Dk Augustine Mahiga alizaliwa Agosti 28, 1945 huko Tosamanganga, Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa (atatimiza miaka 75 ifikapo Agosti mwaka huu). Amesoma elimu ya msingi katika shule za Serikali enzi ya mkoloni na alihitimu darasa la VIII muda mfupi baada ya uhuru. Safari ya elimu ya Dk Mahiga ilikuwa ya umaskini uliopitiliza, alishindwa kuendelea na elimu ya sekondari kwa kutokuwa na fedha za kulipia mashuka na mablanketi hadi aliposaidiwa na msamaria mwema kutoka Shirika la Kennedy wakati huo.

Aliendelea na masomo ya sekondari hapahapa nchini na mwaka 1968, alijiunga katika Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki, Dar es Salaam na kuhitimu Shahada ya Sanaa akibobea kwenye elimu mwaka 1971.

Mwaka huohuo, Dk Mahiga alipata ufadhili na kuendelea na masomo ya juu nchini Canada katika Chuo Kikuu cha Toronto ambako alihitimu Shahada ya Uzamili. Aliendelea na masomo ya Shahada ya Uzamivu (PhD) katika chuo hichohicho akijikita katika Uhusiano wa Kimataifa na kuhitimu mwaka 1975.

Mwaka huohuo 1975 (akiwa na miaka 30), Dk Mahiga alirejea nchini akiwa daktari wa falsafa kitaaluma na alipangiwa kazi ya kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwa mhadhiri katika Idara ya Kimataifa na Ushirikiano wa Kikanda. Alifanya kazi hiyo hadi mwaka 1977 alipohamishiwa katika Ofisi ya Rais kuwa Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo na alidumu hapo akifanya kazi pamoja na Mwalimu Julius Nyerere hadi mwaka 1980.

Kati ya mwaka 1980 hadi 1983, Dk Mahiga alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa. Nafasi hii aliitumikia kwa weledi mkubwa katika historia ya watu waliowahi kuitumikia, aliweza kuifahamu nchi vizuri na mifumo yake kwa mtizamo wa ndani na nje.

Mwaka 1989 hadi 1992, aliteuliwa kuwa mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Kimataifa akifanyia kazi Geneva, Uswisi na mwaka 1992 hadi 1994, Balozi Mahiga aliteuliwa kuwa Kiongozi (Mwakilishi) wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi duniani (UNHCR) mjini Monrovia, Liberia na huu ndiyo wakati aliponusurika kuuawa na Majeshi ya Rais Charles Taylor, kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe. Kuna wakati akiwa katikati ya operesheni ya wakimbizi hapo Monrovia, Serikali ya Tanzania ilimteua kuwa Balozi na kumuongezea jukumu jingine zito.

Mwaka 1994 -1998, Balozi Mahiga alihudumu akiwa Mratibu na Mkurugenzi Msaidizi wa Operesheni ya Dharura ya Ukanda wa Maziwa Makuu akifanyia kazi hiyo kutokea Geneva, Uswisi na kati ya mwaka 1998 - 2002 aliteuliwa kuwa Kiongozi Mkuu (Mwakilishi) wa Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR) huko mjini Delhi India kabla ya kuteuliwa tena kuwa mwakilishi wa shirika hilo katika nchi za Italia, Malta na Jamhuri ya San Marino kati ya mwaka 2002 - 2003.

Balozi Mahiga amepata pia kuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika kipindi cha mwaka 2003 hadi 2010 na alishiriki kikamilifu katika mipango ya kimataifa pamoja na kusimamia mazungumzo ya kuanzishwa kwa Kamisheni ya Ujenzi wa Amani (mwaka 2005). Pia kushiriki kwenye masuala ya maingiliano ya serikali mbalimbali na makundi yanayofanya kazi zisizo rasmi, maendeleo, amani, usalama na ujenzi wa ushirikiano wa uhakika kati ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Balozi Mahiga alirejesha heshima ya Tanzania hadi kuwa mojawapo ya nchi zilizounda Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi yetu ilipopata heshima hiyo, yeye aliteuliwa kuwa mkuu wa ujumbe wa Tanzania katika Baraza hilo, hii ilikuwa ni mwaka 2005.

Mwaka 2015 mwezi Disemba, Rais Magufuli alimteua Balozi Mahiga kuwa Mbunge na baadae kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Naibu wake akiwa Dr Suzan Kolimba.

Machi 03, 2019 Rais Magufuli alimhamisha Wizara na kumteua kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, nafasi aliyoitumikia hadi mauti yanamkuta.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...