenzi wa Halmashauri za Meru na Arusha kushirikiana na wananchi katika kutoa misaada ya haraka katika familia hizo.
Amesema hiyo yote ni njia ya kuweza kunusuru familia hizo ikiwemo kuwatafuta makazi ya muda
Alitumia muda huo kutoa tahadhari ya wananchi waliojenga pembezoni mwa milima na miinuko mikubwa pamoja na wale waliojenga Katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko kuondoka katika maeneo hayo haraka kabla ya madhara zaidi maana mvua bado zinaendelea kunyesha.
Wananchi wakiangalia nyumba iliyobomoka.
Mkuu wa wilaya ya Arumeru Jery Muro akiangalia madhara yaliyojitokeza mara baada ya mvua kunyesha na kudondosha baadhi ya nyumba katika wilaya ya Arumeru.
Wananchi wa Maeneo ambayo yameathirika na mvua zinazoendelea kunyesha wilaya ya Arumeru mkoani Arusha wakiwa katika moja ya nyumba zilizopata madhara baada ya mvua kunyesha na kuleta madhara ya kuangusha nyumba.
Picha na Woinde Shizza, Arusha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...