Tanzania imesema haijalegalega wala kujitenga katika kupambana na maradhi ya COVID – 19  na badala yake imetoa uongozi madhubuti katika kuratibu na kuunda timu ya wataalamu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC kuandaa muongozo na utaratibu wa kukabiliana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kutafuta njia za kupunguza nguvu ama kuleta tiba ya COVID – 19.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi ameyasema hayo wakati akipokea msaada wa dawa inayodaiwa kutibu na kukinga ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona COVID -19 iliyotolewa na Nchi ya Madagascar kwa Tanzania. 

Prof. Kabudi ameongeza kuwa madai yanayotolewa kuwa Tanzania imelegalega ama kujitenga katika kupambana na ugonjwa wa COVID 19 si ya kweli kwa kuwa Tanzania imetoa uongozi madhubuti katika eneo iliyopewa dhamana ya uongozi ya Uenyekiti wa  nchi SADC na imeifanya na inaendelea kuifanya kwa heshima na bidii zote.

 Ameongeza kuwa Tanzania ambayo ni Mwenyekiti wa SADC tangu kuzuka kwa ugonjwa wa COVID -19 tayari imesimamia na kuratibu mikutano iliyoendeshwa kwa njia ya mtandao (Video Conferencing) kwa lengo la kukabiliana na ugonjwa huo na kutoa muongozo wa jinsi ya usafirishaji wa bidhaa muhimu na kwamba mingozo hiyo imetolewa na kukubaliwa na nchi zote wanachama wa SADC

Amesema miongoni mwa masuala waliyokubaliana katika mikutano ya SADC ni pamoja na kukubaliana kuwa kila nchi ya SADC ichangie aidha katika kutafuta njia ya kusaidia kupunguza nguvu ama kuleta tiba ya COVID – 19 na Madagascar imekuwa Nchi ya kwanza miongoni mwa nchi wanachama kupiga hatua ndani ya SADC na ndani ya Afrika na kwamba katika mkutano ujao wa SADC wataitambua Madagascar kwa mchango wake wa kupambana na Virusi vya Corona.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar Mhe. Tehindrazanarivelo Djacoba As Oliva amezitaka nchi za Afrika kuungana kwa pamoja kupata suluhisho la maradhi ya COVID 19 ambayo pia itakuwa suluhisho na faraja kwa dunia nzima.

Ameongeza kuwa kila nchi Barani Afrika inawajibu wa kutekeleza ili kuupatia ufumbuzi ugonjwa huo na ni faraja kwa Madagascar kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC kufika nchini humo kwa ajili ya kujionea dawa hiyo jambo ambalo anaamini kukiwa na nguvu ya pamoja ndani ya SADC mafanikio makubwa yatafikiwa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi wa kulia akinywa dawa ya kutibu ugonjwa wa virusi vya corona


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...