Na Mwandishi wetu Mufindi
Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali
Dkt. Richard Sambaiga ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kisrikali kuhakikisha
miradi wanayoifanya inawaongezea tija wananchi badala na kufadhili miradi
isiyoweza kusababisha maendeleo bayana kwa walengwa.
Dkt. Sambaiga ameyasema hayo Wilayani Mufindi, Iringa wakati
akikagua utekelezaji wa miradi ya kilimo, ufugaji na mpango wa matumizi bora
ya ardhi inayofanywa na Shirika la PELUM Tanzania katika vijiji vya
Kipanga na Lilongole.
"Kuna umuhimu kwa hawa wananchi wanaofanya kilimo au
ufugaji wafanye kwa namna ambayo itawaongezea tija, kuliko kuona
wanatumia nguvu nyingi lakini tija kidogo" alisema Dkt. Sambaiga.
Amesisitiza mwenendo wa mashirika kuripoti kazi walizofanya na
kufanikiwa, ziendane na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi ili miradi hiyo
iwe mfano na kuhamasisha wengine kujiunga.
"Tuongeze vipengele vya kuwezesha utaalamu wa kilimo na
ufugaji uwe wa kisasa ili kuongeza tija na miradi hiyo iwe ni mfano"
Naye Msajili wa Mashirika yasiyo Ya Kiserikali, Vickness
Mayao ameyataka mashirika hayo kutoa taarifa mara kwa mara kwa wananchi kuhusu
kazi zao na kuboresha majukumu wanayoyafanya.
"Bado tunahimiza mashirika kutekeleza majukumu yao kwenye
eneo walilosajili, wanaweza kuongeza thamani ya miradi yao bila kuathiri lengo
lao" amesema Mayao.
Akiwasilisha taarifa ya mradi huo, Mratibu wa shirika hilo
Donati Senzia amesema, shirika kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya
Mufindi, inatarajia kupima mashamba zaidi ya 500 ili wananchi hao wapewe hati
na ardhi ili kuwanufaisha kiuchumi.
"Tuliona kwenye mradi huu tusiishie tu kupima bali
tuangalie ardhi itawanufaishaje wananchi kiuchumi hasa kwa akina mama"
amesema Senzia.
Naye Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Simon Mbago
amesema wanashirikiana na mashirika mbalimbali kuhakikisha wananchi wananufaika
na ardhi kwa kuwapimia na kubainisha matumizi ya ardhi.
Baadhi ya wanufaika wa vijiji hivyo wameelezea kufurahishwa
kwao na PELUM hususani kupata elimu ya kumiliki na kuitumia ardhi kwa manufaa
na kupunguza migogoro ya ardhi kwa kiwango kikubwa.
Hata hivyo, wananchi wengi waliomba Serikali kwa kushirikiana na
NGOs kuwasaidia kutatua kero ya Barabara na maji ili kuwawezesha kujikita
katika Kilimo.
"Kipaumbele kwetu ni barabara kwani hata haya mazao hatuwezi
kuyafikisha kwenye masoko barabara yetu inapitika katika msimu mmoja tu, wakati
wa mvua hatuwezi kufika mjini", alisema mmoja wa wanakijiji.
Ziara ya ukaguzi wa kazi za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
inakusudia katika kujirishisha dhidi ya taarifa za Mashirika zinazowasilishwa
katika Ofisi ya Msajili, taarifa za wafadhili pamoja na kujiridhisha na thamani
halisi ya fedha zilizotumika katika maeneo ya mradi.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Dkt. Faustine Sambaiga
akizungumza na wanakijiji wa Ilogombe, Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa katika
kikao cha pamoja na wanufaika wa miradi ya kilimo na mifugo inayotekelezwa na
shirika la PELUM Tanzania wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi
ya mashirika yasiyo ya Kiserikali.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Dkt. Faustine Sambaiga
akiangalia ubao unaoonesha upimaji wa maeneo na matumizi ya ardhi katika kijiji
cha Kipanga, Wilayani Mufindi, Mkoa wa Iringa. Mradi wa elimu ya matumizi bora
ya ardhi unatekelezwa na shirika la PELUM Tanzania. Kushoto ni Msajili wa
Mashirika yasiyo ya Kiserikali
Vickness Mayao.
Wanufaika
wa miradi ya kilimo na mifugo katika vijiji vya Kipanga na Ilogombe
wakimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali
Dkt. Faustine Sambaiga katika kikao cha pamoja alipotembelea vijiji hivyo
kukagua miradi inayotekelezwa na shirika la PELUM Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...